Jeshi la Polisi Mkoani Katavi linamshikilia mkazi wa mji wa Mpanda, kwa tuhuma za kumnyanyasa kwa kumnyima mahitaji muhimu mtoto wake ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa juzi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari, alisema polisi walipata taarifa hiyo kupitia kituo kimoja cha radio kilichopo mkoani humo wakati mtoto huyo akihojiwa.
Alisema baada ya polisi kusikia kipindi hicho, walifuatilia na kumpata mtoto huyo na kumhoji na kubaini kuwa mzazi wake amekuwa akimnyima mahitaji muhimu ya kimaisha kama mavazi, chakula, matibabu na mahitaji ya shule.
Kamanda Kadavashari alisema mtoto huyo tangu mama yake mzazi afariki dunia mwaka jana na baba yake kuoa mke mwingine, maisha yake yalibadilika na kuanza kuishi maisha ya manyanyaso na mateso, hali iliyomsababisha hata kushindwa kuendelea vizuri na masomo.Alisema katika kanisa ambalo mzazi huyo anasali pamoja na mtoto huyo, imekuwa ikitolewa michango kwa lengo la kumsaidia lakini mtoto huyo hamfikii na kwamba hivi karibuni baba yake alimfukuza nyumbani na kuanza kuishi kwa kutangatanga mitaani.
Kamanda huyo wa polisi mkoa wa Katavi, alisema baada ya baba wa mtoto huyo kusikia kipindi hicho cha radio, alikwenda polisi kutoa taarifa za kupotelewa na mtoto wake huyo na polisi kumshikilia na walipomuhoji walibaini amekuwa akimnyanyasa mtoto wake na tayari amefunguliwa mashtaka na atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment