Chama cha Wananchi (CUF), kisiwani Pemba, kimevunja ukimya na kutangaza mandamano makubwa ya amani pamoja na mkutano wa hadhara kwa lengo la kuunga mkono taarifa ya Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad kwa vyombo vya habari aliyoitoa Januari 11 mwaka huu.
Maandamano hayo, kwa mujibu wa chama hicho, yatatumika kulaani kitendo cha Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kufuta Uchaguzi Mkuu, kinyume na matakwa ya Katiba ya Zanzibar.
Kauli hiyo ilitolewa na katibu wa chama hicho Wilaya Chake Chake, Salehe Nassor Juma, mbele ya waandishi wa habari kwenye mkutano uliojumuisha waliowania nafasi za ujumbe wa Baraza la Wawakilishi, Wenyeviti na Makatibu wa Wilaya na majimbo pamoja na wajumbe wa Baraza Kuu la CUF Taifa waliopo Pemba.
Juma alisema wamepeleka barua kwa Kamanda wa Polisi, Wilaya Chake Chake kumjulisha juu ya mandamano hayo ya amani yanayotarajia kuanza Chanjaani, njia ya uwanja wa ndege hadi kibirizi kesho.Alisema maandamano hayo yatajumuisha wananchi wa mikoa miwili ya Pemba.
Alisema mandamano hayo yanaunga mkono taarifa ya Katibu Mkuu na wapo pamoja naye katika jitihada zake za kutafuta muafaka na haki ya wazanzibari ambayo ipo hatarini kuporwa.
Naye Rashid Khalid Salim, ambaye ni Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Micheweni, alisema wameamua kuvunja ukimya na kuzungumzia juu ya mambo yaliyojitokeza, ikiwa pamoja na kuwapongeza wanachama kwa kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 na kuichagua CUF.
Oktoba 27, mwaka jana, Jecha alitangaza kufuta matokeo ya uchaguzi visiwani humo, akisema uchaguzi huo ulijaa kasoro nyingi.
Jecha alisema kuwa uchaguzi huo haukuwa wa haki na kwamba kulikuwa na ukiukaji mkubwa wa sheria za uchaguzi.
Alisema baadhi ya makamishna wa tume hiyo, badala ya kutekeleza majukumu yao inavyotakiwa kikatiba waligeuka kuwa wawakilishi wa vyama vyao.
"Kumegundulika kasoro nyingi katika uchaguzi huu miongoni mwa hizo ni kubainika kwa baadhi ya vituo; hasa Pemba vimekuwa na kura nyingi kuliko daftari la wapiga kura wa kituo husika," alisema.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment