Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga akizungumza na mahabusu na wafungwa waliopo Gereza la Wanawake Segerea, Dar es Salaam wakati alipofanya ziara katika Gereza hilo jana. Kushoto ni Waziri wa Sheria na Katiba, Dk Harrison Mwakyembe, kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mbarak Abdulwakil na wapili kulia ni Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, CGP John Minja. Picha na Mambo ya Ndani
Dar es Salaam. Kasi ya mawaziri wa Serikali ya Awamu ya Tano jana, ilihamia kwenye magereza ya Keko, Ukonga na Segerea jijini Dar es Salaam na baada ya kushuhudia mrundikano wa wafungwa na mahabusu, waliamua kuunda kamati ya kushughulikia matatizo ya taasisi hiyo.
Sababu za mrundikano huo zimetajwa kuwa ni ucheleweshaji wa kesi mahakamani na upelelezi kuchukua muda mrefu, jambo linalosababisha idadi ya watuhumiwa wanaosubiri hatima yao kuwa kubwa magerezani.
Tangu walipoapishwa Desemba 12, mawaziri wengi wamekuwa wakitembelea taasisi zilizo chini ya wizara zao kufuatilia utendaji na utoaji wa huduma kwa wananchi na kutoa matamko.
Jana, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe na Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga walifanya ziara ya pamoja kwenye magereza hayo, kuzungumza na wafungwa, mahabusu na askari magereza na kisha kuunda kamati ndogo ya watalaam itakayopitia changamoto zote, kuja na majibu ya jinsi ya kuzitatua.
Mrundikano wa wafungwa na mahabusu ni suala linalopigiwa kelele na wanaharakati, huku Jeshi la Magereza likilalamikia gharama za kuwatunza.
Gharama ya kumtunza mfungwa mmoja kwa siku ni Sh3,670 wakati Serikali huchangia Sh1,500. Kwa kiwango cha mchango huo, Serikali hutoa jumla ya Sh20 bilioni kwa mwaka, wakati jumla ya gharama zote ni Sh51 bilioni.
Ili kukidhi mahitaji hayo, Jeshi la Magerezahulazimika kufanya shughuli mbalimbali za kujiingizia kipato kwa ajili ya kuwahudumia wafungwa, ikiwemo kilimo na ufundi.
“Ndio maana tulitembelea magereza ili tujifunze changamoto zilizopo. Lengo ni sisi kwa nafasi zetu kuunganisha nguvu na kutatua hizo changamoto ili tuweze kupiga hatua kwa kasi,” alisema Dk Mwakyembe.
“Tumeona matatizo mengi ambayo tunakwenda kuyafanyia kazi. Msongamano wa mahabusu na wafungwa ni mkubwa sana. Tunabeba mzigo wa zaidi ya mara mbili ya uwezo wa gereza na kuna sababu nyingi zinazosababisha hayo,” alisema Dk Mwakyembe. Alisema changamoto za magereza hayo matatu zinafanana.
“Tumewasikiliza, tumejifunza na tumechukua makabrasha mengi sana,” alisema Dk Mwakyembe akizungumzia mahabusu wanaosubiri kesi zao kumalizika.
Alisema mbali na kuunda kamati ndogo, watatembelea tena magereza mwezi ujao ili kutoa taarifa za jinsi walivyoshughulikia changamoto walizoelezwa na jinsi ya kupatia ufumbuzi wa changamoto nyingine.
Alisema lengo la Serikali iliyopo madarakani aliyosema “imeanza kasi kwa kasi”, ni kuwarejeshea Watanzania matumaini ambayo upatikanaji wake ni kutengenezwa kwa mazingira wezeshi.
“Wizara hizi mbili zina vyombo vinavyohusika na kutoa haki, mtu akiboronga vyombo vyetu hukamata, kupeleleza, kutengeneza mashitaka, kupeleka mahakamani, kuhukumu na kuhifadhi waliohukumiwa,” alisema Dk Mwakyembe.
“Hatuwezi kupata maendeleo kama vyombo hivi vitalegalega.”
Kwa upande wake, Kitwanga alisema: “Tunataka kwenda katika uchumi wa kati. Lazima tufanye kazi kwa ufanisi ili haki itendeke na nchi iendelee kuwa na utulivu. Lazima tujue mazingira ya watu tunaofanya nao kazi. Pia tumewaona wafungwa waliohukumiwa na watuhumiwa waliopo rumande.”
Alisema changamoto kubwa ya askari magereza ni nyumba za kuishi na vitendea kazi, na kwamba tayari Serikali imeingia mkataba wa kujenga nyumba zaidi ya 9,000 kwa ajili ya askari.
Alipoulizwa kuhusu kuanza kutolewa hukumu ya kifungo cha nje kwa waliohukumiwa kifungo cha chini ya mwaka mmoja jela ili kupunguza mlundikano magerezani, Kitwanga alisema suala hilo linafanyiwa kazi na tayari ameshazungumza na Jaji Kiongozi.
“Hivi Dar es Salaam ikiwa na wafungwa wa nje 200 wakafanya usafi mara tatu kwa wiki ni wazi kuwa jiji litakuwa safi sana. Tunaweka utaratibu mzuri wa kutekeleza haya bila kuathiri mfumo wa sheria uliopo,” alisema Kitwanga.
No comments :
Post a Comment