Mratibu wa mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Olengurumwa
Dar es Salaam. Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), unatarajia kufungua kesi kupinga Sheria ya vyombo vya habari baada ya kubaini kuwa ina mapungufu.
Akizungumzia tathmini waliyofanya katika siku 100 za uongozi wa Rais John Magufuli, Mratibu wa mtandao huo, Onesmo Olengurumwa alisema wamebaini mambo mengi kuhusu haki za binadamu, uhuru wa habari, demokrasia na utawala bora na Uchaguzi Mkuu Zanzibar hayakwenda sawa.
Alisema katika tathmini hiyo wameshangazwa na hali mpya inayojitokeza ya uvunjifu wa uhuru wa vyombo vya habari na haki ya kupata taarifa, ikiwamo kufutwa kwa gazeti la Mawio.
Olengurumwa alisema kesi ya msingi itakuwa ni kuhakikisha wanapinga vitu vyote vinavyokandamiza dhana nzima ya uhuru wa habari na kudai marekebisho ya Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 ambayo imeendelea kuvunjwa na kukiuka uhuru huo.
“Sheria hii imeendelea kuwa kandamizi kama ilivyotumika kwa gazeti la Mwanahalisi mwaka 2012 na kusitishwa kwa muda magazeti ya Mwananchi na Mtanzania mwaka 2013, na sasa imefungia moja kwa moja gazeti la Mawio,” alisema.
Alisema wameshtushwa na hali hiyo kwa sababu Serikali yenye lengo la kuwasaidia wananchi kupambana na rushwa ni lazima iweke mbele uhuru wa habari, uwazi na ukweli.
Alifafanua kuwa kwa miaka kadhaa sheria ya magazeti imekuwa ikiorodheshwa kama inayokiuka uhuru wa kujieleza, huku ikimpa waziri mwenye dhamana nguvu kubwa.
No comments :
Post a Comment