Serilali ya JK ilikuwa ikikusanya wastani wa Sh. bilioni 900 kwa mwezi.
Kuwapo kwa utofauti ya wastani wa Sh.bilioni 500 kwa mwezi wa makusanyo ya kodi baina ya serikali ya Magufuli na ya Kikwete, inaonyesha kulikuwapo na mianya mingi ya uvujaji wa mapato kwa miaka mitano ya mwisho ya uongozi wake kuliko tu wizi wa makontena katika Bandari ya Dar es Salaam.
Kaimu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Alphayo Kidata, aliwaambia waandishi wa habari Januari 4 kuwa wamevuka lengo la makusanyo ya mwezi Desemba; baada ya kukusanya Sh. trilioni 1.4, ikiwa ni ongezeko la wastani wa Sh.bilioni 500 kwa mwezi.Kwa kipindi cha miaka mitano ambayo ni sawa na miezi 60 ya uongozi wa Rais Kikwete, TRA haikuwahi kupata kiwango cha makusanyo ya kodi kama kilichofikiwa na uongozi wa Rais wa tano Magufuli, kwa mwezi mmoja.
Kwa maana hiyo inadhihirisha kuwa kwa kipindi cha 2010-2015, watendaji waliopewa dhamana ya kukusanya kodi walishindwa kumsaidia Rais kukusanya kodi vizuri, ambayo ingewasaidia wananchi kupata huduma muhimu za kijamii.
Wakati akilihutubia bunge mjini Dodoma Novemba 20, mwaka jana, Rais Magafuli alisema katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita ukusanyaji wa mapato umekuwa chini ya makadirio kwa sababu mbalimbali ikiwamo watendaji kutosimamia vizuri makusanyo hayo pamoja na rushwa.
Alieleza kuwa serikali atakayoiunda itaongeza nguvu katika upanuzi wa wigo wa kodi na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato.
“Tutahakikisha kwamba kila mtu anayestahili kulipa kodi analipa kodi stahiki," alisema Rais Magufuli na kufafanua "hatutasita kumchukulia hatua mtu yoyote atakaye kwepa kulipa kodi.
"Tunawaomba wananchi mhakikishe mnapewa risiti kila mnaponunua bidhaa au huduma. Kodi ni kitu muhimu lazima kila mtu anayestahili kulipa kodi alipe.”
Alieleza kuwa serikali yake itahakikisha kila senti inayoongezeka katika mapato ya Serikali inaelekezwa katika kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi, kwa kuziba mianya ya upotevu wa fedha za Serikali ambayo inaipunguza uwezo wake wa kuwahudumia wananchi.
Katika kutekeleza agizo hilo, tangu alipoapishwa Novemba 5 hadi 31, mwaka jana serikali ya Rais Magufuli ilikusanya kodi ya Sh. trilioni 1.3 kabla ya kufikia Sh. trilioni 1.4 Desemba, wakati lengo kuu likiwa ni kukusanya Sh.trilioni 12.3 kwa mwaka.
Katika kipindi cha mwezi Julai hadi Desemba, mwaka jana TRA, ilikusanya Sh.trilioni 6.4 kulinganisha na lengo la Sh.trilioni 6.5 ambayo ni sawa na asilimia 95.5 ya makusanyo yote.
TRILIONI 30 ZINGEWEZA KUFANYA NINI
Magari ya kubebea wagonjwa (Ambulance)
Agosti 28, 2014 kulikuwa na taarifa kwenye vyombo vya habari kuwa kampuni ya Biolands International ilikabidhi msaada wa gari la kubebea wagonjwa (ambulance) aina ya Nissan Patrol kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela lenye thamani ya Sh. milioni 76.
Kwa maana hiyo, kama Sh.trilioni 30 zingetumika kununulia magari ya kiwango cha lile la msaada Halmashauri ya Wilaya ya Kyela, maana yake taifa lingepata magari mapya ya kubebea wagonjwa 394,736 na hivyo kumaliza tatizo la ukosefu wa magari hayo katika vituo vya afya na hospitali nyingi nchini.
Uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwa kama Sh. trilioni 30 zinazokadiriwa zingekusanywa katika kipindi cha miaka mitano ya mwisho ya utawala wa Rais Kikwete, zingeweza kufanya mambo mengine mengi ya maendeleo kwa taifa.
MAABARA ZA SEKONDARI
Mkuu wa Shule ya Sekondari Tandika, Hussein Mpungusi, alikaririwa Aprili 20, 2015, akisema walikamilisha ujenzi wa maabara mojawapo shuleni hapo kwa Sh. milioni 58.2. Kwa sababu hiyo, Sh.trilioni 30 zingeelekezwa kwenye maabara jumla ya maabara 515,464 zingepatikana.
VISIMA VYA MAJI SAFI
Aidha, kwa mujibu wa Mbunge wa Singida Magharibi, Emmanuel Kingu (CCM), gharama ya kuchimba kisima cha maji safi kwenye jimbo lake ni wastani wa Sh. milioni 15. Kwa sababu hiyo, kama Sh.trilioni 30 zingetumika kuchimba visima vya kiwango sawa na vile vya Jimbo la Singida Magharibi, vingepatikana visima milioni 2.
MADAWATI
Mbunge wa Kingu aliwahi kukaririwa na gazeti hili mwaka jana akisema wastani wa bei ya dawati moja linalokaliwa na wanafunzi watatu wa shule ya msingi katika jimbo lake ni Sh. 15,000. Kwa sababu hiyo, Sh.trilioni 30 zingetosha kununua madawati billion 2 ya kiwango sawa kama ya Jimbo la Singida Magharibi na kumaliza tatizo hilo nchini kote na mengine yakabaki kwa kukosa wanafunzi wa kuyatumia.
BARABARA ZA LAMI
Vyanzo mbalimbali vinaeleza kuwa wastani wa kujenga barabara ya lami ya umbali wa kilomita moja ni Sh. bilioni moja. Kwa sababu hiyo, Sh.trilioni 30 zingeelekezwa katika ujenzi wa barabara, maana yake taifa lingepata barabara mpya ya urefu wa kilomita 30,000, ikiwa na maana kuwa kusingekuwa na barabara ya vumbi nchini.
MIKOPO WANAFUNZI ELIMU YA JUU
Katika uchunguzi wake, Nipashe imebaini kuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Shahada ya Uhandisi wa Madini katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) anayepata mkopo wa asilimia 100 hulipwa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) jumla ya Sh. 4,219,500 kwa mwaka.
Mchanganuo wa mkopo huo kwa mwaka wote wa masomo ni Sh. 2,099,500 kwa ajili ya chakula na malazi, Sh. 200,000 ya vifaa, Sh. 620,000 kwa ajili ya mafunzo ya vitendo, ada Sh. milioni 1.3.
Kwa sababu hiyo, ikiwa Sh.trilioni 30 zitatumika kuwakopesha wanafunzi wa elimu ya juu kama wa mwaka wa kwanza wa Shahada ya Uhandisi wa Madini wanaolipwa asilimia 100, maana yake wanafunzi milioni 7 wangenufaika na mkopo huo.
VIPIMO CT-SCAN
Vyanzo mbalimbali vya Nipashe vinaeleza kuwa kipimo maarufu cha CT-Scan, aina ya Phillips huuzwa kwa wastani wa Sh. milioni 600 hadi bilioni moja. Kwa kutumia bei ya juu, Sh.trilioni 30 zingeweza kununua CT-Scan 30,000 na kufungwa katika hospitali zote za rufaa nchini na nyingine nyingi zikabaki kwa hospitali za wilaya, vituo vya afya na zahanati katika kila kijiji.
MIKOPO KWA KINA MAMA
Akina mama wengi wanaojihusisha na biashara ndogo ndogo huhitaji mikopo ya kuanzia Sh. 50,000 hadi Sh. 500,000 tu ili kufanikisha biashara zao.
Kwa sababu hiyo, Sh.trilioni 30 kama zingetumika kuwakopesha wajasiriamali wanawake, wanufaika wangekuwa kina mama milioni 60 ambao kila mmoja angepata Sh. 500,000. Jumla ya Watanzani wote ni milioni 45 kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012.
WASOMI WANASEMAJE
Mkurugenzi wa Sera na Ushawishi wa Shirikisho la Viwanda katika sekta binafsi nchini (CTI), Hussein Kamote alisema wakati wa utawala wa Rais aliyetangulia kulikuwa na usimamizi usiokuwa madhubuti katika ukusanyaji kodi.
Alisema serikali isiangalie eneo la bandari tu katika makusanyo ya kodi bali iangalia katika Nyanja za Kodi ya Ongezeko la thamani (VAT) na Kodi ya Mapato.
“Eneo la ushuru wa forodha nalo liangaliwe, wafanyabiashara wengi wanaingiza bidhaa kupitia bandari bubu, pia kama serikali itawekeza katika maeneo ya kutengeneza uchumi nchi itasonga mbele,” alisema Kamote.
Alisema kukusanywa kwa Sh.trilioni 1.4 kunaweza kupunguza mahitaji ya kila mwaka ya kuongeza kodi katika pombe, sigara, sukari na mafuta.
Aidha, alisema kuongezeka kwa makusanyo ya kodi kutasaidia miradi ya maendeleo kutekelezwa, kukua kwa uchumi na kuimarishwa kwa miundombinu.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Uongozi na Ujasiriamali na masuala ya uchumi, Dk. Donath Olomi alisema makusanyo ya Sh.trilioni 1.4 yaliyofikiwa na serikali ya Rais Magufuli yanaonyesha hakukuwa na umakini wa makusanyo ya kodi kwa serikali iliyopita.
Alisema endapo pesa hizo zikitumika katika sekta za afya, elimu, mikopo kwa wanafunzi vyuoni itakuwa imegusa wananchi wengi wa maisha ya chini.
Naye Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi, Profesa Alphonce Kessy alisema kukusanywa kwa kiwango hicho kikubwa cha kodi kumedhihirisha kuwa serikali inaweza kukusanya kodi nyingi ambazo zinaweza kuisaidia nchi.
“Fedha zilizokusanywa ndizo ambazo wanafunzi wa vyuo vikuu sasa hivi wamepewa mikopo, ndizo zilizopelekwa katika shule na wanafunzi wanasoma bure, ndizo zilizopelekwa katika sekta ya afya kununulia dawa,” alisema Profesa Kessy.
Alisema pia hatua hiyo inaonyesha watendaji katika serikali iliyopita hawakuwa makini katika kusimamia na kutekeleza makusanyo ya kodi.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment