Wanasheria na watendaji wengine wa kada ya sheria wametakiwa kutenda haki katika kusimamia na kuendesha kesi kwa misingi ya kisheria.
Kinyume cha hapo, hatua kali zitachukuliwa dhidi yao ikiwamo kufukuzwa kazi, kwa yeyote atakayebainika kukiuka maadili ya utumishi wa umma ikiwamo kushiriki vitendo vya rushwa.
Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Harrison Mwakyembe (pichani), alisema jana kuwa hali ya utoaji haki kwa jamii ni mbaya tangu enzi za uhai wa Mwalimu Julias Nyerere, na imeleta picha mbaya kwa watendaji wa umma kuendekeza rushwa na kuacha kutoa huduma stahiki kwa jamii. Alisema serikali haitakubali kuendelea kufanya kazi na sampuli hiyo ya watendaji akimaanisha ‘wabovu’, badala yake wizara yake kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Biswalo Mganga, itawawajibisha mara moja.
“Sehemu mliyofika kiutendaji mnahitaji kutumbuliwa majipu yenu bila ganzi.
Hapa tunakwenda na kasi ya Rais, hivyo sheria itafuata msumeno na akitokea mmoja wenu anajihusisha na vitendo vya rushwa atawajibika. Hatuna muda wa kulea mambo ya kale hapa ni kazi tu,” alisema Dk. Mwakyembe. Alisema rushwa itaendelea kuitesa serikali kutokana na kuwa kiungo kimojawapo kinachorudisha nyuma maendeleo ya wananchi. Alisema wakati serikali inafanya maboresho kwa wanasheria hao itafanya mchakato wa kuwaondoa wahusika wa rushwa kwanza, kwa sababu Watanzania wamechoka na wanahitaji kasi ya mabadiliko ionekane.
Pia alisema pamoja na kupokea changamoto zinazowakabili wanasheria ikiwamo ya kutishiwa kuuwawa, kupigwa, kukosa vitendea kazi, mazingira, rasilimali fedha, amewaahidi kuimarisha usalama wao. Naye DPP Maganga alisema sekta hiyo imeanzisha kitengo kinachopambana na rushwa, ambapo kitadhibiti makosa dhidi ya binadamu, kesi za mtandao, ubinafsishaji wa mali za udanganyifu na makosa yanayofanyika mpakani mwa nchi.
Kwa mujibu wa Maganga, Septemba, mwaka jana, kesi nane zilizohusika na dawa za kulevya zilitolewa hukumu ambapo wahusika wamehukumiwa kifungo cha miaka 20 hadi 30 jela na faini ya Sh. bilioni 20.
Sambamba na hilo, Oktoba, mwaka huo, waliteketeza kilo 260 za dawa za kulevya aina ya heroine na cocaine.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment