WAFANYAKAZI 350 wa kiwanda cha Sukari Mahonda wapo katika hatari ya kupoteza ajira baada ya shamba la miwa la kiwanda hicho kuchomwa moto kwa mara ya pili ndani ya kipindi cha siku tano, mkoa wa Kaskazini Unguja.
Hayo yalisemwa na meneja wa kiwanda hicho, Tushar Mehta, wakati Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, alipofanya ziara ya kukagua mashamba yaliyochomwa moto ya wawekezaji hao.
Alisema kitendo cha kuendelea kuhujumiwa mashamba yao ya miwa kinaweza kusababisha uongozi wa kiwanda hicho kuzuia ajira mpya 450 baada ya kukamilika kwa matengenezo makubwa na kuanza tena uzalishaji wa sukari.
Alisema watu wasiofahamika waliingia katika shamba hilo na kuwasha moto kwa mara ya pili baada ya tukio kama hilo Disemba 30, mwaka jana.
“Moto uliwashwa katikati ya shamba la miwa juzi, kabla ya waliofanya kitendo hicho kuwasha moto huo waliweka kizuizi kwa makusudi ili vikosi vya uokozi vishindwe kuuzima haraka,” alisema.
Mehta alisema hadi sasa eka 200 zimeteketezwa kwa moto kwenye matukio yote mawili katika kipindi cha siku tano na kusababisha hasara ya dola za Marekani 1,176,234.28 sawa na Sh. bilioni 2.3.
Mehta alisema hadi sasa eka 200 zimeteketezwa kwa moto kwenye matukio yote mawili katika kipindi cha siku tano na kusababisha hasara ya dola za Marekani 1,176,234.28 sawa na Sh. bilioni 2.3.
Akizungumza baada ya kupatiwa taarifa hiyo, Balozi Seif alisema vitendo hivyo vya hujuma haviitakii mema Zanzibar katika harakati zake za kukuza uchumi na kufanikisha mpango wa kukuza uchumi na kupunguza umasikini kwa wananchi wake.
Alisema watu wanaofanya vitendo hivyo wanafanya dhambi kubwa na pia wanawavunja moyo wawekezaji walioamua kuwekeza miradi yao ya kiuchumi Zanzibar kwa lengo la kuisaidia serikali pamoja na wananachi kupata maendeleo.
Alisema fikra za baadhi ya watu kwamba hujuma hizo zitatoa fursa kwao kutumia maeneo ya mashamba hayo ya miwa kuendeleza kilimo na mifugo inafaa kuachwa mara moja kwa vile yataendelea kuwa katika mipango ya serikali ya kuhudumia sekta ya viwanda.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment