Dar esa Salaam. Ndani ya siku 100 za utawala wa Rais John Magufuli, takribani nusu ya Watanzania hawajaridhiki na namna alivyoshughulika mzozo wa kisiasa unaoendelea visiwani Zanzibar, kwa mujibu wa utafiti.
Pamoja na mambo mengi mazuri ambayo mpaka sasa Serikali ya Awamu ya Tano imeyafanya, bado wananchi wanaona haijashughulikia vya kutosha mgogoro huo uliotokana na kufutwa kwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu mwaka jana.
Mgogoro huo uliibuka baada ya mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salim Jecha kufuta matokeo ya uchaguzi huo wa rais, wawakilishi na madiwani na kutangaza kuwa utarudiwa Machi 20, jambo ambalo CUF imelipinga.
Wakati Jecha akitangaza uamuzi huo, tayari matokeo ya majimbo 31 yalikwisha kutangazwa wakati majimbo mengine tisa yalihakikiwa, huku washindi wa uwakilishi na udiwani walitangazwa na kupewa hati za ushindi.
Katika utafiti uliofanywa na InfoTrak Research & