dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Saturday, January 23, 2016

Membe apinga uchaguzi wote kufutwa Zanzibar!





Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Serikali iliyopita, Bernard Membe
   
By Exuperius Kachenje, Mwananchi
Dar es Salaam. Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe amepinga uamuzi wa kufutwa kwa matokeo yote ya uchaguzi visiwani Zanzibar akisema dunia inashangaa, na akaitaka CCM na Serikali isiwaachie watu wawili tu kutafuta njia za kutatua mgogoro huo.
Membe anakuwa mwanasiasa wa kwanza mwandamizi kutoka chama tawala kuonyesha waziwazi kutoridhishwa na uamuzi wa kufuta uchaguzi huo wa Rais wa Zanzibar, wawakilishi na madiwani ambao ulifanyika sambamba na uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, wabunge na madiwani wa Bara na Visiwani.
“Kinachoishangaza dunia si kuahirisha uchaguzi, bali ni kufuta matokeo ya majimbo yote,” alisema mwanadiplomasia huyo katika mahojiano maalumu na waandishi wa gazeti hili mapema wiki hii.
Uchaguzi wa viongozi wa Zanzibar uliofanyika Oktoba 25 sambamba na Uchaguzi Mkuu, ulifutwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salim Jecha Oktoba 28 kwa maelezo kuwa sheria na taratibu zilikiukwa na akaahidi kuitisha uchaguzi mwingine baada ya siku 90 zinazomalizika wiki ijayo.
Chama kikuu cha upinzani visiwani, CUF, ambacho kilimsimamisha Maalim Seif Sharif Hamad kugombea urais, kinapinga uamuzi huo kikisema si mwenyekiti wa tume wala ZEC wenye mamlaka ya kufuta matokeo na kutaka mshindi atangazwe ili chama hicho kwa kushirikiana na CCM vikutane kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
Katika kujaribu kutatua mgogoro huo, Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein na Maalim Seif wameshafanya vikao tisa Ikulu Zanzibar pamoja na marais wa zamani wa visiwa hivyo, Dk Amani Karume, Dk Salmin Amour na Ali Hassan Mwinyi, bila ya mafanikio na tayari katibu huyo mkuu wa CUF ameshatangaza kujitoa kwenye mazungumzo hayo.
Akizungumza kuhusu mgogoro wa kisiasa visiwani, Membe alisema inashangaza kuona uchaguzi ulifutwa kwenye majimbo yote, badala ya yale yaliyokuwa na matatizo.
“Kilichotokea Zanzibar  kimeihuzunisha dunia,” alisema mbunge huyo wa zamani wa Mtama mkoani Lindi. “Watanzania waelewe, kilichoishitua dunia ni kule kufuta matokeo kwa ujumla wake. Yaani majimbo yote hakuna hata moja lililofanya vizuri? Hapa ndipo tunapata kigugumizi. Sasa tunakwenda wapi, tunafanya kitu gani?
“Ilitakiwa kuwe na ubaguzi; majimbo mawili, matatu, manne, matano, haya hayajafanya vizuri ndiyo uchaguzi urudiwe. Kaubaguzi kale kangewekwa, hiyo ingefanana na sura ya dunia ya haki.”
Waziri huyo mstaafu aliyehudumu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa miaka tisa, pia haridhishwi na jinsi mgogoro huo wa kisiasa unavyotafutiwa ufumbuzi kutokana na kuwahusisha zaidi Dk Shein na Maalim Seif.
“Kama kuna mwanasiasa anadhani tatizo la Zanzibar litamalizwa na sehemu moja ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pekee, anafanya makosa makubwa,” alisema Membe.
“Umoja wetu na Zanzibar ni umoja wa kusaidiana wakati wa raha na matatizo. Hili ni tatizo ambalo linaweza kuhatarisha si tu usalama wa Zanzibar, bali pia Muungano wetu. Hatuwezi kukaa tu na kuangalia.
“Chama chetu na Serikali yetu lazima vishiriki kwa vitendo na kauli kumaliza mgogoro wa Zanzibar na ikiwezekana wahamie huko. Hili tatizo ni kubwa.”
Membe alisema katika mgogoro huo, Watanzania wa Bara wana haki  ya kujua kinachozungumzwa ili kushauri kwa lengo la kudumisha Muungano.
 “Kuwaacha viongozi wawili tu wanakutana kila siku kwa muda wa mwezi mzima au miezi miwili na hujui kinachoendelea si sahihi. Huwezi kujua kinachoendelea,” alisema.
“Kuna mambo makubwa yanayoendelea, lakini hawataki tu kutuambia. Msije mkadanganyika kwamba wanakutana mle, wanakunywa chai, wanaondoka halafu mnasema hakuna kinachoendelea.”
Wakati ZEC imetangaza Machi 20 kuwa tarehe ya kurudia uchaguzi, CUF imekuwa imeshasema kuurudia si suluhisho na haitakubalika, badala yake ameitaka Tume kutangaza mshindi.
Membe, ambaye alikuwa mmoja wa makada 38 wa CCM waliojitokeza kuomba ridhaa ya kugombea urais lakini akaishia kwenye tano bora, alikuwa pia na maoni yake kuhusu kurudiwa kwa uchaguzi.
“Lazima uangaliwe kwa mapana, tusiangalie kama turudie uchaguzi au tusirudie. Tusifikiri viongozi wa Zanzibar wakikutana wanaulizana swali  hilo tu kwamba ‘turudie uchaguzi au tusirudie’. Hapana,” alisema Membe aliyeshiriki kutatua migogoro mbalimbali barani Afrika.
“Wenzako swali hilo ni dogo sana. Huenda wako kwenye swali kubwa. Wanaweza kuuliza swali kama ‘hivi tatizo la Zanzibar ni kitu hiki au kuna tatizo kubwa zaidi ya hapa’. Hivi mnaweza kukaa saa tatu au nne mkaulizana tu kwamba, ‘turudie, tusirudie, turudie tusirudie?’”
Waliohama CCM wananitia kichefuchefu
Membe pia alizungumzia kitendo cha baadhi ya wanachama wa CCM walioamua kutimkia upinzani wakati wa harakati za Uchaguzi Mkuu, akisema wanamchefua.
Akijibu swali lililotaka kujua anavyowazungumzia na kujisikia kuhusu watu hao, Membe alisema: “Nikionana nao najisikia kichefuchefu. Tena ukiwaona waambie, chama kichukue hatua kwa wasaliti.”
Alisema zipo taarifa za baadhi ya waliohama CCM kutaka kurejea, akashauri kisiwapokee tena.
“Nasikia wanataka kurudi, wasipokewe, hawa wasirudi,” alisema Membe ambaye alikuwa akichukuliwa kuwa mpinzani mkubwa wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kwenye kinyang’anyiro cha urais ndani ya CCM.
Lowassa alihamia upinzani baada ya kuenguliwa na CCM na akapitishwa na Chadema kugombea urais.

No comments :

Post a Comment