Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.
Dar es Salaam. Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amejiweka kitanzini akidai atamwomba Rais John Magufuli amwajibishe endapo atashindwa kumaliza tatizo la upatikanaji wa dawa za ugonjwa wa saratani kwa bei nafuu.
Akizungumza katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road ambako jana alizindua Bodi Mpya ya taasisi hiyo, Ummy alisema atahakikisha tatizo la ukosefu wa dawa linakuwa historia nchini ili kudhihirisha kuwa uteuzi wake katika nafasi hiyo haukuwa wa makosa.
Ummy alisema uwaziri wake hautaonekana wa maana kama hatawatendea haki wagonjwa wa saratani kwa kuhakikisha bei ya dawa inapungua hasa za dripu. Pia, alishangazwa na Bohari ya Dawa (MSD) kutonunua dawa moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji badala yake inawatumia mawakala kununua dawa hizo.
“Nitajisikia vibaya sana kama nitashindwa kutatua suala la upatikanaji wa dawa hapa Ocean Road kwa sababu wananchi kweli wanateseka. Utakuta mwananchi analipa shilingi laki nane halafu baada ya wiki sita tena anatakiwa arudi hospitalini hapo na kulipa tena laki nane ni jambo ambalo silikubali,” alisema.
Amina Hussein (56) mkazi wa Kilosa, Morogoro ambaye ni ndugu wa mgonjwa aliyelazwa katika taasisi hiyo alilalamika kuwa bora kuuguza mgonjwa mwenye ukimwi kuliko adhabu wanayoipata kutokana na gharama za matibabu kuwa kubwa.
Amina alisema gharama za matibabu zinazofikia Sh800,000 kila baada ya wiki mbili ni kubwa hasa kutokana na kulazimika kulipia dripu za maji ya dawa kwa ajili ya wagonjwa wao na kwamba taasisi hiyo mara nyingi imekuwa ikikabiliwa na upungufu wa damu.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo, Diwani Msemo alisema waliwaeleza MSD, tangu Agosti kuwa maji ya kuwatundikia wagonjwa wanayowapa hayatoshi lakini hadi sasa hakuna hatua zilizochukuliwa.
Alisema kwa mwaka zinahitajika Sh6 bilioni kwa ajili ya maji hayo ya kutundikia wagonjwa na vifaa tiba, na Sh15 milioni zinahitajika kununulia mashine za mionzi.
“Asilimia 90 ya wagonjwa wa saratani wanatibiwa hospitalini hapa hivyo tunaiomba serikali ifanye jitihada tuweze kupatiwa fedha hizo,” alisema Nsemo.
Ummy alimwahidi mkurugenzi huyo na wagonjwa kuwa atakwenda MSD kupata maelezo ni kwa nini hawana dawa. Pia, aliahidi kutafuta wadhamini ili kuhakikisha tatizo la dawa linakwisha nchini.
“Tunayo sera ya matibabu bure kwa wagonjwa wa saratani kwa hiyo sera hii inabidi tuitekeleze na siyo kuipindisha kwa kuhakikisha Serikali inapunguza makali kwa wananchi katika ununuzi wa dawa,” alisema Ummy. “Naamini Rais Magufuli ataniunga mkono katika suala hili la upatikanaji wa dawa kwani hata yeye pia ni miongoni mwa vipaumbele alivyoeleza alipokuwa anaomba kura za urais na hata katika hotuba yake alipokuwa anazindua Bunge mjini Dodoma kuwa upatikanaji wa dawa ndiyo changamoto kubwa nchini katika kuboresha huduma za afya,” alisema.
Ili kukabiliana na changamoto hiyo Waziri Ummy amesema mara baada ya kuwasili katika wizara hiyo aliandika barua kwa Waziri wa Fedha kuomba fungu maalum kwa ajili ya MSD ili wapate fedha moja kwa moja kutoka hazina ziende huko ili kuweza kununua dawa.
Wakati huo huo, Waziri Ummy alizindua bodi mpya ya taasisi hiyo na kuwataka wajumbe wa bodi hiyo kufanya kazi kwa kushirikiana na kuendelea kutoa elimu na kusambaza maarifa dhidi ya saratani na kuwataka Watanzania waondoe dhana potofu inayowazuia wagonjwa wengi kutofika hospitalini hapo.
Alisema ni jukumu la bodi hiyo kuhakikisha matibabu yanatolewa bure kwa wagonjwa wa saratani kwa lengo la kuwafikia wagonjwa wa kipato tofauti.
Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Profesa Hamis Dihenga alisema bodi hiyo inadhamana kubwa ya kufuatilia ni namna gani wagonjwa wanavyopata matibabu katika hospitali hiyo na kuhakikisha wanapatiwa matibabu yaliyo bora.
No comments :
Post a Comment