Katika mwongozo huo, eneo linalozungumzia majukumu ya wazazi na walezi, linasema: “Wazazi na wananchi wengine pia wanatakiwa kuendelea kujitolea nguvukazi na mali ili kuleta ustawi na maendeleo ya shule zilizoko ndani ya jamii.”
Kutokana na kipengele hicho, ni wazi kwamba baadhi ya shule bado zitaendelea kuwatoza wazai michango ama kuchangia vitu vingine tofauti na ambavyo wazazi wengi waliamini kwamba kwa sasa hawatachangia chochote kwa elimu ya watoto wao.
Tayari kumekuwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wazazi wakisema watoto wao wamerudishwa nyumbani wakitakiwa kuchangia vitu mbalimbali ikiwa ni pamoja na chakula na fedha tasilim.Kwa mujibu wa mwongozo huo wa Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, wazazi wanatakiwa pia kununua sare za shule na michezo, vifaa vya kujifunzia yakiwamo madaftari na kalamu na chakula kwa wanafunzi wa kutwa pamoja na matibabu kwa watoto wao.
“Wanatakiwa pia kulipia nauli ya kwenda shule na kurudi kwa wanafunzi wa kutwa na wanafunzi wa bweni wakati wa likizo, kununua magodoro, shuka, vifaa vya usafi binafsi kwa wanafunzi wanaosoma shule za bweni na wanaoishi katika hosteli," unasema mwongozo huo.
Alipopigiwa simu kutoa ufafanuzi, Kamishna wa Elimu, Prof. Eustella Bhalalusesa, baada ya kuulizwa swali na mwandishi alikata simu na kusema yupo kwenye kikao.
Katika hatua nyingine, Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba, alisema mishahara midogo kwa walimu, mazingira mabovu ya kazi na ongezeko la wanafunzi lisiloendana na miundombinu, ni changamoto nyingine kwenye kutimiza lengo hilo la elimu bure.
“Serikali haijaangalia matatizo ya walimu kama mishahara midogo. Siku zote walimu wamekuwa wakilipwa mishahara midogo na ujue hata watoto ambao hawakutaka kuja shule watakuja,” alisema.
Alisema mishahara midogo ni kikwazo kwa kuwa walimu wanakata tamaa.
Taarifa zinaonyesha kuwa mwalimu mpya wa Daraja 3A wa shule ya msingi aliyeajiriwa Julai, mwaka jana, anaanza na mshahara wa Sh. 477,000 kwa mwezi ambao baada ya makato hupokea Sh. 360,000.
Makato hayo ni kodi yaani P.A.Y.E, CWT, NHIF, mifuko kama PSPF au LAPF.
Kuhusu ongezeko la wanafunzi lisiloendana na miundombinu pamoja na vifaa, Mukoba alisema:
“Mwalimu huyu ambaye ana mshahara mdogo, ameongezewa kazi kubwa ya kusahihisha madaftari mengi zaidi na wanafunzi ambao wengine hawana pa kukaa, kwa hiyo ufundishaji unakuwa mgumu.”
Aliongeza kuwa kwenye elimu bure, serikali pia haijaangalia suala la chakula shuleni kwani njaa inaweza kuwa kikwazo kikubwa cha kufanikisha elimu kutokana na kwamba mwanafunzi akiwa hajala, hawezi kuelewa kile anachofundishwa.
“Pia walimu hawapandishwi vyeo kwa wakati. Hili ni tatizo kwa kuwa majukumu yote ya kufanikisha elimu hii yanakabidhiwa kwa walimu waliokata tamaa kwa kutoshughulikiwa kwa matatizo yao hasa hili la kutopandishwa madaraja kwa wakati,” alisema.
Katika uchunguzi wake huo, Nipashe limebaini kuwa hivi sasa baadhi ya walimu ‘wamevurugwa’ kwa kujua kuwa maisha yao yatazidi kuwa magumu kwani kabla ya ujio wa Rais Dk.Magafuli, mara zote walikuwa wakibuni michango mbalimbali ikiwamo ya ‘speed test’ na masomo ya ziada kwa nia ya kujiongezea kipato cha kujikimu wao na familia zao kwa madai kuwa mishahara wanayopata hailingani na gharama za maisha.
Kadhalika, Nipashe limebaini kuwa hadi sasa tayari baadhi ya walimu wameanza kufikiria kujihusisha na shughuli nyingine za ujasiriamali ikiwamo kuendesha bodaboda baada ya serikali ya Rais Dk. Magufuli kuwaondolea mianya ya kupoza makali ya maisha kupitia michango mbalimbali.
Mbali na mchango wa ‘speed test’ kwa baadhi ya shule, Nipashe limebaini kuwa michango mingine maarufu iliyokuwa ikiwaisaidia walimu kwa namna mbalimbali ni pamoja na ya masomo ya ziada (tuition), michango ya uji, michango ya ulinzi, michango ya karatasi za kuchapia mitihani, michango ya ujenzi wa uzio, madawati, lebo za shule, chaki, maji na umeme.
Michango mingine maarufu ni ya michezo, michango ya fulana za shule na sare ambazo huuzwa kwa bei ya juu kulinganisha na bei ya soko na pia michango ya vifaa vya usafi kama kwanja, jembe na fagio.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment