Historia na elimu
Kassim Majaliwa ni Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Tano. Ndiye mtu wa kwanza kuteuliwa na Rais John Magufuli kushika wadhifa huo baada ya kuwa mbunge wa Jimbo la Ruangwa mkoani Lindi tangu mwaka 2010. Kwa sasa ana umri wa miaka 55 na ifikapo Desemba mwaka huu atafikisha miaka 56 kwa kuwa alizaliwa Desemba 22, 1960 Ruangwa mkoani Lindi.
Majaliwa alianza darasa la kwanza mwaka 1970 katika Shule ya Msingi Mnacho, Ruangwa na kuhitimu darasa la saba mwaka 1976. Mwaka 1977 hadi 1980 aliendelea na elimu ya Sekondari katika Shule ya Sekondari Kigonsera. Mwaka 1981 hadi 1983 alisoma na kuhitimu stashada ya Ualimu katika Chuo cha Ualimu Mtwara.
Majaliwa alipata fursa ya kujiendeleza kimasomo mwaka 1994 alipojiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako alitunukiwa Shahada ya Kwanza ya Elimu mwaka 1998 na rekodi zinaonyesha kuwa mwaka 1999 alisoma Stashahada ya Uzamili katika Elimu (Postgraduate Diploma in Education) kutoka Chuo Kikuu cha Stockhom nchini Sweden.
Kwa hakika hakuna ushahidi wa kutosha ikiwa kiongozi huyu alihitimu stashahada hiyo na pia hakuna taarifa sahihi juu ya elimu yake ya kidato cha tano na sita. Majaliwa amemuoa Mary.
Uzoefu
Waziri Majaliwa aliajiriwa serikalini mwaka 1984 kama mwalimu. Alianzia kazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Lindi na kufundisha kwa miaka minne hadi mwaka 1986. Mwaka 1988 aliendelea na kazi ya ualimu akifundisha Shule ya Sekondari Kazima, mwaka 1988 hadi 2000 aliajiriwa kama mkufunzi wa Chuo cha Ualimu Mtwara. Mwaka 2000 hadi 2001 alichaguliwa kuwa Katibu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) ngazi ya wilaya na kuanzia mwaka 2001 hadi 2006 alikuwa Katibu wa Mkoa wa CWT.
Rais Jakaya Kikwete ndiye alimuibua Majaliwa hadi kwenye siasa za kitaifa mwaka 2006 kwa kumteua kuwa Mkuu wa Wilaya katika Wilaya ya Urambo mkoani Tabora na baadaye Rufiji, Pwani.
Majaliwa alijitosa kwenye mbio za ubunge katika jimbo la Ruangwa mwaka 2010 na akaongoza kura za maoni na kupitishwa na CCM. Alishiriki uchaguzi mkuu Oktoba 2010 na kupata ushindi wa kura 27,671 (sawa na asilimia 72.98) dhidi ya Abubakar Kondo wa CUF aliyepata kura 9,024 (asilimia 23.8). Baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge, aliteuliwa na Rais Kikwete kuwa Naibu Waziri wa Tamisemi. Majaliwa amedumu kwenye unaibu waziri hadi Serikali ya JK ilipomaliza muda wake Novemba, 2015.
Kwenye uchaguzi wa Oktoba 2015, Majaliwa alijitokeza tena kwa mara ya pili na kuongoza kura za maoni ndani ya CCM kwa kura 11,988 dhidi ya kura 2,678 za Bakari Nampenya. Kwenye uchaguzi wa ubunge, alipata kura 31,281 dhidi ya 25,506 za mgombea wa CUF, Omar Makota.
Mwanasiasa huyo mwenye bahati aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Novemba 19, 2015. Kwa sababu ni wajibu wa kikatiba wadhifa huu kuthibitishwa na Bunge kwa kura za siri - alipigiwa kura na wabunge 258 kati ya 351 walioshiriki, na kupitishwa kwa asilimia 73.5 ya wabunge na kesho yake akaapishwa rasmi kuwa Waziri Mkuu. Majaliwa ndiye mtu wa 11 kuwa Waziri Mkuu tangu Tanganyika ilipopata uhuru mwaka 1961 na baadaye kuungana na Zanzibar, Waziri Mkuu wa Kwanza alikuwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Majaliwa ni mpenzi mkubwa wa mpira wa miguu. Ni mwalimu na mkufunzi wa walimu wa mpira huo. Ameshiriki katika kozi mbalimbali za ukocha na kutunukiwa vyeti; mwaka 1984 cheti kimoja, mwaka 1990 nyeti viwili, mwaka 1996 stashahada ya ukocha na mwaka 1998 kozi ya Mkufunzi Msaidizi wa Mpira wa Miguu. Ndani ya Bunge, kati ya mwaka 2011 hadi 2015 alikuwa kocha wa timu ya mpira wa miguu ya Bunge.
