Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage.
HISTORIA NA ELIMU
Charles John Mwijage ni Waziri wa Viwanda,Biashara na Uwekezaji katika Serikali ya Awamu ya Tano, ameteuliwa katika baraza la mwanzo la Rais John Pombe Magufuli. Yeye ni mbunge wa kuchaguliwa kutoka jimbo la Muleba Kaskazini, Kagera - tangu mwaka 2010.
Kitaaluma ni mtaalamu mshauri katika Biashara ya Petroli, Masoko na Usimamizi wa Miradi. Hivi sasa Mwijage ana umri wa miaka 55 na ifikapo Septemba mwaka huu 2016 atatimiza miaka 56 kwani alizaliwa Septemba 4, 1960. Alizaliwa wilaya ya Bukoba mkoani Kagera.
Baba mzazi wa Mwijage ni John Paul (marehemu hivi sasa), yeye alikuwa ni fundi mwashi katika uhai wake na mwenyeji wa wilaya ya Muleba mkoani Kagera. Mama mzazi wa Mwijage ni Mariamu Kagole (marehemu pia), yeye alikuwa ni mama wa nyumbani na alifariki wakati mwanawe (Mwijage) akiwa na umri wa miaka mitatu kwa hivyo Mwijage alilelewa na bibi yake aitwaye Mwamini Mukoomwami (Bibi wa Kibuyu).
Mwijage alipata elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari Nyakato iliyoko mkoani Kagera. Alianza kidato cha kwanza mwaka 1977 na kuhitimu cha nne mwaka 1980. Akachaguliwa kuendelea na elimu ya juu ya sekondari katika Shule ya Sekondari Tosamaganga iliyoko mkoani Iringa mchepuo wake ukiwa ni (PCM – Fizikia, Kemia na Hisabati), alianza kidato cha tano mwaka 1981 na kuhitimu cha sita mwaka 1983.
Mwaka 1985 alisoma kwa miezi saba na kuhitimu kozi ya Usafishaji wa Petroli na Oparesheni za Mabomba (Petroleum Refining and Pipeline Operations) iliyosimamiwa na kampuni ya TIPER Refinary ya jijini Dar es Salaam, akatunukiwa cheti.
Mwijage alipata elimu ya juu katika Taasisi ya Maendeleo Mzumbe -Morogoro akasoma na kuhitimu stashahada ya juu ya Usimamizi wa Biashara (ADBA) kuanzia mwaka 1989 na kuhitimua mwaka 1991 (kwa viwango vya sasa stashahada hiyo ni sawa na shahada ya chuo kikuu).
Mwaka 1994 alitunukiwa cheti kingine baada ya kusoma na kuhitimu kozi ya Usalama Viwandani, Uzuiaji wa Moto na Upambanaji wa Moto kutoka Chuo cha Wahandisi wa Kupambana na Moto cha Sargom nchini Zimbabwe.
Mwaka 1994 Mwijage alijiunga Chuo Kikuu cha Salford nchini Uingereza ili kusoma Shahada ya Uzamili (umahiri) ya Usimamizi wa Biashara (MBA) ambayo aliihitimu na kutunukiwa mwaka 1996.
Mwaka 2006 alitunukiwa cheti baada ya kusoma na kuhitimu kozi ya Biashara na Upangaji Bei wa Mafuta ngazi ya Kimataifa kutoka taasisi ya Chevron nchini Uingereza na mwaka huo huo akasoma na kutunukiwa cheti kingine baada ya kuhitimu kozi ya Uratibu na Usambazaji wa Bidhaa za Kikanda iliyotolewa na taasisi hiyo hiyo ya Chevron lakini mara hiyo ikifanyikia katika jiji la Lusaka, Zambia. Mwijage ameoa na ana watoto wanne.
UZOEFU
Mwijage alianza kazi Juni 1984 katika Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kama Msimamizi wa Pampu, kazi kubwa alizokuwa anafanya katika jukumu hilo ni kupima na kuhakiki mafuta jamii ya petroli (uzito wa mafuta na ujazo wake) katika meli, mabomba, matanki ya kuhifadhia mafuta, magari na vituo vya kuhifadhia mafuta. Aliifanya kazi hii hadi mwezi June 1989.
Juni 1991 hadi Juni 1993 amefanya kazi hapo hapo TPDC kama Ofisa Masoko. Novemba 1993 hadi Februari 1994 akawa Ofisa Takwimu.
Novemba 1994 hadi Aprili 1998 alihamishiwa kitengo cha Usalama na Mazingira na kufanya kazi kama Ofisa Mdhibiti wa Usalama na Mazingira. Aprili 1998 akahamia kwenye kampuni ya gesi (Gas Company T – LTD) na kuajiriwa kama Ofisa Masoko, akadumu hapo hadi Machi 1999.
Machi 1999 akapandishwa cheo katika kampuni hiyo ya gesi na kuwa Meneja Masoko na kudumu hapo hadi Juni 2000. Juni 2000 akarudi tena katika Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na kuajiriwa kama Ofisa Mdhibiti Mwandamizi wa Usalama na Mazingira na kukaa hapo hadi Machi 2002.
Machi 2002 hadi mwaka 2005 Mwijage alihamia kwenye kampuni ya CYCLONE na kufanya kazi kama Msimamizi Mkuu wa Masoko (Marketing Executive) na mwaka 2005 hadi 2009 akahamia kampuni ya CHEVRON na kuajiriwa kama Msimamizi wa Biashara wa Afrika Mashariki.
Mwaka 2010 Mwijage alijitosa rasmi kwenye siasa kupitia CCM, akashiriki kura za maoni akiliwinda jimbo la Muleba Kusini na kushinda. Kwenye uchaguzi wa jumla alipambana na mgombea kutoka CHADEMA, Musedemu Millanga. Mwijage alipata ushindi wa kura 30,886 sawa na asilimia 79.74 akimuacha Musedemu wa CHADEMA na kura 6,845 sawa na asilimia 17.67.
Januari 2014, Mwijage aliteuliwa na Rais Kikwete kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini baada ya aliyekuwa naibu wa wizara hiyo George Simbachawene kupandishwa na kuwa waziri kutokana na wadhifa huo kuwa wazi baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini wakati huo (Profesa Sospeter Muhongo), baada ya shinikizo la Bunge juu ya kashfa ya Escrow.
Agosti 2015, Mwijage alitupa tena karata yake Muleba Kaskazini akisaka kipindi cha pili cha ubunge. Kwenye kura ya maoni ndani ya CCM Mwijage alipata kura 20,706 na kumshinda kada mwenzake Ambrose Nshala aliyepata kura 3,523.
Kwenye uchaguzi wa jumla wa Oktoba 2015, Mwijage alipata kura 41,192 na kumshinda mpinzani wake wa karibu kutoka CHADEMA, mwanahabari Ansbert Ngurumo ambaye alipigiwa kura 19,396. Baada ya ushindi huu wa ubunge wa mara ya pili kwa Mwijage ndipo rais JPM alipomteua rasmi na kumkabidhi Wizara ya Viwanda na Biashara.
NGUVU
Jambo la kwanza muhimu kwa Mwijage ni kule kuifahamu vizuri sekta ya biashara ndani ya nchi, amekuwa kwenye sekta hiyo kwa miaka 26 kama mdau muhimu na mtu ambaye anajua vizuri utaratibu wa masoko (ambako biashara zinafanyikia). Kumpa Wizara ya Viwanda na Biashara kunamfanya awe na kazi ngumu kwenye upande wa usimamizi na uanzishwaji wa viwanda lakini akitumia vizuri maarifa yake ya masoko na biashara anaweza kuhuisha viwanda kwani maeneo hayo mawili yanafanana na la kwanza ni la uzalishaji ambalo anaweza kujifunza haraka na bahati aliyonayo hili la pili (biashara) ameliishi kwa miongo karibia mitatu.
Jambo la pili muhimu kwa Mwijage ni uzoefu wake wa ubunge wa miaka mitano lakini kubwa kuliko yote uzoefu wa masuala ya uchunguzi, takwimu na kazi zinazohitaji umakini. Mathalani, Mwaka 1996 alikuwa mwenyekiti wa timu ya Serikali iliyochunguza ajali ya moto uliotokea Disemba 25, 1996 ulioteketeza SBM (SBM ni Mtambo ulioko kwenye maji marefu “bahari kuu” ambako meli za mafuta zenye ujazo wa tani laki moja hufunga ili kushusha mafuta). Mtambo huo ni kwa ajili ya kusaidia meli zenye ujazo mkubwa zipate kina kirefu na kutia nanga hapo. Mwaka 1998 aliteuliwa kuwa mjumbe wa sekretariati ya Serikali iliyohakiki usalama wa uwekaji wa mabomba ya petroli na mafuta nchini Tanzania.
Ndani ya Bunge sote tunafahamu kuwa amefanya kazi na kamati kadhaa za kiuchunguzi ambazo zilileta matokeo yaliyoitikisa Serikali. Kuwa na bahati ya kushiriki kwenye uchunguzi tofauti tofauti kutamsaidia kwenye eneo la kuongeza udadisi wa kufuatilia sekta mtambuka kama biashara na viwanda kwani ni maeneo yanayohitaji ufuatiliaji, udadisi, weledi wa mambo ya kisasa na kujua namna ya kupata taarifa nyeti za kibiashara.
