Rais John Magufuli
Dar es Salaam. Licha ya mawaziri wa Serikali ya Awamu ya Tano kutokaa ofisini wakishughulikia matatizo ya wananchi, wasomi bado wana shaka kuwa huenda kasi waliyoanza nayo ni ya muda na kwamba baadhi yao wanafanya kwa nidhamu ya woga.
Tangu walipoapishwa Desemba 12, mawaziri wengi wamekuwa wakitembelea taasisi zilizo chini yao kufuatilia utendaji na utoaji huduma kwa wananchi na kutoa matamko.
Mathalan, mara baada ya kuapishwa, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na naibu wake, Hamisi Kigwangalla hawakwenda ofisini na badala yake mmoja alikwenda Hospitali ya Amana na mwingine Hospitali ya Mwananyamala kukagua utoaji huduma.
Ziara kama hizo zilifanywa na mawaziri wengi, ambao walifika sehemu zinazowahusu na kuhoji masuala kadhaa na baadhi kutoa muda ili wapewe majibu, wengine wakitangaza kusimamisha watendaji au kusitisha zabuni.
Lakini wachambuzi waliohojiwa wametilia shaka kasi hiyo, baadhi wakisema mawaziri hao walihitaji kupata ripoti kutoka ofisi zao kabla ya kuanza ziara za ufuatiliaji na wengine wakienda mbali zaidi kusema kuna dalili za kutaka waonekane wanafanya kazi.
“Kufanya kazi siyo kwenda mbio na kutoa maagizo lukuki kwa wakati mmoja. Kinachofanyika sasa ni kufuata maagizo zaidi kuliko utendaji wa dhati. Hali hiyo ipo katika ngazi zote na inasababisha baadhi ya watendaji kukiuka Katiba na sheria za nchi,” alisema mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Hamad Salim. Msomi huyo alisema nchi haihitaji mtu kujionyesha kuwa anafanya kazi. “Anayefanya kazi anatakiwa kutambuliwa na watu wanaomzunguka.”
Katika kutekeleza kauli mbiu ya Rais John Magufuli ya “hapa kazi tu”, mawaziri wamekuwa wakifanya ziara hizo za ‘kushtukiza’ wakiwa wameambatana na waandishi wa habari na kuwahoji watendaji wa Serikali kuhusu utekelezaji wa majukumu yao.
Wakati Mwalimu na Kigwangalla walianzia hospitalini, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na naibu wake Dk Medard Kalemani wameanza kazi kwa kutembelea vituo vinavyozalisha umeme kwa kutumia maji.
Muhongo, ambaye alishughulikia madini na nishati kwenye Baraza la Mawaziri la Serikali ya Awamu ya Nne kabla ya kujiuzulu mapema mwaka jana, alitumia fursa hiyo kueleza mikakati yake na kutoa maagizo kuwa kila mteja aliyeomba kuunganishiwa umeme na hahitaji nguzo, afanyiwe hivyo.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Makame Mbarawa akikutana na wadau wa maji, kutembelea Ruvu pamoja na Dawasa.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga alianzia ofisini kwake akipokea taarifa ya ndani na juzi alikuwa na kikao na maofisa wa polisi huku akiwataka kutoa taarifa za sababu ya Jeshi la Polisi kutolinda Bandari ya Dar es Salaam, kazi inayofanywa na kampuni binafsi.
Naye Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Utumishi, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jaffo alikuwa wilayani Bahi ambako alikutana na tatizo la utoro wa watendaji wa Halmashauri ya Bahi.
Tofauti na mawaziri wengine walioamua kufanya ziara za kushtukiza, Mwigulu Nchemba anayeongoza Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, alilazimika kusafiri kwenda Mvomero, Morogoro baada ya kutokea mapigano kati ya wakulima na wafugaji, yaliyosababisha mtu mmoja kufariki, wanne kujeruhiwa na ng’ombe 72 kuuawa.
Lakini alipofika huko aliahidi kushughulikia matatizo ya wakulima na wafanyakazi huku akiwaomba wananchi hao waache kujichukulia sheria mkononi.
Jenister Mhagama, ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, pia alilazimika kutoka ofisini baada ya mvua iliyonyesha kwa kipindi kisichozidi saa nne, iliposababisha mafuriko jijini Dar es Salaam.
Waziri huyo aliagiza kusitishwa kwa zabuni ya mkandarasi wa mfereji wa Buguruni na kutaka maelezo ya ujenzi wa mfereji wa Boko Basihaya.
Wanatumia nguvu nyingi
Lakini wachambuzi wanaona kuna nguvu kubwa inatumika ambayo inaweza kutoa matokeo madogo.
“Mtu akipewa kazi ya kukata mti mkubwa, atakaa siku sita mezani akipanga jinsi ya kuukata,” alisema mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (Sua), Profesa Damian Gabagambi, akimnukuu Rais Barack Obama wa Marekani.
“Utendaji wa kulipuka utatumia nguvu nyingi na kuleta matokeo madogo kwa sababu maeneo yanayohitaji kurekebishwa na kufanyiwa kazi ni mengi na yanahitaji upeo wa kina kuyafahamu, kwanza kwa kushirikisha wataalamu na wadau ili kujadili na kupata ufumbuzi wa pamoja,” alisema Profesa Gabagambi.
Lakini mtaalamu wa mambo ya Katiba, Profesa Ruth Meena alionyesha shaka kama utendaji huo ni nidhamu ya kazi au ya woga.
“Kuna vitu viwili; nidhamu ya kazi na nidhamu ya woga, hivyo inahitaji muda kulibaini hilo. Siwezi kusema mengi kuhusu utendaji kazi unaoonyeshwa na walioteuliwa kwa sababu siamini katika vitu vya mbiombio na tabia ya mtu ya kupenda kazi huonekana bayana, muda utaeleza yote.
“Wapewe muda na mimi nawapa muda pia tuone. Wenye nidhamu ya woga na nidhamu ya kazi wataonekana tu, hawatajificha.”
Mhadhiri wa OUT, Hamad Salim alisema mawaziri hao wanafanya kitu ambacho hakitokani na utashi wao, bali kuiga uchapakazi wa Rais.
“Nafikiri tunahitaji kubadili sheria na taratibu mbalimbali ili kuendana na mfumo uliopo wa kuchapa kazi. Kinachofanyika sasa si sawa. Lakini wasaidizi wa Rais hawafanyi kazi kwa utashi, wanafanya kwa amri na kuimba wimbo wa mtu mwingine wakijiaminisha kuwa ni wimbo wao.”
Hoja ya mfumo pia ilizungumziwa na Profesa Bakari Mohammed wa UDSM: “Ili kuwe na utendaji kazi endelevu, tunatakiwa kuwa na mifumo itakayofanya utendaji kazi wa kasi walioanza nao uendelee hata kama Rais Magufuli ataondoka madarakani,” alisema.
Alisema yanatakiwa mabadiliko ya sheria na kanuni na kuwe na Katiba yenye maelezo ya utendaji kazi wa mawaziri.
Alisema hata Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete naye alianza na kasi kubwa, lakini kutokana na utendaji kazi kutokuwapo kimfumo, ilifikia mahali kasi ikashuka na kuwa ndogo.
No comments :
Post a Comment