Uongozi aliopewa ni wa miaka mitano na siku 100 za kwanza ambazo zinafikia kilele leo, zinatoa dira ya utekelezaji wake, ingawa mpaka sasa baadhi ya ahadi hazijagushwa kwa namna yoyote ile.
Wakati wa kampeni, Rais Dk. Magufuli aliahidi kuundwa kwa mahakama ya kushughulikia kesi kubwa za ufisadi na rushwa ndani ya siku 100 za uongozi wake. Ahadi hiyo ilionyesha dhahiri jitihada zake za kupambana na rushwa kubwa, ambazo zimechangia kudidimiza uchumi wa nchi.
Akizungumza na majaji na wanasheria katika maadhimisho ya mwaka mpya wa Mahakama nchini wiki iliyopita, alimtaka Jaji Mkuu, Othuman Chande, kuharakisha uundwaji wa mahakama hiyo ili kesi husika zishughulikiwe na kuhukumiwa haraka.“Hakuna haja ya kusubiri Bunge ndipo mahakama hiyo iundwe, ianzishwe kama ilivyo Mahakama ya Ardhi na Biashara. Nakuomba Jaji Mkuu kuhakikisha mahakama hii inaanza haraka na kuanza kazi,” alisema.
MIKOPO YA MILIONI 50/-
Wakati wa kampeni, pia alihaidi kutoa mikopo ya Sh. milioni 50 kila kijiji ili kusaidia vikundi vya wajasiliamali kujikwamua kiuchumi.
Hata hivyo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, wakati anasoma mwelekeo wa bajeti ya serikali ya mwaka 2016/17 hivi karibuni Bungeni, mjini Dodoma, hakugusia fedha hizo kama zitakuwapo katika mpango wa serikali.
Kadhalika, ahadi ya kumaliza tatizo la ukosefu wa vitanda vya wagonjwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), nayo imeshindwa kumalizwa, baada ya juzi Rais Magufuli kufika MHN na kukuta hali ikiwa mbaya kwa wagonjwa kulala chini.
Pia aliahidi kumaliza tatizo la wanafunzi wa elimu ya juu kukosa mikopo, mamalishe hawabugudhiwi, kusimamia haki za wasanii.
Nyingine ni ujenzi wa zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya na rufani katika mikoa yote nchini na kuongeza ajira.
Kuwapo kwa umeme wa uhakika ni ahadi nyingine. Aliahidi wananchi kuunganishiwa umeme kwa wakati, wafanyabiashara wadogo na wakubwa kulipa kodi, kuendeleza kilimo, mifugo, uchimbaji madini.
Ahadi nyingine ni kuhakikisha upatikanaji wa majisafi na salama kwa vijijini asilimia 85 na mjini asilimia 95, kurejesha viwanda vilivyohodhiwa na wawekezaji na kutoviendeleza, ujenzi wa viwanda vidogo, vya kati na vikubwa.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment