Halmashauri ya manispaa ya Kinondoni yaanza kutekeleza zoezi la bomoa bomoa ya nyumba zote zilizojengwa kinyume cha sheria katika meneo ya mabondeni.
Wizara ya ardhi nyumba na maendeleo ya makazi imeendesha zoezi la bomoa bomoa kwa kubomoa nyumba zilizojengwa kinyume na sheria katika eneo la bonde la Msimbazi jijini Dar es Salaam.
Wakazi wa maeneo ya mto Msimbazi wilayani Kinondoni leo hii wakumbwa na bomoabomoa ya serikali kufuatia kukiuka agizo la serikali la kuwataka wahame maeneo hayo.
Serikali imeanza kuchukua tahadhari ya mvua zilizoanza kunyesha mwezi huu kwa kubomoa nyumba na kuondoa watu wanaoishi mabondeni.
Nyumba zilizojengwa eneo la Mto Msimbazi Magomeni Mkwajuni, Dar es Salaam zikiwa zimevunjwa jana. Picha na Salim Shao
By Mwandishi Wetu
Dar es Salaam. Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi jana ilitekeleza shughuli ya ubomoaji nyumba zilizojengwa kwenye Bonde la Mto Msimbazi na kusababisha vilio na huzuni kutoka kwa wakazi na wamiliki wake.
Nyumba zaidi ya 100 zilizojengwa kwenye bonde hilo zilibomolewa na maofisa wa wizara hiyo pamoja na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira Tanzania (NEMC) na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni walisema mkakati wao ni kubomoa zaidi ya nyumba 400 zilizojengwa kwenye eneo hilo.
Kulikuwa na ulinzi mkali wa askari polisi wenye silaha mbalimbali zikiwamo bunduki za moto pamoja na mabomu ya kutoa machozi wakati wa ubomoaji nyumba hizo na kuwaacha wamiliki wakihangaika kusalimisha mali zao.
Wakizungumzia hatua hiyo, baadhi ya wakazi wa eneo hilo waliilalamikia Serikali kwa madai kuwa hawakuwa na taarifa za ubomoaji huo kwenye eneo lao na kusababisha wengine kushindwa kuokoa mali zao.
Mkazi wa eneo hilo, Julius Michael alisema ubomoaji huo umefanywa kwa kushtukiza akidai kuwa walishangaa kuona tingatinga linafika na wao kupewa amri ya kuondoka.
“Hakuna aliyejua kama leo (jana) wangekuja kutuvunjia nyumba. Siyo kama tumekataa kuhamia Mabwepande tunacholaumu ni hatua ya kuja bila kutuambia,” alisema Michael.
Kulwa Omega alisema hajui ataelekea wapi na familia yake, baada ya nyumba waliyokuwa wakiishi kukumbwa na bomoabomoa hiyo.
Mkuu wa Kitengo cha Sheria cha NEMC, Manchale Heche aliwataka wananchi waliojenga kwenye maeneo hayo, ambao hawajafikiwa kuanza kuondoka mapema.
Alisema ubomoaji huo ulioanzia eneo la Mkwajuni, Manispaa ya Kinondoni utaendelea hadi kwenye maeneo mengine ambako nyumba zimejengwa kinyume cha taratibu.
“Baada ya kusafisha eneo hili tutahamia kwa waliojenga kuzunguka Mto Kizinga, Mbagala na baadaye jiji zima la Dar es Salaam kabla hatujahamia mikoani,” alisema. “Ni shughuli endelevu na kila anayejiona amejenga eneo lisiloruhusiwa kisheria ni vizuri akahama mapema.”
Ofisa Mipango miji wa Manispaa ya Kinondoni, Dk Charles Mkalawa alisema zaidi ya nyumba 100 zitabomolewa katika Mtaa wa Hananasifu wakati nyumba 300 ni za Magomeni.
No comments :
Post a Comment