Zanzibar. Wakati hali ya kisiasa Zanzibar ikiendelea kuwa njia panda msemaji wa tawi maarufu la CCM Kisonge lililopo Michenzani mjini hapa, Seleman Omar ‘Ganzi’ ameshauri iundwe tume ya maridhiano kwa lengo la kupatanisha pande zinazokinzana.
Mbali na kutoa ushauri huo, Ganzi alishauri pande hizo, kuombana radhi kwa dhati kwa lengo la kufuta chuki na uhasama ambao umedumu kwa muda mrefu.
Oktoba mwaka jana, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha, alifuta matokeo ua Uchaguzi Mkuu akisema ulijaa dosari na kasoro nyingi ikiwamo mgombea wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kutangaza kuwa alikuwa anaongoza katika kinyang’anyiro hicho.
Matumaini ya kupatikana mwafaka katika mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea baina ya viongozi waandamizi visiwani hapa hivi karibuni yaliingia doa baada ya Maalim Seif na Dk Ali Mohamed Shein kutoa kauli zinazokinzana kuhusu hatima ya mkwamo huo wa kisiasa.
Wakati Maalim Seif akisema msimamo wake na wa chama chake ni kuendelea kutangazwa kwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 na kwamba kurudia ni kuvunja Katiba ya Zanzibar na haikubaliki, Dk alisema suala la kurudiwa kwa uchaguzi huo liko wazi na kinachosubiriwa ni ZEC kutangaza tarehe na kuwataka Wazanzibari wajiandae.
Msemaji huyo wa Tawi la Kisonge alisema kinachohitajika sasa ni maridhiano ili kumaliza mgogoro huo.
Aliwashutumu baadhi ya viongozi wa kisiasa kwamba wamekuwa wakitumia fimbo ya vijana kujinufaisha katika mgogoro huo.
“Viongozi wengi wanatumia fimbo ya vijana kukosa ajira hapa Zanzibar kwa lengo la kujinufaisha kimasilahi hili ni tatizo,” alisema.
Alisema mgogoro huo umesababisha kuzorota kwa uchumi wa Zanzibar na kuitaka Serikali kuchukua hatua za haraka kuunusuru hali hiyo.
Akizungumzia tuhuma kuhusu baadhi ya maneno yanayochochea chuki na uhasama Zanzibar ambayo yamekuwa yakiandikwa katika bango lililopo katika maskani hiyo, msemaji huyo alikanusha na kusema kwamba maneno hayo hayana lengo la kuchochea chuki, bali kueleza ukweli wa hali halisi inayoendelea Zanzibar.
No comments :
Post a Comment