Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Monday, January 4, 2016

Membe, Sitta, Wasira, basi tena kwa Magufuli *Wafungiwa vioo bungeni, wizarani *Wamo Mwandosya, Migiro, Mukangara, Sophia Simba aponea cheo chake UWT

Rais John Magufuli
HATIMAYE Rais John Magufuli ametimiza kazi iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu ya kupanga safu yake ya Baraza la Mawaziri na pia makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu wa kila wizara.
 
Katika safu yake hiyo iliyokamilika mwishoni mwa wiki baada ya kuwaapisha makatibu wakuu na manaibu katibu wakuu Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli aliendelea kutoa nafasi zaidi kwa sura mpya huku akiachana na majina kadhaa maarufu ya watu waliowahi kuongoza wizara katika serikali ya awamu ya nne ya Rais Kikwete, wakiwamo Bernard Membe aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Usbirikiano wa Kimataifa, Samuel Sitta wa Wizara ya Uchukuzi, Stephen Wasira wa Kilimo, Chakula na Ushirika na pia Prof. Mark Mwandosya. Baadhi ya vigogo hao wa serikali iliyopita, akiwamo Sitta ambaye pia aliwania Uspika bila mafanikio, wamekaririwa wakisema kuwa sasa wamestaafu rasmi siasa.
 
Membe, Sitta, Wasira na Dk. Asha-Rose Migiro aliyekuwa Waziri wa Sheria na Mambo ya Katiba, ni miongoni mwa makada 38 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliojitosa katika mchakato wa kuwania kuteuliwa kuwa wagombea urais wa chama chao (CCM) ambao mwishowe Magufuli ndiye aliyeibuka mshindi.Uchunguzi uliofanywa na Nipashe kupitia orodha ya wateule wa Rais Magufuli kwa nafasi za ubunge, uwaziri, naibu mawaziri, makatibu wakuu na manaibu katibu wakuu umebaini kuwa vigogo hao na wenzao wengine kadhaa waliowahi kushika uwaziri au kuwa wabunge katika serikali ya awamu ya nne wamejikuta nje ya wizara na bunge baada ya kutoguswa na uteuzi wa Rais Magufuli.
 
Mbali na Membe, Sitta, Wasira na Migiro, wengine miongoni mwa wale ambao sasa kuna uwezekano mkubwa majina yao yakabaki kuwa historia katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni aliyekuwa Waziri wa Fedha na Uchumi, Saada Mkuya Salum; aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Dk. Fenella Mukangara na aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Prof. Mark Mwandosya.
 
Aidha, katika orodha ya watu waliowahi kuongoza wizara kwenye serikali ya awamu ya nne lakini sasa hawajateuliwa na Magufuli na wala kukumbukwa katika nafasi 10 za ubunge zinazotokana na uteuzi wa Rais ni aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Prof. Mark Mwandosya; aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Adam Malima; aliyekuwa Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Godfrey Zambi; aliyekuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Anne Kilango Malecela na aliyekuwa Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla.
 
Rais Magufuli pia hajampa nafasi yoyote kwenye safu yake ya uongozi wa wizara aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wanawake, Jinsia na Watoto, Sophia Simba. Hata hivyo, tofauti na kina Migiro, Sitta, Wasira, Membe na Mwandosya ambao siyo tu wameukosa uwaziri bali pia ubunge na hivyo kutokuwa na uwezekano wowote wa kuonekana tena ‘mjengoni’ mjini Dodoma, Simba anaendelea kuwa mmojawapo wa wabunge wa viti maalum ndani ya CCM kutokana na nafasi yake ya kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM nchini (UWT).
 
“(Sophia) Simba amevushwa  na cheo chake cha kuwa mwenyekiti wa taifa wa UWT… kwa kawaida mwenye nafasi hiyo CCM (mwenyekiti wa UWT) huwa tayari amejihakikishia kuwa mmojawapo wa wabunge wa viti maalum, vinginevyo naye angekuwa na nafasi ndogo ya kuwapo bungeni katika utawala huu wa Serikali ya Rais Magufuli,” chanzo kimoja kiliiambia Nipashe mwishoni mwa wiki.
 