Jambo la pili litakalomsaidia sana Mwijage ni msimamo. Rekodi zake katika Bunge lililopita nyakati ambazo alikuwa siyo waziri alikuwa miongoni mwa wabunge wachache wa CCM ambao mara kadhaa aliikimbia misimamo ya chama chao na kusimamia hoja za kitaifa. Hiyo ilisababishwa na misimamo yake binafsi ambayo pia anaweza kuendelea kuitumia katika wadhifa wa sasa kwani kuna masuala mengi yatakayohitaji msimamo wake binafsi hasa kwenye eneo la viwanda na biashara.
UDHAIFU
Mwijage siyo mtu anayekaa mahali akapatikisa pakatikisika. Alipoteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini katika miaka miwili ya mwisho wa uongozi wa Kikwete, hakusikika sana. Aliyekuwa waziri wake hakusikika na yeye Mwijage (Naibu) hakugundua mapungufu ya mkubwa wake ili afanye kazi kwa juhudi na zionekane. Ndiyo maana Wizara ya Nishati na Madini chini ya Simbachawene na Mwijage ilionekana kama wizara ambayo haina mwelekeo mzuri.
Katika wizara aliyopo sasa ya Viwanda na Biashara changamoto ni nyingi na yeye Mwijage ndiye bosi. Kuanzia sasa kipima mwendo kimeshawekwa kwenye ofisi yake ili kuona kama atafikia malengo ambayo Serikali yake imejiwekea.
Inawezekana hali ya kushindwa kuacha “alama” akaendelea nayo hata katika wizara aliyopo sasa, na hilo lilitokea litathibitisha nini nimekisema hapo juu kuhusu unaibu waziri wake kwenye uongozi wa JK.
MATARAJIO
Mwijage anatarajia kuwatumia sana wadau wa ndani na nje ya nchi kusimamia viwanda na biashara hapa Tanzania. Anaamini Watanzania walio wengi wanahitaji kuona mabadiliko kwenye sekta anazosimamia na anasema atatumia kila uwezo alionao na uzoefu wake katika sekta hizi za kisasa ili kutimiza ahadi na mipango ya rais wake.
Wadau wa sekta zote mbili wanahitaji wizara hii ifanye juu chini kuwakutanisha na wakuu wa Wizara ya Fedha kwani wanaona kwa pamoja wizara mbili zinapaswa kuweka masuala mengi sawa kabla hawajaanza kuchukua kasi ya kutekeleza azimio la Serikali la kuhuisha viwanda. Wengi wanasema ni muhimu kukaa na watu wa fedha kwa sababu kuna vikwazo vingi sana wanavyopata kutokana na masuala ya ulipaji kodi na ukiritimba uliopitiliza kutoka taasisi zilizo chini ya Wizara ya Fedha.
CHANGAMOTO
Changamoto ya kwanza kwa Mwijage ni asili ya wizara aliyopewa na matarajio ya mkubwa wake wa kazi. JPM alinadi sana sera zake akiweka msisitizo kwenye ujenzi wa viwanda, uhuishaji wa viwanda na ukaribishaji wa wawekezaji wenye fedha nyingi, wa ndani na nje ya nchi. Hii ni ahadi kubwa ambayo Rais JPM ameitangaza na hata alipozindua Bunge akaisisitiza sana. JPM atakuwa na aibu kubwa ikiwa atafikiri kuwa anaweza kurudi kwenye kampeni za 2020 huku nchi ikiwa haina viwanda alivyoahidi, atakosa jambo la kuwaeleza wananchi.
Ukweli unabakia kuwa nchi yetu haina viwanda na haina cha kujivunia katika eneo hilo. Viwanda vyote vilivyowahi kuwapo vikivuma na kuzalisha bidhaa mbali mbali vilishajifia na kufilisiwa, vilijaza matumbo ya wakubwa na kutoweka.
Leo Tanzania inanunua kila bidhaa yake kutoka nje, hata vijiti vya kuchokonoa meno vinaletwa kutoka China. Wakulima wa matunda, mboga mboga na mazao mengine ya biashara yanayoweza kutengenezewa katika viwanda vidogo na vikubwa wanataabika na bidhaa na malighafi zao na wanaziuza kwa bei za kutupa kwa sababu ya kukosekana kwa mfumo wa kuhuisha bidhaa na malighafi.
Mwijage na naibu wake na watendaji wao wanalo jukumu la kuhakikisha kunakuwa na mipango thabiti na inayotekelezeka ambayo itafanya walau nchi yetu ianze kujenga viwanda vikubwa kadhaa katika wilaya na mikoa. Kwamba baada ya miaka mitano wakisimama waseme tuna kiwanda wilaya hii, tuna kiwanda wilaya ile. Lakini pia wanapaswa kubuni na kuja na mfumo unaoeleweka ambao utawasaidia wajasiriamali wadogo kuanzisha viwanda vidogo vidogo kila mahali, nchi ijigeuze kuwa ni ya uzalishaji kila kona, wajasiriamali hawa wanahitaji mitaji, elimu ya uwekezaji watakaoufanya na mengine mengi. Mwijage anapaswa kupasua kichwa na kuja na majibu ya namna gani haya yote yatashughulikwa na kuleta ufanisi.
Sekta ya biashara kwa Tanzania ni kama vile imekufa. Hatuna uwekezaji mkubwa kwenye eneo hilo na watu wengi wanaohitaji kufanya biashara ndani ya nchi au nje ya nchi, wanaotokea hapa Tanzania au ughaibuni wanapata shida kubwa kutokana na mifumo yetu iliyofeli. Mtu akitaka kusajili kampuni kubwa hapa Tanzania atazungushwa sana, nchi zingine kampuni inasajiliwa kwa dakika kadhaa na kuanza kazi ilimradi imetimiza masharti.
Kumekuwa na ukiritimba mkubwa kwenye masuala ya ulipaji wa kodi kwa sababu ya milolongo na kodi zisizo na kichwa wala miguu. Matokeo yake wafanyabiashara wanakata tamaa na kuacha kuwekeza kibiashara hapa kwetu.
Mwijage anapaswa apiganie kubadilisha hali hii, sasa tuanze kuona wafanyabiashara wakubwa na wadogo wakiinuliwa na kupewa mbinu, miundombinu na miteremko ya kisera ili wapanue biashara zao na kulipatia Taifa manufaa.
Ikumbukwe kuwa mkakati wa kukuza viwanda na biashara ndiyo siri ya kipekee ya kutatua tatizo la ajira nchini. Vijana wengi wa Tanzania hawana ajira kwa sababu hawana mahali pa kufanya kazi, nchi isiyo na viwanda haiwezi kuwa na ajira na nchi yenye biashara duni haiwezi kuwafanya vijana wake wajiajiri au waajiriwe.
Inabidi Mwijage na wenzake wawe wabunifu zaidi, wapambane kujua biashara zipi zinahitajika sana kwa sasa, za ndani na nje, kuwe na tarifa za kutosha ikiwa mtu anataka kuwekeza, ashauriwe aende wilaya gani kuwekeza kwenye nini.
Lazima Mwijage awasimamie watendaji wake ili kila mara wawe wanajua wapi watapata wawekezaji katika sekta fulani, mikopo kwa ajili ya wamiliki wadogo wa viwanda itachukuliwa wapi.
Sote tu mashahidi kuwa nyakati za mavuno huwa kuna mamilioni ya tani za matunda yanayooza kwa sababu hatuna viwanda vya kusindika hata juisi vijijini. Viwanda vya usindikaji wa namna hii havihitaji wawekezaji wakubwa, vinahitaji watu wa kipato cha kati wakopeshwe mashine na kuandaliwa kitaalamu kusimamia uzalishaji wa juisi.
HITIMISHO
Mwijage siyo waziri maarufu sana, anayo fursa kubwa ya kutumia kipengele hicho kufanya mabadiliko mengi yatakayoleta tija bila kupigiwa kelele, sekta nyeti kama viwanda na biashara ingeweza kukutana na matatizo mengi ikiwa waziri wake angeanza kuleta mabadiliko huku ana wakosoaji wengi.
Mwijage hana wakosoaji wengi hivi sasa na mara zote viongozi wa aina hiyo huwa na nafasi ya kufanya uhuishaji mkubwa kwenye sekta zao bila kuzuiwa na wadau. Atumie nafasi hiyo vizuri ili wakati ukifika ambapo jina lake litakuwa linakaririwa na kutajwa kila kona, wakati ambapo wakosoaji wake watakuwa wengi. Lakini atambue kuwa ikiwa hakutakuwa na viwanda vya kutosha ndani ya miaka mitano ya JPM huenda asimalize muda wake kwenye wizara hii au hata kwenye uwaziri wenyewe.
*Uchambuzi huu unatokana na utafiti na maoni binafsi ya mwandishi*
KUHUSU MCHAMBUZI
Julius Mtatiro ni Mchambuzi wa Masuala ya Kisiasa na Kijamii, ni mmoja kati ya vijana wenye uzoefu mkubwa na siasa za Tanzania. Ana Cheti cha Juu cha Sarufi (“Cert of Ling”), Shahada ya Sanaa “B.A” katika Elimu (Lugha, Siasa na Utawala), Shahada ya Umahiri ya Usimamizi wa Umma (MPA) na Shahada ya sheria (L LB) – Simu: +255787536759, Tovuti: www.juliusmtatiro.com,
Email: juliusmtatiro@yahoo.com).
No comments :
Post a Comment