Mkuu wa Mawasiliano wa Wizara ya Nishati na Madini, Badra Masoud.
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imeingia makubaliano na Japan ya kuipatia mkopo wa masharti nafuu wa Dola 240 milioni za Marekani (sawa na Sh504 bilioni) kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa umeme wa Kinyerezi II wenye uwezo wa kuzalisha megawati 240 za umeme.
Hayo yalisemwa juzi na Mkuu wa Mawasiliano wa Wizara ya Nishati na Madini, Badra Masoud alipozungumza na waandishi wa habari kutoa ufafanuzi wa utekelezaji wa mradi huo.
“Serikali inajiandaa kuweka jiwe la msingi kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi huo ambao utajengwa na kampuni ya Sumimoto ya Japan kama mkandarasi na sio mbia kama ilivyoripotiwa hapo awali,” alisema.
Aliongeza kuwa mradi huo unamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100 kupitia Shirika la Umeme nchini (Tanesco) na hakuna mwekezaji mwingine yeyote.
Kuhusu gharama za mradi, Masoud alisema utekelezaji wake utagharimu Dola 344 milioni za Marekani (sawa na Sh740 bilioni) zikiwa ni mkopo wa masharti nafuu na mchango wa Serikali utakuwa Dola 52 za Marekani (sawa na Sh109 bilioni).
Ufafanuzi huo umekuja baada ya wizara hiyo kudai kuna taarifa za upotoshaji zilizochapishwa kwenye vyombo vya habari zilizoeleza kuwa Serikali imeingia ubia na Kampuni ya Sumimoto ambao unaifanya kuwa na hisa asilimia 40 na zilizobaki zitakuwa za kampuni hiyo.
No comments :
Post a Comment