Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Saturday, February 13, 2016

Maalim Seif aitoa hofu CCM

Katibu Mkuu wa CUF, Seif Shariff Hamad akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana baada ya kukutana na waziri mkuu mstaafu Edward Lowassa jana.Picha na Emmanuel Herman
By Florence Majani, Mwananchi
Dar es Salaam. Wakati saa 864 zimesalia kabla ya kurudiwa kwa uchaguzi wa Zanzibar, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad amehoji sababu za chama tawala cha CCM kuhofia CUF kuongoza visiwa hivyo.
Maalim Seif ambaye aligombea urais wa Zanzibar katika uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka jana ambao matokeo yake yalifutwa, pia amesema endapo CCM itasitisha uchaguzi uliopangwa kufanyika siku 36 zijazo, CUF itakuwa tayari kufanya mazungumzo, lakini siyo wakati huu ambao maandalizi ya kupiga kura yanaendelea.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, katibu huyo mkuu wa CUF aliitoa hofu CCM kuwa chama chake hakina ajenda ya kulipiza kisasi.
Matokeo ya uchaguzi wa Rais wa Zanzibar, wawakilishi na madiwani yalifutwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salum Jecha siku ambayo chombo hicho kilitakiwa kumtangaza mshindi, na mwezi uliopita alitangaza Machi 20 kuwa siku ya uchaguzi wa marudio visiwani humo.
Wakati CUF ikipinga vikali kufutwa matokeo na kutangaza tarehe mpya, Serikali imesema kuna nafasi ya kufanya mazungumzo kabla ya uchaguzi wa marudio kwa kuwa kuna muda ni mrefu wa kufanya hivyo.
Jecha alitangaza uamuzi huo wakati tayari matokeo ya urais ya majimbo 31 yalishatangazwa, na ya majimbo tisa yaliyosalia yalishahakikiwa, huku washindi wa viti vya uwakilishi na udiwani wakiwa wametangazwa na kupewa vyeti vya ushindi.
“Sijui kwa nini CCM wanaogopa sisi tukiongoza?” alihoji Maalim Seif kwenye mkutano huo na waandishi akiwa pamoja na aliyekuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa.
“Wana wasiwasi gani, kwamba CUF ikiongoza kutatokea nini? Sisi hatuna ajenda ya kulipiza kisasi,” alisema.
Katika mkutano huo, Maalim Seif mbaye pia ni katibu mkuu wa chama hicho alisema kama CCM ina wasiwasi na idadi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), haina budi kuondoa shaka kwa kuwa idadi kwa pande zote inakaribiana.
“Hawa wanahisi hawatapata uwakilishi mkubwa, lakini mbona miaka yote tunakuwa na idadi isiyopishana ya wawakilishi?” alihoji.
Hali ilivyo Zanzibar
Katika mkutano huo, Maalim Seif alisema kumekuwapo vitendo vya wananchi kupigwa na vikundi vya watu wasiojulikana.
Alidai wafanyakazi wa Serikali na taasisi zake wameamrishwa kupeleka vitambulisho vyao vya kazi na vya kura serikalini ili vikahakikiwe.
“Hii si mara ya kwanza wafanyakazi wa Serikali kutakiwa kupeleka vitambulisho, sisi tunajua kuwa wanataka wawatishe kuwa watajua nani kapiga kura na nani hajapiga,” alisema na kusisitiza:“Hii ni kama kitisho cha kuwalazimisha wakapige kura, zaidi hasa hizo ni dhuluma ambazo wananchi wanafanyiwa.”
Uwapo wa mazombi
Kadhalika Maalim Seif alizungumzia uwapo wa watu wanaovaa soksi usoni na kuwashambulia raia, akisema Serikali haijachukua hatua stahiki kudhibiti hali hiyo.
Alisema watu hao ambao wamepachikwa jina la mazombi, wamevamia maeneo kadhaa kama Baraza la CUF, Jang’ombe na yaleambayo yana wafuasi wa chama hicho kikuu cha upinzani visiwani humo.
“Wanawapiga watu, wanawajeruhi na wanaiba mali, lakini inashangaza sana mambo haya na si Serikali wala polisi iliyochukua hatua,” alisema.
Maalim Seif alisema amezungumza na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kuhusu matukio hayo ya uharamia wanaofanyiwa wananchi, lakini hakuna hatua zinazochukuliwa.
Alisema CCM wanatafuta sababu ili machafuko zaidi yatokee visiwani humo wapate kisingizio.
Aliwataka wafuasi wa CUF kuvumilia hali hiyo ili nchi isiingie kwenye machafuko kama yaliyotokea mwaka 2000, wakati watu zaidi ya 20 waliuawa na wengine kukimbilia Shimoni, Mombasa nchini Kenya ambako waliishi kama wakimbizi.
Lowassa azungumza
Kwa upande wake, Lowassa aliwataka viongozi wa ngazi za juu wachukue hatua kumaliza mgogoro wa Zanzibar.
“Hili tulichukulie kwa umakini sana. Viongozi wafanye vikao vya maridhiano, tunaipenda sana amani tuliyonayo,” alisema.
Lowassa alisema anashangazwa na jinsi CCM wanavyoshindwa kuheshimu makubaliano ya SUK na kukataa kukubali matokeo.  

No comments :

Post a Comment