Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, December 13, 2015

Safu hii ya Rais Magufuli ilete mabadiliko ya kweli

NA MHARIRI

13th December 2015.

Maoni ya Katuni
Hatimaye Rais, Dk. John Magufuli aliwaapisha mawaziri pamoja na manaibu mawaziri 34  jana katika Ikulu ya Dar es Salaam baada ya kuwateua siku mbili kabla, sherehe za kuwaapisha mawaziri hao zilishuhudiwa na waandishi wa habari pamoja na viongozi wengine wa kitaifa wakiwamo Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Wananchi nchini kote walikuwa katika subira ya hamu ya kujua Rais Magufuli amewateua mawaziri gani ambao wataisaidia serikali kutimiza majukumu mazito ya kuwaletea maendeleo ya kweli  kwa Watanzania.

Kutokana na orodha ya safu ya mawaziri pamoja na manaibu walioteuliwa, ni dhahiri  kuwa Rais amewatambua na kuwaamini kuwa watatekeleza majukumu yao kwa kiwango kikubwa, ni kutokana na ukweli kwamba wengi kati ya hao hawana historia ya kujihusisha na ubadhirifu, ufisadi, wala tuhuma za rushwa.

Ni safu ya wachapa kazi ambao hata baada ya kutahadharishwa wasifanye sherehe baada ya kuteuliwa, bado wameendelea kuonyesha dhati yao ya kuitumikia serikali na watu wake baada ya kula kiapo cha utii mbele ya Rais Magufuli.

Zipo hatua kubwa na zinazoonyesha mafanikio ya uwajibikaji wa serikali, ambazo tayari zimekwisha fanywa na Rais Magufuli pamoja na Waziri Mkuu hata kabla ya mawaziri hawajateuliwa, fedha nyingi zinazokadiriwa kufikia bilioni 10.6/- zimeokolewa katika operesheni ya kuwabana wakwepa kodi katika bandari ya Dar es Salaam, na zaidi ya watuhumiwa 40 tayari wamewekwa mbaroni wakifanyiwa uchunguzi.

Mawaziri walioapishwa jana, wameshuhudia namna kasi ya utendaji wa Rais Magufuli pamoja na Waziri Mkuu Majaliwa ilivyokuwa kwa kipindi kifupi tangu alipoapishwa kushika madaraka mwanzoni mwa mwezi Novemba mwaka huu.

Tunaamini kuwa safu ya uongozi iliyopo, itakuwa na majukumu makubwa ya kuhakikisha vita dhidi ya maadui wakubwa waliotangazwa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu, rushwa, ufisadi, ubadhirifu wa aina yoyote vitakuwa ajenda ya kwanza ya mapambano kwenye awamu hii ya tano ya Rais Magufuli.

Ni dhahiri kuwa vita hivyo vikipiganwa vizuri, mafanikio yake yatakuwa na faida kubwa kwa Watanzania, huduma bora za elimu, afya, ajira kwa vijana, miundombinu pamoja na ustawi wa wananchi wote utatafsiriwa vyema kutokana na uchumi utakaokuwa umeboreka.

Ni imani yetu kuwa matarajio makubwa ya wananchi ya kuona mabadiliko ya kweli ya maisha yao yatategemea ushirikiano mkubwa wa mawaziri walioapishwa jana, wanatakiwa kutoa ushirikiano wa dhati kwa Rais, Makamu wa Rais,  Waziri Mkuu pamoja na viongozi wengine waandamizi.

Mawaziri wapya wanategemewa kusimamia kidete operesheni ya kuziba mianya ya utoroshaji na ukwepaji wa kulipa ushuru wa mapato ya serikali pamoja na kutenda kazi kwa uadilifu mkubwa wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Pamoja na majukumu makubwa yaliyopo mbele ya Baraza hilo la mawaziri, tuna imani kuwa serikali itatekeleza ahadi zake zilizomo ndani ya ilani ya CCM kwa awamu ili kuipeleka nchi mbele kiuchumi, tunaamini kuwa yote yanawezekana ikiwa kila mwananchi atatimiza wajibu wake wa kufanya kazi.   
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments :

Post a Comment