Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Donan Mmbando.
Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Donan Mmbando ameziagiza idara zote zinazotoa huduma chini ya ofisi yake kumpa ripoti ya watumishi waliokwenda nje ya nchi baada ya Rais John Magufuli kupiga marufuku safari hizo isipokuwa kwa kibali kutoka Ikulu.
Agizo hilo limo kwenye taarifa aliyotuma jana kwa wakuu wa idara hizo akiwataka kumpa ripoti kamili ya majina ya watumishi hao, nchi walizokwenda na madhumuni ya safari hizo.
Alisisitiza kuwa wakuu hao wanatakiwa kukamilisha taarifa hiyo na kufikisha mezani kwake Jumatatu ijayo na kuonya kuwa atakayeficha taarifa hizo atachukuliwa hatua.
Agizo hilo limekuja siku moja baada Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue kuwaagiza makatibu wakuu kuwaelekeza wakuu wa idara kutoa taarifa hizo.za watumishi wote waliosafiri nje ya nchi baada ya agizo la Rais.
Rais Magufuli, siku moja baada ya kuapishwa, Novemba 5, alitangaza kufuta safari zote za watumishi wa Serikali nje ya nchi na kutaka shughuli walizokuwa wanakwenda kuzifanya, zitekelezwe na mabalozi waliopo kwenye nchi hizo, vinginevyo waende kwa gharama zao kama hawajapata kibali chake au cha Katibu Mkuu Kiongozi.
Juzi, Balozi Sefue aliagiza taarifa za mtumishi yeyote wa umma aliyesafiri nje ya nchi zipelekwe ofisini kwake ndani ya siku saba na kuhadharisha kuwa katibu mkuu ambaye hatafanya hivyo, ofisi yake (Sefue) itafanya uchunguzi na ikibaini udanganyifu wowote, atakuwa mtu wa kwanza kuwajibishwa.
Alipoulizwa juu ya taarifa hiyo kwa simu, Dk Mmbando hakupokea badala yake alituma ujumbe mfupi akisema yupo kwenye mkutano.
Msemaji wa Wizara hiyo, Nsachris Mwamaja aliliambia alisema taarifa hiyo haikuwa kwa ajili ya matumizi ya umma bali ni ya ndani.
“Watu wasiojua maadili ya utumishi wamevujisha. Hiyo ni taarifa ya ndani na haikutakiwa kufika kwenu (vyombo vya habari),” alisema Mwamaja.
Rais Magufuli alitangaza kufuta safari za nje kwa watumishi wa umma ili kubana matumizi ya fedha za Serikali na kuagiza kiasi kinachookolewa kielekezwe kutatua kero za wananchi.
No comments :
Post a Comment