Nguvu
Kwanza, Majaliwa ni kiongozi mchapakazi na mtendaji. Wakati wote alipokuwa Naibu Waziri wa Tamisemi, wengi walimchukulia hivyo. Naambiwa kila alipofika ofisini kwake alianza kazi moja kwa moja na angetoka jioni sana. Watendaji wa Tamisemi wamekuwa wakimtambua kama mtu anayefanya kazi bila maneno mengi. Jambo hili linaweza kumsaidia hata katika wadhifa wa sasa.
Jambo la pili ambalo linambeba Majaliwa ni usikivu na kuwa karibu na watu. Jimboni kwake wananchi wanamtaja hivyo lakini wakilalamika kuwa majukumu ya unaibu waziri yalipomzidi aliwatelekeza. Magdalena Sakaya, mbunge wa jimbo la Kaliua mkoani Tabora na Naibu Katibu Mkuu wa CUF, anamtaja Majaliwa kama mtu msikivu na aliyemsaidia sana wilayani Urambo hasa yalipotokea matatizo ambayo watendaji wa chini walishindwa kuyatatua. Maoni ya Sakaya aliyatoa mara tu baada ya Majaliwa kupendekezwa kuwa Waziri Mkuu na kutangazwa ndani ya Bunge.
Jambo la tatu kubwa linalomuongezea uzito katika nafasi yake ni ile hali ya kuwa “mtu wa kawaida”. Huko nyuma tumewahi kuwa na mawaziri wakuu kadhaa ambao kwa haiba zao walionekana kama watu wa juu na wanaotaka kusikilizwa zaidi. Baadaye alikuja Mizengo Pinda, mtu wa kawaida kabisa kwa haiba na bahati hiyo imejitokeza kwa Kassim Majaliwa. Mchambuzi wa Masuala ya Kijamii na Kisiasa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Kitila Mkumbo aliwahi kusoma na Majaliwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kitila anamtaja Majaliwa kama “mtu mwenye utulivu wa akili na asiye na majivuno,” hivi ndivyo pia anatajwa na wanafunzi wengine kadhaa aliosoma nao, akiwamo Herieth Mangu, ambaye ni mtumishi wa umma anayefanya kazi Dar es Salaam.
Jambo la nne, kiongozi huyu ana uzoefu wa utendaji kuanzia ngazi ya chini. Watu wa aina yake huwa wanakuwa na umakini mkubwa kuliko wale ambao hupata vyeo vya juu haraka bila kuanzia chini kidogo. Ikumbukwe kuwa Majaliwa alianza kazi akiwa mwalimu wa ngazi ya chini, akapanda na kuwa mwalimu wa Chuo cha Ualimu kisha akawa kiongozi wa walimu baadaye akawa Mkuu wa Wilaya kwa miaka minne. Baadaye tena akachaguliwa kuwa mbunge kwa miaka mitano na kuwa Naibu Waziri kwa miaka mitano kabla ya kurushwa na kuwa Waziri Mkuu. Mahali pa pekee unakoweza kusema amerushwa haraka ni kutoka kuwa Naibu Waziri hadi Waziri Mkuu, jambo ambalo huwa ni nadra sana kutokea.
Na mwisho, kiongozi huyu hana historia mbaya katika utendaji wake. Haijawahi kuthibitika popote kwamba amewahi kuhusika na masuala ya kukosa uaminifu na uadilifu, masuala ambayo ni muhimu sana kwa wadhifa wake wa sasa.
Udhaifu
Pamoja na kwamba Majaliwa ana historia nzuri ya utendaji, nadhani hiyo ni kwa sababu alikuwa na madaraka madogo na “ya kutumwa” zaidi kuliko kushauri na kusimamia kwa miguu yake mwenyewe. Kwa hatua ya sasa ameanza kutuonyesha sura tofauti kidogo, anaonekana kama mtendaji anayetumwa zaidi na Rais wake kuliko kuonyesha dalili za kujisimamia.
Alipokuwa katika jimbo lake la Ruangwa mwanzoni mwa mwaka huu aliongea na kutoa maagizo kwa vyombo vya usalama nchi nzima akizuia wagombea walioshindwa uchaguzi wa oktoba 25 mwaka jana kufanya mikutano ya kuwashukuru wananchi. Majaliwa alisisitiza kuwa huo ndio msimamo wa Serikali. Wachambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii, asasi za kiraia na vyama vya siasa visivyoongoza dola viliishangaa kauli ile na kuichukulia kama “kauli hatari” kuwahi kutolewa na mtu wa hadhi ya Waziri Mkuu katika zama za sasa ambazo serikali zote duniani zinalo jukumu la kwanza la kukuza demokrasia na kulinda haki za kiraia.
Majaliwa asingekubali Serikali yake ichukue uamuzi ambao unavunja Ibara za 18 (1), 18 (2), 20 (1) na 21 (1) za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, zikisomwa pamoja na kifungu cha 11 cha Sheria namba 258 ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002. Sheria hizo zimeeleza kwa uwazi kuwa vyama vya siasa na waliomo ndani yake watakuwa na haki na wajibu wa kufanya mikutano, na Serikali itawapa ulinzi. Wachambuzi wa mambo na wakosoaji wa Majaliwa wanaanza kutabiri kuwa huenda katika miaka mitano ijayo akawa si msaada kwa Rais kwenye ushauri kwa kuwa asili ya Rais wa sasa inaweza kumuogofya na asiwe na jambo la kumpa changamoto mkubwa wake huyo. Hatari ambayo inaikabili nchi yoyote ile ni kuwa na washauri wa karibu wa Rais kikatiba ambao ni waoga na wanasubiri au kupendekeza yale anayoyapenda Rais. Majaliwa ameanza uwaziri mkuu kwa mguu wa kushoto na kama hatasimama, akageuka nyuma, akakumbuka mambo mengi yaliyompa sifa na kujenga taswira yake thabiti, atashindwa kuwa Waziri Mkuu bora.
Kwa vyovyote vile, Waziri Mkuu imara hawezi kukubali Serikali yake na Rais wake wafikie uamuzi wowote unaovunja sheria na katiba ya nchi kwa makusudi bila kuwa na hofu. Waziri Mkuu wa namna hiyo atakuwa ni tatizo hata kabla hajamaliza miaka yake mitano.
Matarajio
Matarajio ya Majaliwa lazima yawe kwenye kuipaisha Serikali ya sasa, ambayo walau inaye Rais anayefanya maamuzi na yuko tayari kusimamia masuala ya msingi kila anapoona inapaswa kufanyika hivyo. Majaliwa anatambua pia kwamba kwa sababu JPM hatabiriki sana, asipoitendea haki nafasi hii aliyokabidhiwa, huenda akajikuta anakosa nafasi kwenye awamu ijayo, jambo ambalo hawezi kukubali limtokee.
Wananchi walio wengi kwa ujumla wanahitaji kuwa na Waziri Mkuu msikivu na anayechukua hatua. Awamu iliyopita ilikuwa na Waziri Mkuu msikivu, lakini mwenye kigugumizi kwenye ufanyaji uamuzi. Hali hiyo ilimuangusha na wengi wanatarajia kwamba Majaliwa atakuwa amejifunza mengi na kusikia malalamiko mengi dhidi ya Waziri Mkuu aliyepita ambaye alikuwa ni bosi wa Majaliwa.
Changamoto
Changamoto ya kwanza inayomkabili Majaliwa ni namna atakavyojipanga kwenye eneo la kumshauri Rais katika kufanya uteuzi wa nafasi mbalimbali. Katiba ya Tanzania bado inatoa mamlaka na madaraka makubwa kwa Rais kufanya uteuzi wa watu wanaoshika nyadhifa kubwa serikalini na kwenye taasisi za umma. Mathalani, Rais anapaswa kuteua mabalozi, wakuu wa mikoa na wilaya, wakurugenzi wakuu au watendaji wa mashirika ya umma. Ili uteuzi huu uwe na tija, ni lazima Waziri Mkuu awe mfuatiliaji wa kila jambo kwenye nchi na mfuatiliaji wa kila mtendaji makini. Rais anapotaka kuteua lazima Waziri Mkuu “amshtue” haraka kama uteuzi huo si sahihi au mteuliwa si mtu sahihi. Hii ni changamoto kubwa kwa sababu itamtaka Majaliwa awe na taarifa za kutosha.
Pili, kuna changamoto kubwa kwenye eneo la usimamizi wa mawaziri. Mara nyingi mawaziri wanao wataalamu na watendaji kwenye wizara zao na hutokea waziri akawa na weledi mkubwa katika wizara yake kuliko Waziri Mkuu. Majaliwa ni mtu wa kawaida sana hata kwenye elimu yake, lakini anawasimamia mawaziri wengi wenye elimu na uzoefu mkubwa kumshinda. Lazima naye sasa ajenge uwezo wa kiusimamizi ambao utaheshimiwa na mawaziri hawa. Vinginevyo anaweza kujikuta yeye ndiye anapokea maelezo ya nini cha kufanya kutoka kwa mawaziri kwa sababu wanazijua vizuri wizara zao na wamebobea kuliko yeye.
Tatu, Waziri Mkuu ndiye daraja muhimu kati ya Bunge na Serikali. Hii ni changamoto ya kipekee. Tayari huko nyuma tuna historia zilizoonyesha namna mawaziri wakuu walivyoshindwa kuiwakilisha vizuri Serikali bungeni, au kujiwakilisha wao na wale wanaowasimamia. Kumekuwa na tabia ya mawaziri kutojibu hoja wanazoelekezewa na kisha hutegemea kulindwa na Waziri Mkuu. Majaliwa analo jukumu gumu la kuwabana mawaziri wake watimize wajibu wao ndani na nje ya Bunge na ikiwezekana awape maelekezo bungeni na hadharani pale wanapokuwa hawatimizi wajibu. Kama anaongoza serikali ya “Hapa Kazi Tu”, bila shaka kazi haziwezi kwenda ikiwa Waziri Mkuu anawaacha mawaziri wake wasitimize wajibu wao.
Mwisho, Majaliwa anazo changamoto mtambuka zinazoihusu Serikali kwa ujumla. Unapoitwa “msimamizi mkuu wa serikali na mawaziri” maana yake wewe ndiye kila kitu kuhusu hiyo serikali inayotajwa. Kila jema litakalotendwa na serikali utasifiwa, kila baya litakalotendwa na serikali litakuangukia kwako. Waziri fulani akichukua rushwa mahali, lazima na Waziri Mkuu wake naye atachunguzwa ikiwa alishirikiana naye na hata kama Waziri Mkuu hakuhusika kwa njia yoyote ile bado atahojiwa alichukua hatua gani na kama atasema hakujua jambo hilo ataulizwa, kwa nini anaendelea kuwa Waziri Mkuu ikiwa hajui nini mawaziri wake wanafanya. Mfano mwingine, ikiwa utoaji wa elimu bure utazua changamoto nyingi kupita kiasi, wa kwanza kuulizwa kwa sasa ni Waziri Mkuu. Lazima Majaliwa ajipange sana ili asije kuingia kwenye historia ya watu waliowahi kuwa mawaziri wakuu na hawakuitendea haki nafasi hiyo.
Hitimisho
Serikali ya mwaka huu imekuwa ni ile ya “kuokota maembe dodo kwenye jangwa.” Watu waliokuwa wanapewa nafasi kubwa kupitishwa na CCM kuwa “wagombea urais” hawakupita, akaja JPM ambaye nafasi yake haikuwa kubwa kuwashinda. Vivyo hivyo ilipofika wakati wa kupendekeza mgombea mwenza wa CCM, JPM alimpendekeza mtu ambaye wengi hawakutarajia na ndiye Makamu wa Rais leo. Kwenye Uwaziri Mkuu ndiyo kabisa, hakuna mtu aliyempa nafasi Majaliwa, na hata Majaliwa mwenyewe hakutegemea wala hakuamini, alishtukizwa.
Mtego mmoja ambao Majaliwa ametwishwa na huenda haujui, ni kwamba marais wengi wa nchi za Afrika huteua mawaziri wakuu wasio na nguvu ili wawadhibiti. Mawaziri hao wengi hukubali kudhibitiwa na mwisho wa siku humaliza zama zao za uongozi wakiwa hawasikiki na kujulikana wala kuacha alama muhimu. Wakubwa wao ndiyo hushikilia kila kitu, hadi akili na fikra zao.
Namtakia Majaliwa kila la heri lakini lazima ajiongeze na kutambua kuwa wadhifa wake ni wa kikatiba na anayo nafasi kubwa katika kumsaidia Rais kufanya mabadiliko nchini kwa kutumia njia sahihi, zinazokubalika kikatiba na kisheria na zenye nia njema.
*Uchambuzi huu unatokana na utafiti na maoni binafsi ya mwandishi.
Kuhusu mchambuzi
Julius Mtatiro ni Mchambuzi wa Masuala ya Kisiasa na Kijamii, ni mmoja kati ya vijana wenye uzoefu mkubwa na siasa za Tanzania. Ana Cheti cha Juu cha Sarufi (“Cert of Ling”), Shahada ya Sanaa “B.A” katika Elimu (Lugha, Siasa na Utawala), Shahada ya Umahiri ya Usimamizi wa Umma (MPA) na Shahada ya sheria (L LB) – Simu: +255787536759, Tovuti: www.juliusmtatiro.com, Email; juliusmtatiro@yahoo.com).
/Mwananchi.
No comments :
Post a Comment