UAMUZI wa kuondoa majukumu ya kushughulikia mizigo kutoka menejimenti ya Bandari ya Dar es Salaam (TPA) na kuyakabidhi kwa kamati ya watu watano, imebainika kuwa chanzo cha upotevu wa mankotena na kuisababishia Serikali hasara ya mabilioni ya shilingi.
Inadaiwa kuwa timu hiyo ya watu watano ilishindwa kutekeleza majukumu yaliyokuwa yakifanywa na menejimenti ya Bandari ya Dar es Salaam na kutoa mwanya uliochangia upotevu.
Uchunguzi wa MTANZANIA umebaini kuwa aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa TPA, ambaye hivi sasa ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, Mhandisi Madeni Kipande, alimwandikia barua Mkurugenzi wa Utumishi, Februari 5, mwaka 2013, yenye maelekezo hayo.
Katika Barua hiyo yenye kumbukumbu namba DG/3/3/06, yenye kichwa cha habari “KUSIMAMIA TICTS, ICD’s na CFS, ilibatilisha majukumu ya Bandari ya Dar es Salaam na kuyakabidhi kwa timu ya watu watano.
Barua hiyo ya Kipande inasomeka; “TPA ina wajibu wa kimkataba wa kusimamia vitengo tajwa hapo juu kwa nia ya kuboresha utendaji na kuongeza tija TPA.
“Kwa muda wote tangu vitengo hivi vianzishwe kazi hii imekuwa ikifanywa na Dar es Salaam Port, hata hivyo kutokana na sababu kama vile:
(I). Kuipunguzia mzigo Bandari ya Dar es Salaam
(II). Kuondoa mgongano wa kimasilahi kati ya Dar es Salaam Port na vitengo hivyo ambavyo kimsingi wanafanyakazi za aina moja. (III). Kuongeza ufanisi katika ufuatiliaji, utendaji na kukusanya mapato.
“Menejimenti imeamua kwamba kazi hii sasa isimamiwe na kamati maalumu ya wataalamu kutoka idara za makao makuu.
“Suala hili litafanywa na idara za Ulinzi, Fedha, Teknohama, Utekelezaji na Huduma za Kisheria za Makao Makuu. Pamoja na mambo mengine, majukumu yao muhimu yatakuwa:
“(I). Kuhakikisha kuwa TPA inapata fursa ya kuhakiki mifumo ya ICT uthibiti wa makontena yote yanayopokelewa na ulipaji tozo. (II). Kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mikataba kati ya TICTS na Serikali. (III). Kuhakikisha kuwa “State Police & Security” wanapewa fursa ya kusimamia masuala ya ulinzi na usalama wa Bandari yote. (IV). Usimamizi wa utunzaji wa mazingira unaozingatia masharti na taratibu zilizoainishwa kimataifa.”
Utekelezaji wa maagizo:
Baada ya maagizo hayo, Februari 19, mwaka 2013, Mkurugenzi wa Utumishi wa TPA aliwaandikia wateule hao watano barua yenye kumbukumbu namba HR/1/2/30, yenye kichwa cha habari “KUSIMAMIA TICTS, ICD’s na CFS.”
Wateule hao ni Mkurugenzi wa Ulinzi, Mkurugenzi wa Fedha, Mkurugenzi wa Teknohama, Mkurugenzi wa Utekelezaji na Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria.
Sehemu ya barua hiyo ilisema. “Kaimu Mkurugenzi Mkuu amewateua kuunda kamati maalumu ya wataalamu ili kutekeleza wajibu wa TPA wa kimkataba wa kusimamia vitengo vilivyotajwa hapo juu kwa nia ya kuboresha utendaji na kuongeza tija,” ilisema barua hiyo.
Massawe atengua uamuzi wa Kipande:
Baada ya kuteuliwa kuwa Kaimu Mkurugenzi wa TPA Februari 16, mwaka huu na baadae kuwa Mkurugenzi Mkuu, Awadh Massawe, ambaye uteuzi wake ulitenguliwa siku kadhaa zilizopita na Rais Dk. John Magufuli, Agosti 10, mwaka huu alitengua uamuzi wa Kipande baada ya kubaini kuwapo usimamizi mbovu.
Katika barua yake ya Agosti 15, mwaka huu kwa Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam yenye kumbukumbu namba DG/4/3/02, pamoja na mambo mengine Massawe alisema; “Itakumbukwa kwamba katika waraka huo ilielekezwa kuwa jukumu la usimamizi wa shughuli za siku hadi siku za kiutekelezaji katika vituo hivyo utafanywa na kamati maalumu ya makao makuu.
“Moja ya majukumu ya kamati hiyo maalumu ilikuwa ni kuongeza ufanisi katika ufuatiliaji, utendaji na kukusanya mapato. Katika kufuatilia utendaji katika vituo hivyo imegundulika kuwa kamati iliyoteuliwa ikihusisha Mkurugenzi wa Fedha, Mkurugenzi wa Teknohama, Mkurugenzi wa Utekelezaji, Mkurugenzi wa Sheria na Mkurugenzi wa Ulinzi haikutimiza majukumu yake kama ilivyokusudiwa.
“Kutokana na hali hiyo, ofisi yako inaelekezwa kuendelea mara moja na usimamizi wa vituo hivyo ikiwamo kusimamia shughuli zote za kiutekelezaji makusanyo na mapato na shughuli nyingine zote za kiutendaji kufuatana na mikataba iliyopo.
“Inasisitizwa kwamba kwa sasa makao makuu itahusika na masuala ya kisera na ushauri wa kisheria katika kusimamia vituo hivyo.”
Mapato ya TPA
Mamlaka ya Bandari Tanzania ina majukumu ya kusimamia na kukusanya mapato ya aina tatu, huku shughuli nyingine zote za ukusanyaji mapato bandarini zikifanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Aina ya kwanza ya mapato inaitwa (Stevedoring), ambayo ni mapato yanayotokana kupakuliwa mzigo kutoka kwenye meli na kuwekwa nchi kavu.
Aina ya pili ni (Shore handling) ambayo mapato yatokanayo kutoa mzigo uliopakuliwa kutoka melini na kuupeleka sehemu ya kuhifadhi (yard).
Ambapo aina ya tatu ni (wharfage), ambayo ni gharama inayolipwa kutokana na thamani ya mzigo, ambapo mteja hutakiwa kuwasilisha nyaraka za mzigo (bill of landing), ambapo katika hatua hiyo taratibu za TRA hufuata.
Kauli ya Kipande
Alipoulizwa kwa njia ya simu, Mhandisi Kipande alisema; “Sina ufafanuzi wowote ule wa kutoa, andika unachotaka,” kisha alikata simu.
Dakika chache baadae alituma ujumbe mfupi wa maandishi unaosema. “Kikiandikwa kitu ambacho si kweli ni mahakamani tu sina simile endeleeni kutetea majizi,” alisema.
Massawe azungumza
Kwa upande wake, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa TPA ambaye uteuzi wake ulitenguliwa na Rais Magufuli, Masawe alisema kwa sasa hana mamlaka yoyote kuzungumzia masuala ya taasisi hiyo.
“Rais ambaye ni mkuu wa nchi ameshatoa maamuzi, sasa sidhani kama ni busara kuzungumzia masuala ya bandari, kwa hiyo sina la kusema,” alisema Massawe.
Novemba 27, mwaka huu Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alifanya ziara TPA na kubaini upotevu wa makontena 329 huku Desemba 4 akifanya ziara nyingine na kubaini upotevu wa makontena 2,387.
“Ziara yangu ilinipitisha hatua zote za upitishaji mizigo ambazo pia kwa mujibu wa taarifa ya uchunguzi wa ndani wa tarehe 30 Julai 2015, tuligundua kuwepo kwa mianya mingi ya ukwepaji wa kodi ikiwamo na makontena 2,387 yaliyopitishwa kati ya Machi na Septemba 2014 kinyume cha taratibu.
“Vitendo hivi vinaonyesha kuwa bandari yetu hupitisha makontena mengi bila ya kulipiwa kodi na hakuna hatua yoyote inayochukuliwa, upotevu huo unaenda sambamba na mfumo usiokidhi wa kupokea malipo ambao unatoa mwanya mkubwa wa kupoteza mapoto ya Serikali,” alisema Majaliwa.
Alisema ripoti ya TPA iliadhibu watu wa ICD tu lakini yeye amesimamisha na wale viongozi wa sekta iliyoruhusu makontena kwenda bandari kavu, kwa kuwa ufisadi huo ulifanywa kwa maofisa hao kushirikiana.
Alisema wakuu hao wa vitengo wamechukuliwa hatua kwa kuwa wao ndiyo wahusika wakubwa wa kutoa makontena hayo bandarini na walikuwa na nafasi ya kujua kila kitu kilichokuwa kikiendela ICD, lakini walishindwa kubaini kilichotokea.
No comments :
Post a Comment