Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Serikali iliyopita, Bernard Membe ameungana na waziri mwenzake wa zamani, Dk Makongoro Mahanga kukosoa sera ya kubana matumizi ya Rais John Magufuli ya kudhibiti safari za nje na kuteua baraza dogo la mawaziri.
Kama ilivyokuwa kwa Dk Mahanga, waziri huyo aliyedumu kwa miaka tisa kwenye Wizara ya Mambo ya Nje amesema kiuhalisia, Rais hajapunguza idadi ya wizara kama alivyosema bali amepunguza “idadi ya mifuko”, huku akisisitiza kuwa mkuu huyo wa nchi atalazimika kutoka nje “atake asitake”.
Membe amekuwa waziri wa pili wa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete kukosoa sera ya kubana matumizi ya Serikali ya Awamu ya Tano baada ya Dk Mahanga, ambaye sasa amehamia Chadema, kumkosoa akisema idadi ya wizara inapimwa kwa kuangalia makatibu wakuu na si wizara na hivyo ukubwa wa Baraza la Mawaziri bado uko palepale.
Katika mahojiano maalumu na Mwananchi mapema wiki hii, Membe alikuwa na maoni kama hayo na akaenda mbali zaidi kuzungumzia hata sera ya kudhibiti safari za nje na Rais kujizuia kusafiri, akisema “Tanzania haiwezi kuishi kama kisiwa” katika dunia ya leo.
Kubana matumizi
Membe, ambaye alikuwamo kwenye kinyang’airo cha urais na kufika hadi tano bora, alisema Rais hajabana matumizi yoyote kwa kupunguza ukubwa wa Baraza la Mawaziri, bali alichofanya ni kupunguza idadi ya mawaziri na siyo wizara.
“Alichofanya ni sawa na kuwa na mayai kumi halafu ukaamua kuyaweka kwenye mifuko kumi, maana yake ni kwamba utakuwa na mifuko kumi yenye mayai,” alisema Membe.
“Lakini unaweza kuwa na idadi hiyo hiyo ya mayai na ukaamua kuyagawanya; mayai matatu unayaweka kwenye mfuko mmoja, mawili kwenye mfuko mwingine na yaliyobaki kwenye mfuko mmoja. Maana yake ni kwamba utaendelea kuwa na mayai kumi lakini idadi ya mifuko imepungua. Hapa sasa utakuwa hujapunguza gharama za kuyatunza hayo mayai.”
Rais aliahidi kwenye kampeni na hotuba yake ya uzinduzi wa Bunge kuwa atapunguza ukubwa wa Baraza la Mawaziri ili kubana matumizi. Alitekeleza ahadi yake kwa kuunda baraza lenye mawaziri 34 tofauti na lililopita ambalo lilikuwa na mawaziri 55.
Rais aliahidi kwenye kampeni na hotuba yake ya uzinduzi wa Bunge kuwa atapunguza ukubwa wa Baraza la Mawaziri ili kubana matumizi. Alitekeleza ahadi yake kwa kuunda baraza lenye mawaziri 34 tofauti na lililopita ambalo lilikuwa na mawaziri 55.
Upunguzaji huo wa baraza ulifanywa kwa kuunganisha wizara na hivyo kufanya makatibu wakuu, ambao ni maofisa masuhuli wa wizara kuwa zaidi ya mmoja kwenye baadhi ya wizara.
“Ameendeleza wizara zilezile, lakini akaamua kuzikusanya pamoja. Hiyo haimaanishi kuwa atakuwa amepunguza gharama za uendeshaji wake,” alisema Membe.
“Hilo tutaliona kwenye Bajeti ya Serikali ya mwaka huu. Tuone kama bajeti itaongezeka au itapungua? Kwa sababu kama wizara zimepungua kama tunavyoamini, lazima bajeti ipungue, sasa bajeti ikiongezeka au ikibaki vilevile maana yake hakuna kilichofanyika.”
Membe alitoa mfano wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambayo sasa inaitwa “Wizara ya Mambo ya Nje, Kikanda na Ushirikiano wa Afrika Mashariki”, akisema itapaswa kuwa na bajeti mbili; ya Mambo ya Nje na Bajeti ya Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki kinyume chake ni vigumu kuiendesha.
Membe alikiri kuwa hata yeye angeingia kwenye mtego wa kupunguza idadi ya wizara kama angefanikiwa kuchaguliwa kuwa Rais kama ilivyokuwa nchini Namibia ambako wizara zilipunguzwa kutoka 32 hadi 20.
“Baadaye nikagundua kuwa hata Namibia yenyewe inajuta,” alisema.
Alisema siku ya kuapishwa Rais Magufuli, alikutana na Makamu wa Rais wa Namibia, Nickey Lyambo na baada ya kusalimiana na kumpongeza kwa hatua ya kupunguza wizara, kiongozi huyo wa Taifa hilo la kusini mwa Afrika alimweleza kuwa uamuzi huo umewasababishia matatizo makubwa bungeni
“Aliniambia katika Bunge la Namibia kuna mjadala mkali wa kutaka wizara ziongezwe,” alisema Membe akimnukuu makamu huyo wa rais wa Namibia.
Membe alibainisha kuwa kwa Tanzania, mfumo huo mpya wa wizara pia unaweza kuathiri uwasilishaji wa bajeti bungeni kwa kuwa mawaziri sasa watahitaji muda mwingi zaidi kuliko ilivyokuwa awali ili kuzungumzia wizara kadhaa zilizounganishwa, jambo ambalo lililalamikiwa pia na kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni, Tundu Lissu. “Kila kitu kina form na content (muundo na maudhui). Alichofanya Rais Magufuli ni kubadili form na siyo content ya wizara, wizara ni zilezile na mzigo ni uleule,” alisema.
Safari za nje
Mbunge huyo wa zamani wa Mtama mkoani Lindi, pia alikosoa udhibiti wa safari za nje, akisema Tanzania si kisiwa.
Alikuwa akijibu swali lililomtaka aeleze uhalisia wa mpango wa Rais Magufuli kubana matumizi kwa kufuta safari za nje za mawaziri na watumishi wengine wa umma.
Mara tu baada ya kuingia madarakani, Rais Magufuli alifuta safari zote za nje ya nchi kwa watendaji na watumishi wa umma, isipokuwa zile tu ambazo zingepata kibali cha Ikulu, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kubana matumizi ya Serikali.
Rais Magufuli alisema katika hotuba yake ya kuzindua Bunge kuwa kuanzia mwaka 2013 hadi 2015, safari hizo ziliigharimu Serikali Sh356.3 bilioni na kwamba kati ya fedha hizo, Sh183.1 bilioni zilitumika kwa ajili ya tiketi za ndege, Sh68.6 bilioni kwa ajili ya mafunzo na Sh104.5 bilioni kwa ajili ya posho.
Bila kugusia madhara ya kufuta safari hizo, Rais Magufuli alijielekeza zaidi kwenye matumizi ya fedha ambazo angeokoa.
“Lakini tujiulize fedha hizo zingeweza kutengeneza zahanati ngapi? Zingeweza kutengeneza nyumba za walimu ngapi? Zingeweza kutengeneza madawati mangapi? Zingeweza kununua dawa hospitalini tani ngapi?” alihoji Rais Magufuli katika hotuba yake iliyotoa mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Lakini Membe, ambaye wizara yake iliwahi kutetea safari za Jakaya Kikwete nje ya nchi baada ya wapinzani kusema ziligharimu zaidi ya Sh4 trilioni, alisema safari za nje zina umuhimu kwa taifa lolote.
“Tanzania si kisiwa, hata ukiwa tajiri namna gani lazima utoke nje ya nchi yako,” alisema Membe ambaye ana shahada ya umahiri ya uhusiano wa kimataifa aliyoipata Marekani.
“Lazima utakwenda mwenyewe au mawaziri wako na hasa Waziri wa Mambo ya Nje kwa sababu kuna vikao nje ya nchi ambavyo mabalozi hawaruhusiwi kuingia.
“Ukijaribu kujifanya kisiwa utakuwa kama Zimbabwe. If you isolate yourself you will be isolated (ukijitenga, utatengwa).”
Membe alisema nchi ina mabalozi 36 tu duniani kote kati ya nchi 194 zinazohitaji uwakilishi huo na kibaya zaidi, mabalozi hawaruhusiwi kuingia kwenye baadhi ya vikao, na hata wakiingia wakifika kwenye hatua ya uamuzi watazuiwa kushiriki.
“Kwa mfano, Uturuki hatuna ubalozi, sasa unapoona ndege inaleta watalii kutoka Uturuki, unadhani Bunge la Uturuki liliketi kutuletea watalii Tanzania? Hapana. Tulitoka nje na kuwashawishi wakaja,” alisema Membe aliyewahi kueleza kuwa wakati wa awamu ya Rais Jakaya Kikwete mawaziri walikuwa wanapishana angani kana kwamba kuna moto ardhini.
“Pia, leo unaposikia gesi, gesi, gesi nayo imepatikana nje ya ubalozi. Mawaziri walitoka nje ya nchi wakatafuta wawekezaji. Ni kazi ya wizara kufanya yote hayo.”
Membe alirudia kauli aliyoitoa siku chache kabla ya kuanza mchakato wa Uchaguzi Mkuu mwaka jana kuwa lazima waziri wa mambo ya nje awe nje ya nchi kwa muda mwingi na ikitokea yuko ndani ya nchi kwa mwezi mmoja mfululizo, lazima ni mgonjwa.
No comments :
Post a Comment