Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, January 24, 2016

KONA YA MAKENGEZA : Hii ni bomoa-komoa

 Image result for bomoabomoa
By Richard Mabala
Waishiwa wenzangu, leo nawaletea kitendawili. Kuna watu wamependekeza kubadilisha neno la Kiswahili. Hawataki neno Serikali kwa kuwa inaleta wazo kwamba ukali ni msingi wa uongozi. Hivyo wengine walipendekeza iitwe Serikazi kuonyesha kwamba jukumu lake kweli ni kazi, kazi ya kutuhudumia sisi wananchi. Lakini mwingine akaleta neno la Serijali.
Hapo ukazuka mjadala mkali. Wengine walisema kwamba maana yake ni seri-jali, yaani inawajali wananchi na kuweka maslahi yao mbele daima. Serikali ni kama baba. Lakini wako wengine waliopinga vikali sana na kusema tafsiri yake ni se-rijali. yaani Serikali ni rijali, ni dume, inaweza kufanya jambo lolote, tena kwa nguvu na ubabe, haishindwi.
Sasa katika mjadala huu, nimepokea maoni ya watu wengi kuhusu zoezi la bomoabomoa. Ni bomoabomoa kweli au ni bomoakomoa?
Ndiyo, unapopita Barabara ya Morocco na kuangalia hali ya pale, imekuwa seri-jali? Kutokana na tishio la mafuriko, kubomoa nyumba za watu wote hadi mlimani kabisa ni kuwajali watu, kuwakomboa? Au ni se-rijali? Sisi madume, mtatuweza wapi? Tunarudisha utawala wa sheria na ole wenu mliokaa huko!
Hebu tusikie maoni yao
Ninakujua Makengeza,
Ninakujua na upumbavu wako wa kuwajali wadogo hadi unatetea vitetea vya ujinga. Ninakujua na kelele zako za haki za binadamu, bila kutaka kutambua kwamba bila damu ya binadamu hakuna haki. Ndiyo. Serikali ni kali, ni se-rijali, ni babe si baba. Tunachofanya sasa ni kurudisha utawala wa sheria na watakaoumia shauri yao.
Wewe hujui kwamba Se-rijali inafanana na Mungu. Inaangalia, inatamka, inatekeleza. Basi! Na wanaopinga wataswagwa tu. Huoni mafanikio yetu? Tunaamka na kusema shule za sekondari ziwepo. Hazijakuwepo? Zimejaa kila kona. Potelea mbali kama hakuna walimu wala vitabu, potelea mbali kwamba wengine wanalalamika kiwango cha elimu kimeshuka. Si hoja. Hoja ni kwamba tumesema shule ziwepo, na zimekuwepo.
Haya na maabara pia. Kudengua kunasaidia nini? Serikali, rijali, inaamka, inaangalia, inatamka na kutekeleza. Tulisema, maabara yawepo. Na atakayekaidi amri hii aswagwe. Wacha watu wahangaike, na matokeo yake ni nini? Maabara yapo. Hata kama walimu wa sayansi hawapo, na vifaa vya sayansi havipo, maabara yapo kwa kuwa tumetamka yawepo. Torati yasema: Ikawa jioni, ikawa asubuhi, Se-rijali imefanikiwa.
Na vivyo hivyo tunaweza kuamka na kubomoa pia. Utafiti wa nini? Maandalizi ya nini? Maandalizi ni kutafuta nyenzo zinazofaa na kuanza kazi ya kubomoa wasiotakiwa. Wengine wakiumia shauri yao. Kama inasababisha kupindupindu au malaria, potelea mbali, ndiyo gharama za maendeleo. Mtalalamika, mtachoka na Serikali itabaki na urijali wake. Nakuambia Makengeza, pinga uone
Barua ya pili ilikuwa tofauti sana.
Bwana Makengeza,
Tangu nilipokuwa mwanafunzi shuleni, nilichukia sana mtindo wa adhabu kwa wote kwa makosa ya wachache. Mwanafunzi mmoja anapiga kelele, darasa zima linachapwa, au kulazimishwa kulima. Baadaye nilipokuwa mwalimu nilielewa kwamba lazima walimu wanapenda hii maana ni rahisi kutekeleza lakini bado sijasahau hisia zangu za hasira kwa nini niadhibiwe kwa makosa ya wengine.
Na polepole nilianza kuelewa kwamba mbinu kama hizo zinatumika dhidi ya wasio na uwezo tu. Ukiwa tabaka la chini utabakwa tu. Hebu ona. Hawa watu wote wanabomolewa nyumba zao na miongoni mwa sababu zinazotolewa ni kwamba ni wakaidi, wengine wamelipwa fidia, wengine wamepewa hata viwanja sehemu nyingine lakini wakauza na kurudi papohapo. Kwa hiyo wote waadhibiwe kwa makosa ya wachache. Hakuna cha huruma tena.
Basi tutumie mantiki hii kwa maeneo mengine. Kwa kuwa waheshimiwa wa sponji wengine wamehusishwa na ufisadi, tuwafukuze wote na kuwapeleka mahakamani. Naam. Na kwa kuwa kuna walimu wazembe, basi walimu wote wakatwe mshahara kama adhabu ya uzembe wao.
Upumbavu? Kabisa. Lakini ndiyo mantiki ya vita pia ya kudondosha mabomu, ili watu wa tabaka la chini wauawe kwa sababu ya ukaidi wa wakubwa wao. Unamshindwa mkubwa hivyo unamaliza hasira zako kwa wadogo.
Ndiyo maana nashindwa kuamini kwamba Mheshimiwa Mkuu ameamuru wadogo wateswe hivyo. Yeye alipoingia alilenga bomoabomoa ya watu wanaokwamisha mipango yote, wezi wakubwa wa mali yetu, wasababishi wa mateso katika jamii, wapinga maendeleo kwa vitendo vya ubinafsi. Na mambo yamebadilika tayari na naamini akiendelea na bomoabomoa hii, kweli tutaanza kunusa nchi ya maziwa na asali.
Sasa inavyoonekana wenzake walio wengi hawataki bomoabomoa ya wanene hao, watu ghorofa, bali wanamaliza hasira zao kwa watu wa hali ya chini. Sikatai kwamba wengine kule ni wakorofi pia, wameshapewa eneo wakauza, wanakaidi kuhama lakini maafa yakitokea wanataka msaada ya Serikali tu. Lakini ni wote? Nashukuru kwamba hatimaye Serikali (jali) imetoa tamko kuhusu zoezi lakini bado nabaki na maswali.
Iwapo Serikali inaweza kujenga kituo kikubwa cha mabasi ya kasi na kuwa na uhakika kwamba hakitadhurika na mafuriko, kwa nini haiwezi kufanya hivyo kwa wananchi? Iwapo waliweza kujaza vifusi kibao huko Mikocheni kwenye eneo la ardhi uoevu ili tabaka la maghorofa liweze kujenga mahekalu yao, wameshindwa nini huko Msimbazi? Na tusisahau kwamba huko Mikocheni, hawa wamahekalu wamesababisha mafuriko mengi kwa wengine wa hali ya chini mwanzoni lakini wamahekalu waliendelea na mipango yao.
Pia Makengeza, usifikiri kwamba sielewi tatizo na kwamba Serikali inadai kujali katika urijali wao. Lile ni eneo la hatari, hatutaki watu wadhurike. Sawa. Lakini vitendo vyaonyesha tofauti na kujali.
Sijaelewa mantiki ya kuwakomboa watu wasisombwe na mafuriko, kwa kuwaweka kwenye mazingira ya kuuliwa na kipindupindu au malaria hata kabla ya mafuriko kuja. Iwapo kweli ni seri-jali, kwa nini haikufanya maandalizi yoyote kwa kujua ukibomoa eneo kubwa namna hiyo lazima watakuwepo wengi ambao wataathirika vibaya sana.
Lakini baada ya kuwaacha pale wakihangaika, se-rijali inathubutu kutamba kwamba hakuna mahali pa kuwaweka. Sasa tamko la jana linasema kwamba wamegundua kwamba wengi pale ni wapangaji, hawana pa kwenda, hawakujua hivyo kabla? Kweli? Na sasa hakuna msaada wa serikali, wala mashirika, wala maAZAKI, wala mashirika ya dini. Ni kama hawa si Watanzania wenzetu.
Masuala magumu
Haya, na mwisho tujiulize kwa nini watu hawataki kuhama pale. Si wajinga. Kazi zao, biashara zao, zipo katikati ya mji. Wakibwagwa huko Mabwepande na kwingineko, mbinu zao za kujikimu zimekwisha. Ndiyo maana wanajua kuna hatari ya mafuriko, na wanajiandaa kwa hilo. Kwa kiingereza tunasema wanafanya ‘calculated risk taking’. Huwezi kuwafukuza watu. Watarudi tu.
Kwa hiyo, mwisho nasema, nikiangalia tofauti kati ya mahoteli makubwa, na Mikocheni upande mmoja na hawa wenzetu wa bondeni upande wa pili, inabidi niseme kweli kuna matabaka mawili. Kwa wanene, utawala wa sheria, kwa wakondefu utaliwa na sheria.
Kwa wanene, mipango inafanyika, inaandaliwa, na kutekelezwa kwa umakini, kwa wakondefu hakuna sababu ya kufanya hivyo, bomoa twende tu, swaga twende tu, tena swaga kwa swaga kubwa ya wanene. Narudia kusema kwamba siamini kwamba ndio maana hali ya H2K. Kazi msingi wake ni umakini katika maandalizi, ni kufanya uchunguzi vya kutosha na kuchukua hatua ambazo zinawajali watu. Na bomoabomoa hasa ni kwa wale wanaosababisha hali ya wananchi kuteseka, si kwa wale wanaoteseka na mfumo.
Duh! Huu mjadala ni sheeeeda. Seri-jali au Se-rijali?

No comments :

Post a Comment