Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Tuesday, December 15, 2015

Wakuu wa shule wanaotoza michango washughulikiwe

NA EDITOR

15th December 2015.

Moja ya ahadi kubwa za Rais Dk. John Magufuli, ilikuwa kutoa bure kuanzia elimu ya msingi hadi ile ya sekondari.
 
Ahadi hii aliinadi wakati wa kampeni zake za kuwania urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na bila shaka wananchi watakuwa wanasubiri utekelezaji wake kuanzia mwakani.
 
Kipindi hiki ndicho wazazi wengi wanaandaa watoto wao kujiunga na darasa la kwanza mwakani.
 
Hata hivyo, katika hali ya kusikitisha, kuna wakuu wa shule wanaopuuza agizo la Rais na kuendelea kutoza michango.
 
Watendaji kadhaa wa serikali wamerudia mara kadhaa kutoa karipio kwa wakuu wa shule husika kutii agizo la serikali.
 
Tunaomba serikali itekeleze kwa vitendo kwa kuhakikisha inachukua hatua kali kwa wale wote wanaopuuza agizo lake.
 
Tunafahamu sote kuwa suala la elimu bure, ni kati ya ahadi kubwa za Rais Magufuli.
 
Katika kudhihirisha umuhimu wake, Rais Magufuli bado hajateua mtu wa kuongoza Wizara ya Elimu kwa kuwa bado hajapata mtu wa kuiongoza kutokana na unyeti wake.Tungependa kuona ahadi ya Rais inatekelezwa kwa vitendo na siyo baadhi ya wakuu wa shule kupuuza agizo hilo na kuachwa hivi hivi.
 
Tunafahamu kwa miaka mingi sasa suala la michango limekuwa kama mpango mahususi wa baadhi ya walimu wa shule ili kujinufaisha.
 
Bahati mbaya masuala ya michango yalikithiri mno huku yakifumbiwa macho na viongozi wa halmashauri mbalimbali nchini wenye dhamana ya kusimamia shule hizo.
 
Hata hivyo, pamoja na ukweli kuwa wazazi wengi watahamasika kupeleka watoto kwenye shule za serikali kutokana na kutoa elimu bure, lakini pia lazima serikali iboreshe shule zake.
 
Katika miaka ya nyuma, lilikuwa jambo la fahari kwa mzazi kusomesha mtoto wake katika shule ya serikali mathalan, Sekondari za Mzumbe, Songea, Bwiru, Ilboru, Umbwe, Milambo, Tabora, Weruweru, Rugambwa, Malangali, Bwiru na nyinginezo.
 
Hata hivyo, katika miaka ya karibuni, hali imekuwa tofauti kutokana na ukweli kuwa hule za serikali ziko katika hali mbaya.
 
Hakuna mazingira mazuri ya mtoto kufaulu wala kuishi na matokeo yake wazazi wengi wameelekeza nguvu zao kusomesha watoto wao shule binafsi.
 
Na ushahidi ulio wazi ni jinsi wanafunzi wa shule binafsi wanavyofanya vizuri katika mitihani mbalimbali ya kitaifa.
 
Sasa ni jambo la kusikitisha kuona kuwa serikali inaingilia uendeshaji wa shule za binafsi wakati imeshindwa kusimamia shule zake.
 
Ushauri wetu kwa serikali ni kuwa pamoja na kutoa elimu bure, lakini lazima iboreshe shule zake ili zitoe kiwango bora cha elimu.
 
Watendaji wenye dhamana ya kusimamia sekta ya elimu nchini, wanapaswa kuelekeza nguvu zao katika kuhakikisha wanaboresha mazingira ya utoaji wa elimu ya shule za serikali.
 
Serikali ya awamu ya nne ilikuja na mpango kamambe wa kujenga shule katika kila kata.
 
Ni kweli shule zilijengwa kwa kasi, lakini jambo la kusikitisha ni kuwa shule hizo zina matatizo lukuki kama uhaba wa walimu na zana za kufundishia.
 
Kutokana na mazingira duni ya shule nyingi za serikali, kumechochea baadhi ya wakuu wa shule kuanzisha michango mbalimbali.
 
Tunaomba wakuu wa shule wasiachwe kuvunja agizo la serikali na badala yake hatua zichukuliwe ili kuhakikisha ahadi ya Rais Magufuli inatekelezwa.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment