dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Saturday, January 23, 2016

...Jecha atangaza uchaguzi Machi 20

Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha
By Salma Said/ Bakari Kiango, Mwananchi
Zanzibar/Dar: Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imetangaza Machi 20 kuwa ndiyo tarehe ambayo Uchaguzi Mkuu wa visiwa hivyo utarudiwa.
Saa chache kabla ya kutangazwa tarehe hiyo, wananchi mjini hapa walishikwa na butwaa baada ya ulinzi kuimarishwa katika maeneo mbalimbali kutokana na magari ya polisi kufanya doria zaidi mitaani.
Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, ambaye alitumia kituo cha televisheni cha Shirika la Habari la Serikali (ZBC) kutangaza kufuta uchaguzi, jana alitumia tena chombo hicho kutangaza tarehe ya uchaguzi wa marudio.
Jecha alisema uchaguzi huo utahusu uchaguzi wa Rais wa Zanzibar, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na madiwani.
Jecha alisema uchaguzi wa Zanzibar ulifutwa kutokana na kasoro mbalimbali zilizojitokeza katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 25 mwaka jana.
Hata hivyo, mwenyekiti huyo hakueleza ni kifungu gani cha sheria kilichompa mamlaka ya kutangaza kurudiwa kwa uchaguzi huo.
Kutangazwa tarehe hiyo ya uchaguzi, kumekuja ikiwa ni takribani siku 90 tangu Jecha atangaze uamuzi wa kuufuta Oktoba 28 mwaka jana. Juhudi za kutafuta suluhisho la kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi huo zilizowashirikisha Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein na katibu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, ambao wote waligombea urais, zilishindikana.
Tayari Maalim Seif ameshajitoa kwenye mazungumzo hayo yaliyohusisha vikao tisa.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF-Bara, Magdalena Sakaya hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo kwa kuwa alichelewa kupata taarifa.
Wazanzibari walipiga kura Oktoba 25, lakini Jecha alitangaza kufuta matokeo ya uchaguzi wa nafasi hizo siku ambayo alitakiwa kutangaza mshindi wa kiti cha urais.
Kabla ya kutangaza uamuzi huo, Jecha hakuonekana kwenye Hoteli ya Bwawani ambako ZEC walikuwa wakitumia kutangaza matokeo, na badala yake akaonekana kwenye kituo cha televisheni akitangaza kufuta matokeo na kuahidi kuitisha uchaguzi mpya baada ya siku 90. 
Kauli ya Jecha ilipingwa vikali na wanasiasa, wanaharakati na wanasheria kutoka Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS) kwa madai kwamba hakuna kifungu cha sheria kinachotoa mamlaka ya kufuta kwa uchaguzi.
Mbali na hao, viongozi na wanachama wa CUF walitangaza kususia uchaguzi endapo utatangazwa kurudiwa, wakiamini kuwa ulishafanyika na baadhi ya wawakilishi walishatangazwa kushinda na kupewa hati za ushindi, kitu kinachomaanisha kuwa pingamizi dhidi yao lilitakiwa lipelekwe mahakamani.

No comments :

Post a Comment