Dar es Salaam. Zaidi ya wanafunzi 122,486 wa elimu ya juu wamenufaika na mkopo baada ya Serikali kutoa kiasi cha Sh459bilioni kwa ajili ya kugharamia masomo kwa mwaka wa masomo 2015/16.
Mkurugenzi wa Upangaji na Utoaji Mikopo ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), Onesmas Laizer alisema jana Dar es Salaam kuwa kwa mara ya kwanza bodi hiyo imefanikiwa kutoa kiasi hicho kikubwa toka kuanzishwa kwake mwaka 2006.
Laizer alisema kati ya wanafunzi waliopata mikopo hiyo, wa mwaka wa kwanza ni 53,618 na wengine ni 68,916 ni wanaoendelea na masomo.
“Tayari tumeshapeleka fedha hizi kwenye vyuo husika. Hata hivyo, kuna wanafunzi 1,659, wamekata rufaa kwa kutoridhika na mkopo waliopatiwa, tutapitia rufaa zao na tutawapa mikopo kabla ya mwezi huu haujamalizika,” alisema Laizer.
Alisema walitoa kipaumbele kwa wanafunzi wanaosoma programu za udaktari wa binadamu, meno, wanyama, famasia, uguuzi, ualimu wa masomo ya sayansi, hesabu, uhandisi wa umwagiliaji, yatima na walemavu.
Wakati huohuo; Bodi hiyo imewataka wanufaika wa mikopo na waajiri katika taasisi za umma na binafsi, kuhakikisha wanarejesha mikopo hiyo kwa wakati.
Ofisa Elimu na Uhusiano wa HESLB, Omega Ngole alisema sheria ya bodi hiyo inawataka waajiri kuwatambua waajiriwa wao ambao ni wanufaika na kuwakata sehemu ya mishahara kwa kiasi kisichopungua Sh50,000 na kuiwasilisha kwenye bodi kama marejesho ndani ya siku 15, baada ya kila mwisho wa mwezi.
Alisema kwa mwaka 2006 - 2017 walikusanya Sh53.6 milioni na 2014 - 2015 kilikuwa Sh21.7 bilioni na 2015-2016 walipata Sh12.1 bilioni.
“Tunatakiwa kukusanya Sh883 bilioni ndani ya miaka 10,” alisema.
Ngole alisema tayari Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ameanza kukagua kama taasisi za umma zinazingatia matakwa hayo na hatua za kisheria zitachukuliwa kwa watakaobainika kukiuka sheria.
No comments :
Post a Comment