Dar es Salaam. Zaidi ya wakazi 50 wa Kijiji cha Kerege wilayani Bagamoyo wamevamia shamba la waziri zamani wa Nishati na Madini, Daniel Yona lililopo jirani na kijiji lakini hawakutimiza azma yao ya kugawana baada ya kukurupushwa na polisi.
Mmoja wa wanakijiji hao, Issa Hemed alisema wananchi walifika kwenye shamba hilo jana saa 12:00 asubuhi na kuanza kupimiana maeneo, huku kila mtu akiweka alama za kiwanja anachotaka.
Hemed alisema shamba hilo lililoko mkoani Pwani halijaendelezwa kwa muda mrefu na limekuwa msitu ambao alidai hutumiwa na majambazi kama sehemu ya maficho.
Alisema wanakijiji hao waliunda kamati kwa ajili ya kuchukua eneo hilo na kuwagawia kwa sababu haliendelezwi.
Hata hivyo, alisema wakati wakiendelea kugawana jana saa 5:00 asubuhi, polisi walifika na wananchi kulazimika kukimbia, huku baadhi yao wakikamatwa.
Alisema yeye ni mpangaji ambaye hana ardhi ya kujenga hata chumba kimoja, lakini sasa anashukuru kupata eneo.
Alipoulizwa kama haoni ni kosa kuchukua ardhi ya mtu mwingine, Hemed alisema haiwezekani mtu mmoja akamiliki ekari nyingi bila kuziendeleza, huku wengine wakikosa eneo dogo la kulima bustani.
Mkazi mwingine wa Kerege, Naomi Bandawe alisema Serikali inapaswa kuwagawia wananchi mashamba hayo kwa kuwa watu wengi walihodhi, lakini wameshindwa kuyaendeleza.
“Kuna faida gani ya kuwa na misitu isiyoendelezwa wakati wananchi wengi hawana ardhi,” alisema.
Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Pwani, Jaffer Mohamed alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema watu 10 wanashikiliwa na jeshi hilo kwa kosa la uvamizi.
Alisema kumekuwa na matukio ya mara kwa mara ya uvamizi wa mashamba na kwamba kuna watu wengi waliokamatwa na kesi zao zinaendelea mahakamani.
“Baada ya polisi kufika eneo hilo, baadhi ya wananchi walikimbia, lakini wengine 10 walikamatwa na watafikishwa mahakamani kwa kuvamia mashamba ya watu,” alisema.
Alisema hata siku ya Uhuru wakati wananchi wanafanya usafi, wengine walikuwa wanagawana mashamba ya watu jirani na eneo hilo na walikamatwa na polisi.
“Tabia hii imeota mizizi katika Wilaya ya Bagamoyo ya watu kujichukulia sheria mkononi kwa kugawana mashamba ya watu wengine,” Kamanda Mohamed.
No comments :
Post a Comment