Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Ashatu Kijaji akiapa
Historia na Elimu
Dk Ashatu Kijaji ndiye Naibu Waziri wa Fedha na Mipango katika Serikali ya Awamu ya Tano, ameteuliwa katika baraza la mawaziri la mwanzo la Rais John Pombe Magufuli. Kiongozi huyu mwanamama na kijana ameteuliwa katika nafasi hii kwa kuwa yeye ni mbunge wa kuchaguliwa kutoka jimbo la Kondoa Vijijini liliko mkoani Dodoma. Kabla hajawa mbunge Kijaji amekuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu.
Hivi sasa Dk Kijaji ana umri wa miaka 39 na ifikapo Aprili mwaka 2016 atafikisha miaka 40, kwani alizaliwa Aprili 26, 1976 huko Kalamba Wilaya ya Kondoa.
Kijaji alianza elimu ya msingi wilayani Kondoa katika Shule ya Msingi Kalamba kati ya mwaka 1984 hadi 1990 akajiunga Shule ya Sekondari Kilakala iiliyoko mkoani Morogoro kati ya mwaka 1991 – 1994, kabla ya kwenda kidato cha tano na sita katika Taasisi ya Biashara Shinyanga (SHYCOM) akisoma masomo ya biashara, hii ilikuwa ni mwaka 1995 – 1997.
Safari ya elimu ya juu ya Kijaji aliianzia katika Chuo Kikuu cha Mzumbe akibobea katika Uchumi, alisoma tangu mwaka 1998 hadi 2001 na kutunukiwa Stashahada ya Juu (Advanced Diploma) ya Mipango ya Uchumi, stashahada hiyo ya juu ni sawa na Shahada ya Sayansi katika Uchumi ambayo inatolewa na Chuo Kikuu cha Mzumbe hivi sasa.
Mara baada ya kuhitimu stashahaa hiyo alipata fursa ya kuendelea na masomo ya juu nchini Norway katika Chuo Kikuu cha Kristiansand, alifanya masomo yake chuoni hapo tangu mwaka 2006 hadi 2008 na kutunukiwa shahada ya umahiri ya Sayansi (MSc) katika Usimamizi wa Biashara akijikita zaidi kwenye Usimamizi wa Kimataifa.
Safari ya ubobezi ya Dk Kijaji iliendelea tena mwaka 2008 (kwa miaka mitano) katika Chuo Kikuu hicho hicho (Kristiansand cha Norway), mara hii akisomea shahada ya uzamivu (PhD) ambayo alifanikiwa kutunikiwa mwaka 2013 akibobea kwenye Uchumi, lakini akijikita katika Usimamizi wa Kimataifa.
Dk Kijachi ameolewa, ana watoto wawili na anazungumza lugha tatu kwa ufasaha, Kiswahili, Kiingereza na Ki-Norwegian, lakini pia ana uwezo wa kati katika lugha ya Kiarabu.
Uzoefu
Pamoja na umri wake wa kawaida, Dk Kijaji ana uzoefu mkubwa wa kazi. Amewahi kuwa Ofisa Mipango katika Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe kati ya mwaka 2001 – 2002 ambapo alisimamia masuala ya mipango, bajeti na uratibu wa miradi mbalimbali ya maendeleo. Mwaka 2002 kuanzia Machi hadi Agosti alipandishwa na kuwa Ofisa Mipango Miji wa wilaya nzima kwa hiyo akapata wasaa wa kuongoza idara ya mipango katika Wilaya ya Kisarawe.
Uzoefu wa miaka miwili katika halmashauri ulimtosha Dk Kijaji, akaamua kubadilisha mazingira, akarudi katika taaluma pale Chuo Kikuu cha Mzumbe kati ya mwaka 2005 - 2009 akifanya kazi kama Mfundishaji Msaidizi (Teaching Assistant), hii huwa ni kuwasaidia wahadhiri na maprofesa katika ufundishaji.
Lakini pia kati ya mwaka 2008 hadi 2013 Dk Kijaji amefanya kazi kama Mtafiti Mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Agder akiwasaidia maprofesa katika ufundishaji na kufanya utafiti.
Kuanzia mwaka 2009 – 2014 Dk Kijaji amefanya kazi kama Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe (kama kawaida kwenye mafunzo, ushauri wa kitaalam na utafiti) akijikita katika utengenezaji na uchambuzi wa sera, uchambuzi wa kitaasisi, uchumi wa kazi na maendeleo, usimamizi wa kistratejia, maendeleo ya vijijini, usimamizi wa miradi na masuala ya ushirikiano wa kimataifa kwenye uchumi.
Kuanzia Julai 2014 hadi karibia na wakati wa Uchaguzi Mkuu, Dk Kijaji amekuwa Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe akisimamia masuala yale yale na akifundisha masomo ya uchumi.
Kati ya Januari 2012 hadi Desemba 2014 mwanamama huyu amekuwa Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Sera katika Taasisi ya Masomo ya Maendeleo ya Chuo Kikuu cha Mzumbe. Kuongoza idara hii kulimpa fursa pana ya kusimamia uandaaji na uchambuaji wa sera na miradi mbalimbali. Kupanga, kutengeneza bajeti na kuratibu shughuli za maendeleo ikiwa ni pamoja na kutekeleza, kusimamia na kufanya mapitio ya miradi husika, pamoja na kazi nyingine nyingi za kitaaluma ambazo zilikuwa na tija kwa mustakabali wa mipango ya mbeleni ya uchumi wa taifa.
Dk Kijaji ameandika na kuchapisha zaidi ya tafiti tisa katika majarida ya kitaaluma ya kimataifa ikiwemo Jarida la Usimamizi wa Uongozi (Uongozi Journal of Management), Jarida la Kimataifa la Biashara na Menejimenti (International Journal of Business and Management), Jarida la Kimataifa la Mapitio ya Sayansi za Jamii (International Review of Social Sciences and Humanities), Jarida la Masuala ya Afrika (African Affairs Journal), Jarida la Kazi Linganishi za Jamii (Journal of Comparative Social Work), Jarida la Usimamizi wa Umma wa Marekani na China (US-China Public Administration).
Kwa upande wa vitabu, mwanamama huyu kijana na nguli amechapisha jumla ya vitabu vitano hadi sasa kati ya hivyo, viwili ameandika yeye mwenyewe na vitatu kwa ushirikiano na wabobezi wengine. Vitabu vyake ni pamoja na Athari za Uwezo wa Kitaasisi wa Soko la Ajira katika kutengeneza Uhakika wa Ajira kwa Waajiriwa (Tafsiri yangu).
Kama mtaalamu, Dk Kijaji amewahi kushinda na kusimamia tafiti sita kubwa au ambazo zina matunda ya kitaifa na kimataifa. Mathalani, Mwaka 2003 hadi 2004 alifanya utafiti juu ya Sababu zinazowakwamisha wanawake wa Tanzania Kiuchumi, huu ulifadhiliwa na Taasisi ya Utafiti ya Sayansi Jamii ya Mashariki na Kusini mwa Afrika (OSSREA). Kati ya mwaka 2008 na 2009 alifanya utafiti juu ya Kupungua kwa Samaki wa Asili kutoka Ziwa Victoria, huu ulifadhiliwa na Vyuo Vikuu vya Mzumbe na Agder. Na mwaka 2011 na 2012 alifanya utafiti juu ya masuala ya ajira, ukisimamiwa na OSSREA.
Kwa upande wa siasa Dk Kijaji amekuwa mwanachama mtiifu wa CCM kwa kipindi kirefu kabla hajaamua kujitosa kuusaka ubunge katika jimbo la Kondoa Vijijini, akashiriki kura za maoni na kuongoza kwa kupata kura 9,162 dhidi ya Lubuva Hasani aliyekuwa na kura 9,113 na Monica Mohamed kura 4,641. Baada ya kupitishwa rasmi na vikao vya CCM na kupambana vilivyo majukwaani, alifanikiwa kutangazwa mshindi wa ubunge katika jimbo hili kutokana na kura zilizopigwa Oktoba 25, 2015.
Nguvu
Jambo la kwanza na muhimu linalompa nguvu Dk Kijaji ni usomi na ubobezi. Bila shaka mwanamama huyu ni mmoja wa wanawake wachache waliobobea kikweli kweli hapa Tanzania. Katika ngazi ya uwaziri au unaibu waziri, bila shaka elimu ni jambo la msingi sana, lakini elimu ya ubobezi unaothibitika ni jambo lingine muhimu zaidi na Kijaji amepata bahati hiyo. Kwa sababu wizara anayoiongoza ina wasomi nguli lukuki, lakini kukiwa hakuna ufanisi mkubwa wa kusifia, anaweza kuwa chachu ya kipekee ya kufanya kombinesheni ya weledi, ujana na upambanaji na akajikuta anakuwa mmoja kati ya wanamama wanaofanya vyema katika sekta nyeti za umma hapa Tanzania.
Jambo la pili muhimu ni uwezo wa kiutafiti. Nilipoonesha hapo juu baadhi ya tafiti ambazo mwanamama huyu amewahi kuzisimamia kuna watu wanaweza kudhani ni tafiti za ‘kitoto’, baadhi ya wahadhiri wa uchumi nilioongea nao kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe wanamtaja Dk Kijaji kama mmoja kati ya vijana wahadhiri wenye sifa zote muhimu ambao walikuwa tegemeo katika kitivo cha uchumi katika chuo hicho. Kwenye utafiti mara zote amekuwa mtu aliyefanya kwa mafanikio makubwa.
Tatu, hili ni jambo binafsi na huwenda yeye mwenye halijui vizuri. Wanafunzi wa Mzumbe nilioongea nao, ambao wamewahi kufundishwa au kusimamiwa darasani, katika uandishi wa tasnifu ili kupata shahada zao wameniambia kuwa usiombe ukasimamiwa na Dk Kijaji, kama uliingia chuoni kwa njia za kona kona unaweza ukashindwa kuhitimu shahada yako. Mwanamama huyu ni mtu “wa kawaida sana, mwenye misimamo kazini lakini mcheshi”. Wanafunzi waliopitia kwake wanakiri kuwa ni lazima uwe na nidhamu ili uwe mwanafunzi wake na hiyo ni habari njema sana ikiwa mwanamama huyu atahamishia haiba hiyo pale kwenye wizara sugu na iliyokubuhu kwa mizaha, kushindwa kukusanya mapato.
Udhaifu
Dk Kijaji anakabiliwa na udhaifu mmoja mkubwa, ugeni katika siasa. Mwanamama huyu ndiyo kwanza anaingia kwa mara ya kwanza katika siasa za kitaifa, za uendeshaji wa Bunge, za mipango ya Serikali. Siyo siri kuwa ugeni huu akiuendekeza utamsumbua na kumuangusha. Kazi ya kuendesha Serikali na katika wadhifa wa Naibu Waziri siyo sawa na kufundisha Chuo Kikuu na kufanya utafiti, mhusika akiwa anachelewa kujifunza, hawezi kufika popote. Ikiwa Dk Kijaji atachukua muda mrefu kujifunza mambo ya wizara, kwa asili ya wizara hii atayumbishwa sana na watendaji na wadau kwani wizara yake inapaswa kuwa kazini saa 24 ili nchi ikue kimapato na haina muda wa kujifunza wala kufanya makosa ya mipango wala utekelezaji
Kwa hiyo nusura yake ni kujipanga kujifunza mambo ya kisiasa haraka, lugha za wanasiasa, mitizamo ya wanasiasa, namna ya kuwapinga wanasiasa na bado ukawa rafiki yao n.k. Lakini ugeni huu naamini hautamsumbua kwenye kipengele cha kurudisha nidhamu na utendaji unaofuata sheria na taratibu wizarani.
Matarajio
Matarajio ya Dk Kijaji ni kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa nchi ya mfano katika ukusanyaji wa mapato na udhibiti wa wanaokwepa kulipa kodi. Anaamini haya yanaweza kufanyika ikiwa atapewa ushirikiano kutoka kwa wadau wote hususani bunge na mawaziri wenzake kwani yeye anaongoza wizara mtambuka.
Hata hivyo, matarajio ya wadau na hasa wataalamu wa uchumi ambao wanamfahamu Dk Kijaji wanasema kuwa nchi hivi sasa imepata mtaalamu muhimu pale wizarani, mtu ambaye ana weledi wa kutosha katika uchumi wa kimataifa na kwa hivyo kilichobaki ni rais kuleta Waziri wake ambaye atakuwa anabobea kwenye uchumi wa jumla au uchumi wa ndani ya nchi. Kwamba kombinesheni ya wawili hao inaweza kuwa mwarobaini wa usimamizi wa masuala ya mipango na uchumi hapa nchini kwetu.
Changamoto
Moja ya Changamoto kubwa ambazo zinaikabili Serikali yetu ni kushindwa kukusanya mapato yote kutoka kwenye vyanzo vilivyopo. Vyanzo vya mapato vichache vilivyopo vimeendelea kuwa sehemu ya utajiri wa watu binafsi na hilo linafanyika kwa uwazi na bila kificho. Maofisa wengi na watendaji wakuu na wadogo wanaosimamia mapato ndiyo Watanzania wanaoongoza kwa kuzunguka mitaani na magari ya mamilioni ya fedha na makumi ya majumba yaliyojengwa kwa mabilioni ya shilingi za Tanzania. Hizi ni fedha za umma na zinachotwa waziwazi. Lazima wizara hii na Kijaji mwenyewe asaidiane na waziri wake ili nidhamu na uaminifu katika masuala ya fedha virudi.
Lakini changamoto ya pili iliyopo ni kutowekeza na kukusanya kodi katika vyanzo vipya vya mapato. Kwa wale wanaofuatilia mabunge ya bajeti kila mwaka, wanakumbuka kuwa “mikwara” ya waziri wa fedha na “briefcase” yake huwa inaishia tu kuongeza kodi kwenye soda, bia, sigara, mafuta ya taa, petrol, diesel na kodi za magari. Wakati Serikali inapoteza muda kila kukicha kukimbizana na kodi ya soda, imeshindwa kabisa kuanzisha vyanzo vya uhakika vya kodi kutoka katika maeneo mengine makubwa yanayotokana na asili ya utajiri wa nchi yetu. Watanzania wanataka kuona vyanzo vipya vya mapato vinapanuliwa na nchi inakuwa na sehemu nyingi za kupata fedha.
Changamoto ya tatu ambayo imekuwa inakosekana kwa kipindi kirefu ni kukosekana kwa vipaumbele vya Serikali. Tanzania imekuwa inajiendesha bila vipaumbele thabiti, kila mara wizara ya fedha huja na mipango mipya ya kufanya kila jambo, na kabla haijapima ufanisi wa mipango hiyo utakuta imeshabadilishwa, kila anapokuja waziri mpya anakuja na mipango yake na vipaumbele vyake na staili yake ya utekelezaji, matokeo yake mfumo wa uchumi, mipango na fedha unavurugika nchi nzima kwa sababu wizara mama ya uchumi na mipango kila mara ina jambo jipya.
Dk Kijaji na waziri atakayeteuliwa wana kazi ya ziada kuhakikisha kuwa mipango ya kiuchumi ya nchi inaendeshwa kwa utaratibu, vipaumbele mahsusi na utulivu wa hali ya juu. Lakini kubwa kuliko yote mipango hii lazima izingatie mwelekeo wa uchumi wa dunia ili mwisho wa siku Serikali na nchi yetu isijikute matatani kwa kupanga mambo ambayo mataifa karibia yote yanayakwepa.
Jambo lingine kubwa ambalo ni changamoto kwa Dk Kijaji na wenzake ni kusimamia upunguzaji wa mzigo wa madeni. Taarifa zinaonesha kuwa deni wakati Rais Jakaya Kikwete anaingia madarakani mwaka 2005 deni la taifa lilikuwa takribani Sh6 trilioni (bilioni 6,000), mwaka 2011 (miaka saba baadaye) inasemekana deni hilo liliongezeka hadi kufikia Sh22 trilioni (bilioni 22,000) na mwaka 2015 (miaka mitatu baadaye) deni limekua na kufikia Sh40 trilioni 40 (bilioni 40,000).
Ukopaji mkubwa unaopitiliza umewahi kuziingiza Serikali nyingi sana matatani na mwaka 2013 Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi isiyo ya kiserikali inayojishughulisha na masuala ya Madeni ya Taifa na Maendeleo (TCDD), Hezron Mwakagenda alisisitiza kuwa “nchi yetu inatakiwa kujifunza kwa nchi za Hispania, Ugiriki na Ireland ambazo zimekumbwa na matatizo makubwa ya kiuchumi kutokana na kuwa na madeni makubwa” alikuwa anatoa maoni hayo kutokana na sakata la Serikali yetu kuendelea kukopa fedha nyingi kutoka kwenye benki za ndani.
Kitisho cha ukopaji uliopitiliza na ambao umesababisha sasa Tanzania kuwa na mzigo wa madeni ni changamoto ambayo Dk Kijaji na wenzake wana kazi ya ziada ya kuitatua, njia mbalimbali zinaweza kutumika mojawapo ikiwa ile ya kuomba kusamehewa madeni bila masharti magumu kama alivyofanya Benjamin Mkapa miaka ya 1995 – 2005, na hii itamhusu zaidi Dk Kijaji na utaalamu wake wa Uchumi wa Kimataifa.
Hitimisho
Dk Kijaji si mtu hapa Tanzania, wengi katika kada ya kawaida ya maisha ndiyo wanamsikia kwa mara ya kwanza, hasa alipotangazwa kuwa naibu waziri kwenye wizara hii inayogusa maisha ya kila mkulima, mfanyakazi na mwanachi wa kawaida wa Tanzania. Kujiamini kwake, ubobezi wake, elimu yake, nidhamu yake kazini na umahiri katika utafiti ni mambo yanayoweza kuwa kinga yake dhidi ya changamoto ambazo ziko mbele yake na wizara yake. Sina shaka kuwa kwa mipango ya maendeleo ya sasa, mwanamama huyu atajifunza haraka na kuwa kiongozi wa kutegemewa katika masuala ya uchumi hapa Tanzania. Namtakia kila la heri katika utumishi wake.
Kihusu Mchambuzi
Julius Mtatiro ni Mchambuzi wa Masuala ya Kisiasa na Kijamii, ni mmoja kati ya vijana wenye uzoefu mkubwa na siasa za Tanzania. Ana Cheti cha Juu cha Sarufi (“Cert of Ling”), Shahada ya Sanaa “B.A” katika Elimu (Lugha, Siasa na Utawala), Shahada ya Umahiri (M.A) ya Usimamizi wa Umma na Shahada ya sheria (L LB); +255787536759, juliusmtatiro@yahoo.com, https://www.facebook.com/JuliusSundayMtatiro/, - Uchambuzi huu unatokana na utafiti na maoni binafsi ya mwandishi).
No comments :
Post a Comment