Rais Yoweri Museveni wa Uganda
Mwaka 2016 ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu katika nchi mbalimbali za bara la Afrika.
Miongoni mwa nchi zinazotarajiwa kufanya uchaguzi mwaka huu; ni Uganda, Jamhuri ya Kongo Brazaville, Chad, Djibouti, Gabon, Equatorial Guinea, Gambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Ghana.
Baadhi ya nchi hizo tayari kumeshatokea mauaji ya kutisha kwa wananchi wake, huku wengine wakilazimika kuzihama kabisa nchi zao na kukimbilia nchi jirani.
Awamu ya kwanza ya Uchaguzi Mkuu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati ilifanyika Desemba 31 mwaka jana na ilipangwa kuwa awamu ya pili ya uchaguzi huo itafanyika Januari 31 mwaka huu baada ya kukosekana mgombea aliyepata zaidi ya nusu ya kura zilizopigwa.
Uchaguzi Mkuu Uganda utafanyika Februari 18. Katika uchaguzi huo, Rais Yoweri Museveni aliyetawala kwa kipindi cha miaka 30 atachuana na wapinzani wawili wakubwa ambao ni mpinzani wake wa siku nyingi yaani Dk Kizza Besigye na waziri mkuu wa zamani, Amama Mbabazi.
Wachambuzi walisema, Museveni atakabiliwa na ushindani mkubwa ikilinganishwa na chaguzi zilizopita.
Hata hivyo, anasisitiza kwamba, kutoungana vinara hao wawili wa upinzani na kukosekana umoja miongoni mwa kambi ya upinzani vitampa ushindi Yoweri Museveni japokuwa hautakuwa wa kishindo.
Rais wa Niger, Mahamadou Issoufou atajitosa tena ulingoni Februari 22 kuchuana na wapinzani ambao baadhi yao wanakabiliwa na kesi mahakamani.Jambo hilo linadhoofisha kambi ya upinzani na kutabiri ushindi wa mapema wa kiongozi huyo.
Mpinzani mkuu wa Rais Issoufou, Hama Amadou aliwahi kuwa waziri mkuu na Spika wa Bunge la Niger pia anakabiliwa na kesi mahakamani.
Taifa la Benin kutakuwa na uchaguzi wa rais utakaofanyika Februari 28 na utaamua hatima ya utawala wa Thomas Boni Yayi aliyeiongoza nchi hiyo tangu mwaka 2006.
Katiba ya Benin inasema kwamba, Boni Yayi haruhusiwi kugombea urais kwa mara ya tatu.
Mchuano mkali katika uchaguzi huo utakuwa baina ya Waziri Mkuu wa sasa wa Benin, Lionel Zinsou na mfanyabiashara, Patrice Talon.
Pia, Talon anatuhumiwa kuwa ndiye alipanga jaribio la mapinduzi dhidi ya Serikali mwaka 2012, alirejea Benin Oktoba mwaka jana baada ya kuishi uhamishoni kwa miaka miwili.
Jamhuri ya Congo Brazaville, mamlaka inayosimamia uchaguzi ilitangaza Machi 20 kuwa ndiyo siku ya uchaguzi huo, lakini vyama vya upinzani vinasema muda huo hautoshi kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi huru na wa haki.
Nchini Djibouti wapinzani wa Serikali wametishia kususia uchaguzi ujao uliopangwa kufanyika Aprili.
Rais Ismail Omar Guelleh ameiongoza Djibouti tangu mwaka 1999 na mwaka 2011 alifanya marekebisho ya katiba yaliyomruhusu kugombea nafasi hiyo kwa mara ya tatu mfululizo.
Baada ya kuapishwa, Omar Guelleh alikula kiapo kwamba hatagombea tena mwaka huu. Hata hivyo kuna tetesi kwamba huenda kiongozi huyo akagombea tena.
Gabon wanatarajia kufanya Uchaguzi Mkuu mwaka huu. Hadi sasa hakuna mwanasiasa aliyejinadi kwamba atagombea kiti hicho lakini inaonekana kuwa Rais Ali Bongo Ondimba aliyeongoza Taifa hilo tangu 2009 baada ya kufariki dunia baba yake, Omar Bongo, anataka kuwania kiti hicho kwa kipindi kingine cha miaka saba.
Uchaguzi Mkuu Kongo unapaswa kufanyika Novemba, lakini Rais Kabila anatakiwa kukabidhi madaraka baada ya kukamilisha vipindi viwili vya utawala.
Mjadala umeibuka nchini humo kuhusu nia ya chama tawala ya kutaka kufanya marekebisho ya katiba yatakayomruhusu kiongozi huyo kugombea kwa mara ya tatu.
Imeandaliwa na Hussein Issa kwa msaada wa mitandao
No comments :
Post a Comment