MSIMAMIZI wa bomoabomoa inayoendeshwa Dar es Salaam, Heche Suguta ambaye pia ni mwanasheria wa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), amesimamishwa kazi.
Habari zinasema hatua hiyo imechukuliwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba.
Suguta ambaye ni wakili daraja la pili amesimamishwa kazi na wenzake wawili kwa kukiuka miiko ya kazi katika kusimamia kiwanda cha kusindika minofu ya punda kilichopo Dodoma.
Taarifa iliyotolewa na Idara ya Mazingira, Ofisi ya Makamu wa Rais jana ilieleza kuwa uamuzi huo umefikiwa baada ya kikao kilichoitishwa juzi na waziri huyo kuzungumzia njia za kuimarisha utendaji ndani ya wa NEMC.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa umekuwapo ukiukwaji wa makusudi na wa wazi wa miiko ya kazi katika kiwanda cha kusindika minofu ya punda uliofanywa na watumishi wa NEMC walioshughulika na kiwanda hicho.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Waziri ameagiza kusimamishwa kazi mara moja watendaji watatu wa baraza hilo.
Mbali na Suguta wengine waliosimamishwa ni Ofisa Mazingira Mwandamizi, Dk. Eladius Makene na Ofisa Mazingira, Boniface Kyaruzi.
“Waziri amewasimamisha kazi watumishi hawa wa Baraza kwa kukiuka miiko ya kazi katika kusimamia kiwanda cha kusindika minofu ya punda na kuagiza zichukuliwe hatua nyingine za nidhamu na sheria,” ilieleza taarifa hiyo.
Alisema mbali na kusimamishwa watumishi hao, zitafuata hatua nyingine za nidhamu na sheria kwa watendaji hao.
January pia ameagiza mamlaka husika kumpa barua ya onyo kali na la mwisho, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Bonaventura Baya kwa udhaifu katika usimamizi wa watumishi wa Baraza.
Barua hiyo ilitolewa baada ya kubainika kutakuwepo na usimamizi makini na thabiti kwa watumishi wa NEMC jambo linalosababisha malalamiko mengi kuhusu utendaji wa Baraza hilo.
“NEMC kama chombo muhimu nchini kilichopewa jukumu la kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira inatarajiwa kazi zake zifanyike kwa ufanisi wa kiwango cha juu kulingana na majukumu yaliyoko kwenye sheria,” ilieleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa kwa upungufu unaojitokeza January ameahidi kuunda jopo la wataalam wasiozidi watano ndani ya wiki moja kutathmini utendaji wa NEMC na changamoto mbalimbali katika usimamizi wa hifadhi ya mazingira na kuishauri Serikali ipasavyo.
Alisema ndani ya wiki hiyo pia litatolewa tangazo litakalokuwa na mambo mbalimbali ikiwamo anwani ya barua pepe, nukushi,namba ya simu, namba ya Whatsapp ili mtu yeyote mwenye malalamiko au aliyewahi kuombwa rushwa chochote na watumishi kinyume na maadili ya kazi yao atoe taarifa mara moja na kufanyika uchunguzi.
January pia ameagiza kuitishwa mkutano wa dharura wa bodi ya NEMC ndani ya wiki tatu kufanya uamuzi juu ya changamoto za utendaji katika Baraza.
No comments :
Post a Comment