Na Joster Mwangulumbi , Mwananchi.
Historia ni mwalimu mzuri. Migogoro mingi ya kisiasa hutokana na kiburi cha watu wenye madaraka ambao hudhani wanaweza kupambana na nguvu ya umma kwa mitutu ya bunduki na makombora yaliyonunuliwa kwa ajili ya vita.
Watawala wa Zanzibar wana fursa ya kujifunza kwa yaliyotokea Myanmar. Jeshi katika nchi hiyo lilitaka kumfuta kwenye historia mpigania haki Aung San Suu Kyi lakini lilishindwa. Jeshi lilimzuia kushiriki siasa, likamweka chini ya kifungo cha nyumbani lakini chama chake cha NLD kiliposhiriki uchaguzi mwaka 1990 yeye akiwa kifungoni kilishinda kwa asilimia 59. Jeshi likafuta uchaguzi.
Baada ya jeshi kugundua mwanamke huyo hazuiliki na alikuwa na mbinu za kumfunika lilimwachia huru mwaka 2010 ila lilisimamia mabadiliko ya Katiba. Katika Katiba kiliingizwa kifungu kinachosema mtu yeyote ambaye atakuwa ameolewa na raia wa kigeni hawezi kuwa rais. Walimlenga Suu Kyi ambaye aliolewa na Mwingereza na kwamba watoto wake wana hati za kusafiria za Uingereza.
Mwanasiasa huyo aliyezaliwa Juni 19, 1945 enzi nchi hiyo ikiitwa Burma katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Novemba 8, 2015, NLD ilishinda kwa asilimia 86 hivyo kuwa na fursa ya kumchagua rais na makamu wa rais. Kuhusu kifungu cha kikatiba kinachomzuia yeye kuwa rais, mwanamke huyo mshindi wa Tuzo ya Nobel alisema “kwa vyovyote itakavyokuwa nitakuwa juu ya rais.”
Seif na njia ya Suu Kyi
Njia hiyo aliyopita Suu Kyi ndiyo amepita Seif Sharrif Hamad tangu mwaka 1988 visiwani Zanzibar. Bila shaka Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein ana jambo la kujifunza kutoka Myanmar.
Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir Mayardit alipoona makamu wake wa rais (wakati huo) Riek Machar akijiandaa kuwania kiti cha enzi kupitia chama tawala cha SPLM, alikasirika akamfukuza ili akose pepo. Alikandamiza wazo lolote pinzani ndani ya chama hicho.
Kiir aliiridhisha nafsi yake kuwa hakutakuwa na upinzani tena lakini Desemba 2013 wakati wa mkutano wa ndani wa SPLM ziliibuka tofauti na ghafla mapigano yakaanza nje. Sudan Kusini ambayo ilikuwa na takriban miaka miwili tangu ipate uhuru wake ikawa imetumbukia kwenye moto wa risasi, makombora na maroketi uliokuwa unarushwa kuua kabila pinzani.
Mamia ya watu wamekufa, maelfu wamekosa makazi, na uchumi umeporomoja. Baada ya kiburi cha miaka mingi hatimaye Kiir amepata akili ameridhia mapendekezo ya Jumuiya ya Kimataifa ya kumaliza uhasama kwa kugawana madarakana hasimu wake.
Bila shaka Rais Ali Mohamed Shein ana jambo la kujifunza ili asiifikishe Zanzibar huko iliko Sudan Kusini.
Pierre Nkurunziza akihangaikia kufia Ikulu aliamua kuipa tafsiri mpya Katiba iliyokuwa inamzuia kugombea urais kwa muhula wa tatu. Baada ya mazungumzo ya muda mrefu ya kumaliza uhasama Burundi iliandaliwa Katiba kwa kuzingatia makubaliano ya mjini Arusha kwamba rais aliyechaguliwa na wananchi hataongoza zaidi ya vipindi viwili vya miaka mitano mitano.
Ili kuirejesha haraka nchi kwenye utawala unaoeleweka wa kiraia, Bunge la Burundi lilipewa mamlaka ya kumchagua rais kwa niaba ya wananchi na aliyeshinda alikuwa Nkurunziza na aliapa kuheshimu na kuilinda katiba. Nkurunziza aliwania kipindi cha pili akashinda na kwa kuzingatia makubaliano ya Arusha mihula yake iliisha Juni 2015 lakini kwa hila amewania tena akidai huu ndiyo muhula wa pili kuchaguliwa na wananchi maana ule unaodaiwa kuwa wa kwanza alichaguliwa na Bunge.
Mgawanyiko ulitokea kwenye chama chake, wasaidizi wake walikimbilia uhamishoni na baadhi ya wajumbe wa Tume ya Uchaguzi ya Burundi (CENI) walitoroka kupinga tafsiri batili ya Nkurunziza.
Tangu Aprili 2015 alipolazimisha kuteuliwa na chama chake cha CNDD-FDD kuwania urais na kushinda uchaguzi huo uliofanyika Julai, zaidi ya watu 400 wamekufa katika mapambano kati ya vikosi vya serikali na raia wanaopinga rais huyo anayedaiwa mlokole kuongoza tena.
Bila shaka Rais Ali Mohamed Shein ana jambo la kujifunza ili asiifikishe Zanzibar huko iliko Burundi.
Joseph Kabila aliyeshika madaraka nchini DRC mwaka 2001 baada ya baba yake, Laurent Desire-Kabila kuuawa alisimamia marekebisho ya Katiba yaliyoweka ukomo wa mihula miwili ya miaka mitano mitano. Alichaguliwa kidemokrasia kwa mara ya kwanza mwaka 2006 na mara ya pili 2011 lakini sasa hapati usingizi; anahangaika kuhakikisha anagombea tena licha ya katiba ya kumzuia.
Jaribio lake la kutaka ifanyike kwanza sensa ya watu na makazi mwaka jana lilipokewa kwa maandamano. Hadi leo hakuna mchakato unaoeleweka kuhusu uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu. Msuguano ni mkubwa lakini kwa vile yeye ni Amiri Jeshi hajali.
Bila shaka Rais Ali Mohamed Shein ana jambo la kujifunza ili asiifikishe Zanzibar huko iliko DRC.
Rwanda
Paul Kagame aliamua kutumia njia tofauti nchini Rwanda. Akionekana kama mtu asiyependa kufia madarakani alifanya ushawishi matawi ya chama chake yaanze kupiga debe ukomo uliowekwa kikatiba uondolewe.
Kura ya maoni iliandaliwa ukomo wa mihula miwili ya miaka saba saba kwa rais ukaondolewa, naye siku ya Mwaka Mpya alitoa neno.
“Lakini sifikiri kwamba lengo letu ni kuwa na rais wa maisha, wala mimi sihitaji,” alisema Kagame. “Haraka, kadri inavyowezekana, ofisi hii itakaliwa na mtu mwingine katika namna itakayosaidia kuendeleza kusudi hilo, siyo kwa kuweka mfano tu iwe sisi au wengine.”
Hayo ndiyo maneno aliyoamua kuyatumia siku ya Mwaka Mpya akipokea kwa furaha matokeo ya Kura ya Maoni ambayo yamemtengenezea njia pana ya kuomba vipindi vingine aweze kutawala bila shaka hadi mwaka 2034.
Kagame aliyeongoza kundi la kijeshi la RPF na ambaye alifanikiwa kuingia madarakani baada ya mauaji ya kimbari mwaka 1994 akiwa makamu wa rais, aliiongoza Rwanda kuandika Katiba iliyoweka ukomo wa mihula miwili ya uongozi kila kimoja kikiwa cha miaka saba. Kwa kuzingatia katiba hiyo, alichaguliwa kuwa Rais wa Rwanda kwa mara ya kwanza mwaka 2004 na mara ya pili 2011 lakini hata kabla hajamaliza muhula wa pili, ukoma umeondolewa na yeye amepewa fursa ya kugombea tena na tena.
Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amechelewa na hawezi kutumia mbinu za Kagame, Kabila wala Compaoré. Yamemkuta. Baada ya kuishi peponi miaka mitano, mwelekeo wa matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015 unaonyesha hawezi kurudi peponi, inabidi akabidhi pepo.
Dk Shein amegeuka. Anaukataa uchaguzi ulioandaliwa na serikali ya chama chake; sheria na refa (Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar-ZEC) wa CCM. Katika mazingira tata dola ikatumika.
CCM imeamua kumtumia refa, Jecha Salum Jecha kuzua mgogoro. Baada ya kusimamia uchaguzi na kutoa hati za ushindi kwa wagombea wa udiwani na baraza la wawakilishi, Jecha alitimua mbio akaenda peke yake kwenye vyombo vya habari vya serikali na kufuta uchaguzi akidai kuna hitilafu zilijitokeza.
Hadi Jecha anafikia uamuzi huo, matokeo yalikuwa yanaonyesha mpinzani wa Dk Shein, Seif Sharrif Hamad wa CUF alikuwa anaongoza.
Dk Shein ameshikilia hapo kwamba uchaguzi lazima urudiwe huku Maalim Seif akisema kamwe hawatashiriki. Dk Shein hataki kuachia madaraka kama Kabila, Kagame na hata Yoweri Museveni wa Uganda.
*Kwa mawasiliano tuma ujumbe kwa mwangulj@gmail.com
No comments :
Post a Comment