Katika eneo la demokrasia, utawala wa Katiba na sheria, utawala bora na mambo kama hayo ameingilia mguu wa kulia. Hivi karibuni Rais mwenyewe wakati anahutubia siku ya sheria alisisitiza “yeye si dikteta” na akaomba Watanzania waelewe kuwa kuna mambo lazima afumbe macho ayafanye kwa sababu hali ndani ya Serikali ni mbaya.
Naam! Mbona suala la Zanzibar hafumbi macho na kuliingilia kama Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi ya Ulinzi na Usalama na Mkuu wa Tanzania?
Unajua mtu anaweza kuwa siyo dikteta kama anavyoomba Magufuli aeleweke. Lakini vitendo vinavyotendwa na mtu husika au wanaofanya naye kazi katika mstari mmoja vikaleta dhana ya udikteta na mwishoni mhusika ‘mkuu’ hurundikiwa udikteta kamili na kuukwepa kwa maneno hakutoshi kwani madikteta hufanya mambo kwa vitendo na wanaweza kuyaepuka kwa vitendo pia.
Hakuna uwezekano wa kuondoa vitendo vya udikteta kwa maneno na huwezi kukwepa kuitwa dikteta kama walioko chini yako wanafanya vitendo vya kidikteta na wewe uliyeko juu huwachukulii hatua na unaendelea kufanya nao kazi wakati wanavunja katiba na sheria.
Maamuzi ya Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Zanzibar, Jecha Salum Jecha ya kufuta matokeo ya uchaguzi halali unaomhusu rais wa Zanzibar, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na madiwani ulifanywa kwa kuvunja Katiba na Sheria za Zanzibar (hilo lilishaelezwa).
Maamuzi hayo yameleta mkwamo mkubwa Zanzibar na yamevunja miiko mikubwa ya utawala wa sheria na maamuzi ya wananchi kwani wao ndiyo huamua nani awaongoze. Yalipotokea hayo ya Jecha aliyekuwa Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete alibariki vitendo hivyo vya kidikteta vilivyofanywa na mwenyekiti wa ZEC, Kikwete akaenda mbali zaidi, akaendelea kumtambua Dk Shein kama Rais wa Zanzibar na mwana CCM mwenzake bila kujali kuwa Shein na ZEC hawana uhalali na mamlaka ya kimaadili kuendelea na nyadhifa zao. Huku kumekuwa ni kuunga mkono vitendo vya kidikteta bila kuficha.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimekutana kwenye vikao vyake, kikapongeza na kukubaliana na maamuzi ya ZEC (kikayahalalisha) kwa kujibaraguza ati “tumeyapokea na kuyakubali kwa shingo upande”, kikatangaza kitashiriki kwenye uchaguzi ulioitishwa kinyume cha sheria na katiba, kibabe, kwa kuvunja miiko ya demokrasia na utawala bora.
Kwa hiyo CCM ikaingia katika mtego wa kuunga mkono ‘udikteta na ubabe’ na mawaziri wa CCM wakiwamo vijana kama January Makamba wamesikika wakiweka bayana kuwa msimamo wa Serikali pia ni kurudia uchaguzi ulioitishwa na NEC. Kwa hiyo hawa pia kwa niaba ya serikali wanaunga mkono udikteta bila kujificha.
Majadiliano ya maridhiano yalipoanza mtu anayetuhumiwa kuidhinisha vitendo vya kidikteta vifanywe Zanzibar ili vimlinde akaamua kuendeleza mchezo huo. Akajitwisha uenyekiti wa vikao vya maridhiano bila kujali kuwa yeye ni sehemu ya mgogoro. Unakuwa mchezaji kwenye mechi, unajigeuza refa na kumhujumu mchezaji mwenzio lakini anapokujulisha haja ya kukata rufaa na kupata maoni ya mahakama ya juu zaidi, wewe tena ndiye unakuwa mkuu wa majaji wa mahakama hiyo! Udikteta wa hali ya juu!
Na kama hiyo haitoshi, baada ya mazungumzo kwenda kombo, mtuhumiwa mkuu wa ‘masuala ya Zanzibar’, Dk Shein amekuja hadharani na kutamba mbele ya wana CCM kwamba “lazima CCM ishinde” na ndiyo jukumu la chama hicho (ushindi ni lazima). Shein anasisitiza juu uendelezaji wa vitendo vya kidikteta na anaungwa mkono na wana CCM na wakubwa wenzake bila aibu. Ameng’ang’ania madarakani. Udikteta ni vitendo.
Msajili wa vyama vya siasa tena jaji wa Mahakama Kuu anaviandikia vyama vya siasa barua ndefu akijenga hoja zisizo na mbele wala nyuma, kuunga mkono haya ya Zanzibar, bila soni wala aibu! Jaji, mtoa haki! Anavisisitiza vyama vishiriki uchaguzi ili kukidhi matakwa ya kidikteta. Anaweza kujificha nyuma ya pazia lakini anaonekana kirahisi. Udikteta ni vitendo.
Hotuba ya Mwenyekiti wa CCM, Kikwete, mwanadiplomasia wa muda mrefu, mtatuzi mashuhuri wa migogoro duniani, anasimama hadharani kusisitiza lazima CCM isonge mbele na itimize kiu yake, ushindi wa chama chake Zanzibar ni wa lazima! Udikteta na vitendo.
Funga kazi ni msimamo wa mkuu wa nchi, John Pombe Magufuli, huu unatolewa na Waziri wake wa Mambo ya Nje, mwanadiplomasia nguli Dk Augustine Mahiga. JPM anasisitiza kuwa suluhisho la uvunjifu wa Katiba na sheria uliotokea Zanzibar baada ya kupangwa kimakusudi, ni kurudia uchaguzi, kupokonya haki na sauti za wananchi. Udikteta ni vitendo.
Dhana ya udikteta ni pamoja na kukubali walioko chini yako au wanaofanya kazi juu yako au sambamba na wewe, wafanye vitendo vya kidikteta na tena unaweza kutovikubali vitendo hivyo lakini ukakaa kimya, ukatulia tuli kama maji ya mtungi na kuacha udikteta utamalaki, wewe utaitwaje?
Hakuna jambo hatari duniani kama kuyakalia kimya maovu. Wanafalsafa husema mambo maovu siyo hatari kwa dunia kuliko watu wanaotizama na kutoyakemea maovu hayo, tena wakiwa na mamlaka ya kufanya hivyo.
Julius Mtatiro (Adv Cert in Ling, B.A Hons, M.A Hons, LL B Hons) www.juliusmtatiro.com. Baruapepe: juliusmtatiro@yahoo.com,0787 53 67 59.
No comments :
Post a Comment