Hakuna kifungu chochote cha Katiba ya Zanzibar au Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar kinachotoa uwezo kwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar na hata kwa Tume yenyewe kufuta uchaguzi au kuitisha uchaguzi wa marudio.
Kauli ya Waziri mwenye Dhamana
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, January Makamba aliliripotiwa kusema haya kuhusiana na uhalali wa kufutwa kwa uchaguzi wa Zanzibar:
“Hakuna mwenye uhalali kikatiba wala mahakama yoyote inayoweza kupingana na Tume kwa kuwa Katiba ya Zanzibar imeipa meno ya kufanya hayo ambayo yalifanyika,” alisema Makamba.Na kwamba, uchaguzi huo ulifutwa kwa kutumia Katiba ya Zanzibar Ibara ya 119 inayoipa Tume, (ZEC), uhuru mkubwa wa kuamua, pamoja na Sheria Namba 5 ya Uchaguzi ya Zanzibar ambayo inampa mwenyekiti mamlaka ya kufuta uchaguzi kama ataona kuna dosari. Alitaja dosari nane ambazo ni pamoja na malalamiko kutoka kwa vyama vilivyoshiriki uchaguzi huo pamoja na mmoja wa wagombea kujitangazia matokeo.
Hivyo basi, kulingana na kile ambacho kimetangulia kuelezwa hapo juu. Kwanza kabisa, kwa mujibu wa Ibara ya 7(1)-(4) ya Katiba ya Zanzibar ili uchaguzi utambulike kuwa ni halali, ni lazima kanuni, vigezo na masharti yote yaliyoelekezwa na Ibara husika tangulia kutajwa hapo yatimizwe kwa ukamilifu wake. Hii ikiwa na maana kwamba, ili uchaguzi uhesabike/kutambulika ni halali ni lazima uwe ulifanyika kwa kuzingatia na kufuata kanuni na taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa Sheria. Tofauti na hapo, uchaguzi huo utahesabika kuwa ni batili na si vinginevyo.
Dhana hii pia inaweza kuonekana kupitia Kifungu cha 39(1)-(3) cha Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar.
Na kama haitoshi, kwa mujibu wa Ibara ya 28 ya Katiba ya Zanzibar. Ili kupata tafasiri sahihi ni lazima masharti ya Ibara husika yatazamwe kwa upana wake bila ya kuyatenganisha, lengo na dhumuni likiwa ni kupata tafasiri sahihi ya uwepo wa Ibara yenyewe katika Katiba ya Zanzibar.
Kwa kuanza na sharti la kwanza linalosema: kutoka Ibara ndogo ya kwanza (1), ... mtu ataendelea kuwa Rais mpaka Rais anayefuata atakapo kula kiapo cha kuwa Rais wa Zanzibar. Na ile Ibara ndogo ya pili (2), ambayo inasema: Kufuatana na maelezo ya kijifungu (1) cha kifungu cha 28, Rais ataacha madaraka yake mara baada ya kumalizika miaka mitano...
Muhimu: Uwepo wa maneno: "kufuatana na maelezo ya kijifungu (1) cha kifungu cha 28..." inaonyesha dhahiri kwamba, ili kupata tafasri sahihi ya Ibara husika ni lazima masharti yote toka Ibara zote ndogo mbili yasomwe kwa pamoja.
Sanjari na Ibara ya 31(1) ..., mtu anayechukua Madaraka ya Urais, kabla ya kuanza wadhifa huo, atakula kiapo cha uaminifu na kiapo cha kazi kama kitavyowekwa na Baraza la Wawakilishi....
Kwa kulingana na tafasri inayopatikana hapa, ni kweli kabisa Dk. Ally Mohamed Shein toka ale kiapo cha uaminifu na kiapo cha kazi mwaka 2010 tayari miaka mitano imeshapita. Hii ni kwa mujibu wa Ibara ndogo ya pili (2). Lakini, kwa mujibu wa Ibara ndogo ya kwanza (1), Dk. Shein anapata uhalali wa kuendelea kuiongoza Zanzibar. Hii ni kutokana ukweli kwamba, mara baada ya Tume, (ZEC), kufuta uchaguzi wa Zanzibar uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana, hali hiyo imepelekea kutofanyika zoezi lolote la kiapo cha uaminifu na kiapo cha kazi anachotakiwa kuchukua/kula mshindi wa uchaguzi wa Rais kwa mujibu wa sheria.
Vile vile, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, (ZEC), kwa mujibu wa Ibara ya 119(9) ya Katiba ya Zanzibar, kwa madhumuni ya utekelezaji bora wa majukumu yake, itakuwa ni Idara inayojitegemea na mtendaji mkuu wake atakuwa ni Mkurugenzi wa Uchaguzi ambaye atateuliwa na kufanya kazi kwa mujibu wa masharti ya Sheria iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi.
Halikadhalika, kwa mujibu wa Kifungu cha 38(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar, (The Zanzibar Election Act of 1984), inaipa mamlaka kamili Tume, (ZEC), ya kuteua siku itakayofanyika uchaguzi wa Rais kwa majimbo yote. Na tena haishii hapo tu.
Kwa mujibu wa Kifungu chake kidogo cha pili (2): Tume, (ZEC), inaweza kupanga siku tofauti ya kufanyika kwa uchaguzi wa Rais kwa majimbo tofauti na hata inapobidi kutengua maamuzi yake, yenyewe, kuhusiana na uteuzi wa siku ya kufanya uchaguzi wa Rais na kisha kupanga siku nyingine tofauti na ile ya awali.
Kwa mantiki hiyo basi, kama Sheria inaipa mamlaka Tume, (ZEC), kuwa huru na kufanya kazi zake kwa kuzingatia masharti ya Sheria iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi, yakiwemo na mamlaka ya kupanga siku ya uchaguzi wa Rais katika mazingira yote tuliyotangulia kuyaona hapo awali, hiyo dhana iliyojengwa ya kuwepo "ukakasi wa kisheria" uliopelekea ujenzi wa hoja kwamba: "Hakuna kifungu chochote cha Katiba ya Zanzibar au Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar kinachotoa uwezo kwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar na hata kwa Tume yenyewe kufuta uchaguzi au kuitisha uchaguzi wa marudio" ni dhahiri haina tija kwa mujibu wa Sheria kama inavyoendelea kudaiwa.
Kwani kama Tume, (ZEC), ina mamlaka ya kutengua maamuzi yake, yenyewe, kuhusiana na uteuzi wa siku ya kufanya uchaguzi wa Rais na kisha kupanga siku nyingine tofauti na ile ya awali kwa ngazi ya majimbo, kivipi basi ishindwe kufuta uchaguzi wote kwa Zanzibar nzima?!
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment