Hivi inawezekana mtu mmoja akawaletea maendeleo Watanzania zaidi ya milioni 45?
Mwandishi maarufu, Walter Rodney katika kitabu chake kiitwacho ‘How Europe underdeveloped Africa’ aliandika kuwa tatizo na chanzo kikubwa cha matatizo ya Afrika ni uongozi.
Uongozi katika nyanja za mabadiliko na maendeleo ni kila kitu. Ukweli ni kuwa sehemu yenye maendeleo nyuma yake kuna kiongozi, vivyo hivyo sehemu isiyo na maendeleo yupo kiongozi pia.
Kwa kuzingatia ukweli huu, ndipo tunapopata kada mbili za viongozi, yaani viongozi bora na bora viongozi.
Kada ya pili ndiyo anayoizungumzia Roodney. Hawa kwa hakika ndiyo sababu ya bara la Afrika kuwaka moto kwa matatizo tena ya kujitakia
karibu kila kitu cha ovyo Afrika chanzo chake ni kuwapo kwa watu hawa waitwao bora viongozi. Hawa si Afrika pekee, pia wapo katika mabara ya Asia na Latin America.
Viongoz hawa wamekuwa chanzo halisi cha ubadhirifu wa rasilimali za umma, uchu wa madaraka, ubinafsi, uchoyo na chanzo cha vita. Vitu vyote hivi vinasababisha vifo na umasikini mkubwa kwa Waafrika.
Kundi la pili ni hawa viongozi bora ambao ni nadra kuwapata katika nchi za Kiafrika, kama waliokuwapo basi ni enzi zile za kina Mwalimu Julius Nyerere, Patrice Lumumba na wenzao.
Hata hivyo, katika ukanda wa Afrika Mashariki, kuna nyota imeanza kuchomoza.
Rais John Magufuli ameanza kuonyesha kuwa anaweza kuwa miongoni mwa viongozi wenye dira, uzalendo, uadilifu katika bara hili la Afrika.
Unaweza kusema ni mapema kumtathmini katika kipindi kifupi alichokaa madarakani, lakini tukumbuke maandiko ya Biblia yasemayo: ‘’acha kuupuuzia ishara ndogo’’
Kwa wanaojua saikolojia hasa jinsi ya kumsoma mtu, namna Magufuli anavyozungumza na ishara yake ya mwili, utagundua kuna uhusiano wa karibu na ukizidi kuwa na utambuzi, basi utaelewa anayoyasema yanatoka katika sakafu ya moyo wake.
Kwa hakika nchi hii ilishafanywa “shamba la bibi” kila mtu kwa manufaa yake binafsi alifanya Tanzania sehemu ya kujinufaisha bila kujali masilahi ya Taifa
Kasi ya Magufuli ni nzuri, ingawa bado wengi wanaona kasi yake kama ni jeshi la mtu mmoja, ila katika watu wanaoamini mabadiliko yanaletwa na yanaanza na mtu mmoja, ni mimi.
Kama mwanahistoria mchanga nimesoma historia ya dunia inayoonyesha mapinduzi mengi ya kijamii hayakufanikiwa kwa asilimia kubwa.
Vita anayopambana nayo Magufuli si ndogo; anapambana na mfumo ulioota mizizi, hivyo kilichopo ni ama aumalize mfumo au mfumo ummalize yeye.
Ndiyo maana nasema anahitaji maombi na dua za Watanzania, Ili kuwaletea Watanzania maendeleo. Inawezekana.
Kama ulishakuwa na jipu nadhani unajua maumivu yake hasa yale majipu yanayoota sehemu hatarishi kama jichoni, kwapani au sehemu za siri.
Magufuli bila kujali, atumbue majipu ya mahali popote na atoe hadi kiini cha jipu, tena kwa sindano kali ili iwe fundisho kwa vizazi vijavyo ili kujenga uzalendo na mahaba ya dhati kwa Tanzania.
Watanzania tumekuwa na asili ya uvivu, hatupendi kufanya kazi, wakati mwingine tunafanya kazi kwa mazoea, huku tukifurahia wingi wa siku za mapumziko na sikukuu. Hatusikitiki kuona kazi zinalala.
Sasa ni wakati wa kujituma, kuweka kando uvivu na uzembe ili nasi ifike wakati tule mbivu.
Noel Shao ni mhitimu wa shahada ya elimu Chuo Kikuu cha Dodoma 0769735826
No comments :
Post a Comment