KILICHOWAONDOA BUNGENI 
Katika uchunguzi wake, Nipashe imebaini kuwa baadhi ya mawaziri na manaibu waziri walijitosa katika mchakato wa kuwania ubunge ndani ya CCM lakini wakakosa kura za kutosha ili kuwa wateule wa chama chao katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 na hivyo kujikuta wakiwa nje ya Bunge na pia nje ya Baraza la Mawaziri katika Serikali ya awamu ya tano. 
 
Hawa ni pamoja na Dk. Pindi Chana aliyekuwa Naibu Waziri wa Wanawake, Jinsia na Watoto; Kaika Telele aliyekuwa Naibu Waziri wa Uvuvi na Maendeleo ya Mifugo, Dk.  Binilith Mahenge (Mazingira), Adam Malima aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha, Dk. Titus Kamani aliyekuwa wa Wizara ya Uvuvi na Maendeleo ya Mifugo, Dk. Seif Rashid (Wizara ya Afya) na Makala aliyekuwa Naibu Waziri wa Maji.
 
Vigogo wengine ni Pereira Ame Silima (Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani), Mathias Chikawe (Waziri wa Mambo ya Ndani), Mahadhi Juma Maalim (Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa), Christopher Chiza (Uwekezaji na Uwezeshaji) na Gaudencia Kabaka (Kazi na Ajira) na Dk. Abdulla Juma Abdulla aliyekuwa Naibu Waziri wa Afrika Mashariki.
 
Aidha, wapo mawaziri ambao walipitishwa na CCM kugombea ubunge lakini wakaangushwa katika uchaguzi mkuu. Hao ni pamoja na Aggrey Mwanry aliyekuwa Naibu Waziri Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk. Stephen Kebwe aliyekuwa Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii; aliyekuwa Naibu Waziri wa Elimu, Anne Kilango Malecela; aliyekuwa Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji), Christopher Chizza;   aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Dk. Mukangara; aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Wasira na aliyekuwa naibu waziri wake, Godfrey Zambi.
 
Kadhalika, wapo vigogo ambao hawakugombea  ubunge na badala yake kuwekeza nguvu zao katika kuwania nafasi ya urais kupitia CCM bila mafanikio. Hao ni pamoja na Sitta, Prof. Mwandosya, Membe na Dk. Makongoro Mahanga aliyeihama CCM na kutua Chadema. 
 
Kadhalika, wapo pia waliowahi kuteuliwa kuwa wabunge na Kikwete kabla ya kupewa uwaziri au unaibu waziri lakini hawakugombea ubunge na sasa kuwa nje ya Serikali ya awamu ya tano, baadhi yao wakiwa ni Dk. Migiro na Saada Mkuya Salum. Waliokuwa mawaziri, Dk. Abdallah Kigoda wa Wizara ya Viwanda na Biashara na Celina Kombani aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma) walifariki dunia kabla ya uchaguzi mkuu Oktoba 25, 2015.
 
SABABU ZAIDI KUKOSEKANA VIGOGO WA AWAMU YA NNE
Uchunguzi uliofanywa na Nipashe kupitia mahojiano na wachambuzi mbalimbali wa masuala ya siasa nchini umebaini kuwa zipo sababu nyingi zilizowapoteza baadhi ya wanasiasa wenye majina makubwa katika orodha ya viongozi wa wizara au wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
 
Inaelezwa kuwa athari za makundi ndani ya CCM wakati wa mchakato wa kumsaka mgombea urais;  dhamira ya Rais Magufuli kuleta mabadilio ya kweli kuanzia katika safu ya juu ya uongozi; kupoteza mvuto kisiasa kwa baadhi ya watu waliokuwa wakishikilia nafasi za juu na pia ‘madudu’ yanayoibuka sasa katika wizara mbalimbali ni miongoni mwa sababu tele zilizowaweka nje ya mifumo ya utawala baadhi ya wale waliokuwa wateule wa Rais Kikwete.
 
