WIZARA ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi imeteua shule sita za sekondari nchini kuingia katika mpango maalumu wa wanafunzi wake kufundishwa somo la lugha ya Kichina kuanzia mwaka huu.
Kutokana na uamuzi huo, walimu 12 kutoka China wamekamilisha utaratibu wa mpango kazi wa namna ya ufundishaji wa somo hilo kwa shule zilizoteuliwa mara zitakapofunguliwa rasmi mwezi huu.
Ofisa Elimu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Salum Salum, alitaja shule zilizoingizwa kwenye mpango huo katika awamu ya kwanza ni Benjamin Mkapa na Chang’ombe (Dar es Salaam), Msalato na Dodoma (Dodoma), Morogoro na Kilakala za mkoani Morogoro.
Salum alitoa taarifa hiyo juzi wakati akifungua mafunzo ya kazi na mipango mikakati iliyoandaliwa na Taasisi ya China inayojihusisha na lugha ya Kichina kwa walimu wake walioteuliwa kufundisha somo la lugha ya kichina katika shule hizo.
Alisema kabla ya kufunguliwa kwa shule, viongozi wa China wamekutana kwa siku mbili mjini Morogoro kufanya mafunzo ya kazi ya kujiandaa kuingia darasani baada ya shule kufunguliwa.
Alisema kabla ya kufunguliwa kwa shule, viongozi wa China wamekutana kwa siku mbili mjini Morogoro kufanya mafunzo ya kazi ya kujiandaa kuingia darasani baada ya shule kufunguliwa.
“Mafunzo kazini ni ya kujiandaa na kupeana mikakati na nini kifanyike kabla ya shule kufunguliwa ili kuingia madarasani kufundisha wanafunzi wa kitanzania lugha ya kichina,” alisema Ofisa Elimu Mkuu.
Alisema wanafunzi watatahiniwa somo hilo la lugha ya kichina katika mitihani yao na watakapohitimu watahesabiwa alama za ufaulu sawa na yalivyo masomo mengine yanayofundishwa katika shule za sekondari kama ilivyo kwa Kifaransa na Kijerumani.
Alisema wizara inaona ni njia nzuri kwa vijana wa Kitanzania kuwa na lugha ya mawasiliano katika kuwasaidia kujifunza zaidi na kutumia fursa zitakazopatikana China ikiwemo kujiendeleza na elimu ya juu zaidi.
Mkurugenzi wa Taasisi ya China ya lugha ya kichina, Ambar Zheng, kutoka katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), alisema walimu 12 wa China wameshapatiwa mafunzo ya namna ya kufundisha somo hilo kwenye shule husika.
Alisema kila shule ya sekondari iliyoteuliwa katika mikoa hiyo ya Dodoma, Dar es Salaam na Morogoro, zitapangiwa walimu wawili kila moja kwa ajili ya kufundisha somo hilo kuanzia mwaka wa masomo unaoanza mwezi huu.
Alipongeza ushirikiano mzuri uliooneshwa kati ya Serikali ya Tanzania na China na wizara husika kuwezesha kuanzishwa kwa somo hilo katika baadhi ya shule za sekondari nchini. Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Waislamu cha Morogoro, Profesa Hamza Njozi alipongeza Serikali ya China kwa kuendeleza ushirikiano katika nyanja mbalimbali, ikiwemo elimu ya vyuo vikuu.
CHANZO: HABARI LEO
No comments :
Post a Comment