Kama mtu anapata angalau mlo mmoja kila siku na huku anapitisha siku moja, mbili au tatu bila ya kupata choo kikubwa, anatatizo la kukosa choo, hivyo anahitaji kupatiwa ushauri wa kitabibu.
Mtu akikosa choo kikubwa kwa siku tano mpaka saba mfululizo anaweza kupoteza maisha.
Vilevile, kama mtu anapata choo kigumu au kidogo, anasikia maumivu makali au atakuwa anapata choo kinachoonekana kama punje kama cha mbuzi na wakati mwingine kikiwa na damu, ni wazi kuwa anakabiliwa na tatizo la kukosa choo.
Pia, watu wenye matatizo ya kukosa choo hutumia nguvu na muda mwingi wakati wa kujisaidia haja kubwa, hukosa hamu ya chakula na wakati wote tumbo huwa limejaa.
Kwa kawaida mtu mwenye afya njema anapaswa kupata choo cha uhakika mara moja au mbili kwa siku.
Tatizo la kukosa choo kwa watu wazima husababishwa zaidi na ulaji usiofaa, kutokunywa maji ya kutosha kila siku, maradhi, matumizi ya sigara, pombe kupita kiasi na maisha ya kukaa bila ya kufanya mazowezi au shughuli za kutoka jasho.
Vyakula vya watu wengi wanaoishi katika miji ni vile vinavyotokana na wanyama na vyakula vilivyotengenezwa kwa kutumia nafaka zilizokobolewa (kama mikate meupe). Vyakula hivi havina nyuzinyuzi za kutosha, kwa hiyo vinachochea magonjwa kama vile kisukari, uzito, unene kupita kiasi, kansa ya utumbo mpana na kukosa choo kikubwa.
Mtu anapokosa choo kikubwa kwa siku nyingi, uchafu hujikusanya tumboni na sumu na vijidudu (bakteria) vilivyomo katika kinyesi huingia katika mfumo mzima wa damu na kusababisha maradhi mbalimbali.
Ukosefu wa choo kikubwa unaweza kuchochea matatizo mengine mwilini kama vile saratani ya utumbo mpana, presha, uzito kupita kiasi, tumbo kujaa gesi, kisukari, magonjwa ya ini, figo, kushindwa kufanya kazi vizuri, kukakamaa kwa mishipa ya damu, magonjwa ya ngozi na magonjwa ya moyo.
Ili kupunguza hatari ya kukosa choo kikubwa watu wajenge tabia ya ulaji unaofaa ikiwemo kula vyakula vya mbogamboga.
Mboga mboga ni chanzo muhimu sana cha nyuzi lishe (dietary fiber), vitamini, madini na kemikali nyingine zinazo usaidia mwili kupambana na maradhi. Kuongeza virutubisho vya aina hii katika mlo wa asubuhi vikiwa kama saladi, matunda au juisi itauwezesha mwili kuondoa sumu na kuimarisha kinga na afya kwa ujumla.
Kunywa maji safi na salama ya kutosha kila siku ni tabia nyingine ya ulaji unaofaa. Kunywa maji ya kutosha kuna manufaa mengi ikiwemo kuuwezesha mwili kufanya kazi barabara, kukua vizuri, kusaga chakula vizuri, kujikinga na maradhi, kupoza mwili, mwili kutoa sumu mwilini hasa kwa njia ya mkojo, kuimarisha ngozi, kupunguza uzito, mtu kupata choo kikubwa mara kwa mara, kuondoa uchovu wa viungo na kuzuwia kuumwa kichwa.
Kupunguza ulaji wa vyakula vya kukaanga na vile vya “fast food” ni katika ulaji unaofaa.
Usile mikate meupe au vyakula vingine vinavyotokana na nafaka zilizokobolewa bila ya kula na mboga za majani za kutosha. Kwa siku mtu mzima ale vikombe vitatu au mafungu (kama yale ya mchicha) matatu ya mboga za majani.
Maswali na majibu piga na sms kwa simu: 0655 654900
/Mwananchi.
No comments :
Post a Comment