Mmoja wa wachambuzi aliiambia Nipashe kuwa tukio kama lililojitokeza ndani ya kamati kuu ya CCM (CC) wakati aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, Simba na Adam Kimbisa walipojitokeza hadharani kupinga kuondolewa kwa Edward Lowassa kwenye orodha ya wateule watano wa mwisho kuwania urais ndani ya chama hicho (CCM) linaweza kuwa doa mojawapo la makundi lilichangia baadhi ya watu ‘kufungiwa vioo’ katika serikali ya awamu ya tano. Hata hivyo, inafahamika kuwa baadaye Lowassa alijiondoa CCM na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambako mwishowe aligombea urais kwa mwavuli wa muungano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya Chadema, Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na NLD. Wote watatu -- Nchimbi, Simba na Kimbisa -- waliachana na Lowassa aliyehamia Chadema na kutangaza wazi kuwa wanamuunga mkono mgombea wa chama chao (Magufuli).  
 
“Ni kweli kwamba baada ya jina la Magufuli kupitishwa, Nchimbi, Simba na Kimbisa walisahau yaliyopita na kuungana na wenzao kumpigia debe mgombea huyo wa chama chao (Magufuli)…hata hivyo, sidhani kama hilo peke yake linatosha. Hii inawezekana kabisa kuwa miongoni mwa sababu za kutokumbukwa kwa watu wa aina hiyo kwenye serikali ya awamu ya tano,” alisema mmoja wa wachambuzi wa siasa.
 
Aidha, inaelezwa zaidi kuwa baadhi ya mawaziri waliokuwa na majina makubwa katika serikali ya awamu ya nne wamepoteza nguvu waliyokuwa nayo awali kisiasa na kwamba hilo limechangia pia kuachwa kwao kwani mchakato wa uchaguzi umedhihirisha kuwa hawana nguvu waliyokuwa nayo miaka kadhaa iliyopita.
 
“Kuna watu wameshindwa kutetea majimbo yao na sasa yameangukia upinzani. Wengine walishaachana na ubunge na kujielekeza zaidi katika kuwania urais, wapo wengine hawana ubunge na wizara walizokuwa wakiziongoza zimekutwa na madudu mengi yaliyofanyika enzi zao. Katika hali kama hiyo, ni wazi kwamba wengi wao walikuwa na nafasi ndogo ya kuteuliwa na Rais Magufuli,” mmoja wa wachambuzi aliiambia Nipashe.
 
Kadhalika, hoja ya kuleta mabadiliko kiutendaji na kuondokana na kauli zilizozoeleka kutoka kwa baadhi ya mawaziri na manaibu waziri wa serikali ya awamu ya nne kama ‘tuko mbioni’, ‘tuko kwenye mchakato’ na ‘tuko kwenye hatua nzuri’ ni moja ya sababu iliyotajwa na mchambuzi mwingine kwamba imechangia kuachwa nje ya mfumo kwa baadhi ya majina ya vigogo.
  
“Kuna hili la Rais Magufuli kutimiza ahadi yake ya kuleta mabadiliko ya kweli kupitia CCM na kwamba, hataki tena kusikia blaablaa za maneno kama tuko mbioni… ni wazi kwamba ili kufanikisha dhamira hiyo, ni lazima mabadiliko yaanzie kwenye safu za juu za uongozi, hasa kwa kuwapa nafasi watu wapya ili washirikiane na wazoefu kutimiza ndoto ya kuwaletea Watanzania maisha bora,” alisema mchambuzi huyo, huku akiongeza kuwa ufisadi unaweza kushughulikiwa vizuri kwa kuweka watu wapya watakaopambana kwa dhati dhidi ya vitendo kama vilivyoibuliwa hivi karibuni vya ukwepaji kodi wa makontena yanayopitishwa kwenye Bandari ya Dar es Salaam.
 
Hadi sasa, Rais Magufuli ameshatumia nafasi zake kadhaa kati ya 10 za kuteua wabunge, baadhi zikitua kwa Dk. Tulia Ackson ambaye ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Augustine Mahiga ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa; Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu), Dk. Abdallah Possi; Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa; Waziri wa Elimu, Teknolojia na Ufundi, Dk. Joyce Ndalichako; Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Phillip Mpango na naibu wake, Dk. Ashatu Kijaji.  
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment