Waziri aipa polisi siku moja kujieleza
Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga
Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga ametoa siku moja kwa Jeshi la Polisi kueleza ni kwa nini askari hawalindi Bandari ya Dar es Salaam badala yake kazi hiyo inafanywa na kampuni binafsi za ulinzi.
Kitwanga amepanga kukutana na viongozi waandamizi wa Polisi kesho ili kujadili mipango na mikakati mbalimbali ya kuongeza ufanisi wa kazi ya kuwahudumia wananchi.
Akizungumza na maofisa waandamizi wa polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam baada ya kufanya ziara katika Chuo cha Taaluma ya Polisi na kuangalia makazi ya askari, Kurasini, Kitwanga alieleza kusikitishwa na hatua ya polisi kuacha kutoa ulinzi bandarini na kuita kitendo hicho kuwa ni udhaifu wa jeshi hilo.
Alisema kitendo hicho kimetoa mwanya kwa baadhi ya wafanyabiashara kukwepa kodi wakati wa kushusha bidhaa zao akisema Bandari ni eneo la mpaka ambalo linahitaji ulinzi wa polisi kama mipaka mingine ya nchi.
Akionekana kukerwa, Waziri Kitwanga alimkatisha Kamishna wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alipojaribu kutoa sababu akimtaka kutumia siku nzima ya leo kuandaa majibu ili kesho wayazungumze kwenye kikao rasmi. Waziri Kitwanga amelitaka pia jeshi la polisi kumweleza mipango ya kukabiliana na dawa za kulevya kwa sababu ndiyo zimekuwa chanzo cha matukio mengi ya uhalifu ikiwamo tishio la ugaidi.
Alisema haiwezekani kitengo cha kupambana na dawa za kulevya kikaachiwa jukumu hilo wakati jeshi la polisi liko kwenye operesheni zake kila siku.
Kuhusu msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam, waziri huyo alisema ni uzembe wa askari wa usalama barabarani kwa sababu wameshindwa kusimamia sheria na kuwachukulia hatua madereva wazembe.
Alisema zipo nchi za Afrika ambazo hazina askari wa barabarani kwa sababu kiwango cha nidhamu ya madereva wake ni kikubwa na wamekuwa wakifanya vizuri kuhakikisha kwamba suala la msongamano usio wa lazima unadhibitiwa kwa kufuata sheria.
Askari wazungumzia kero zao
Baadhi ya askari walimweleza Kitwanga kero zao. Mmoja wao, Alphonce Malowa alisema nyumba za askari ni chache na nyingi zimechakaa kiasi cha kuwafanya kudharaulika mbele ya wananchi.
Inspekta Novatus Makondowa alieleza juu ya umuhimu wa Serikali kuwasomesha walimu wa chuo cha taaluma za polisi ili kuwajengea uwezo zaidi wa kufundisha maofisa wengine chuoni hapo.
No comments :
Post a Comment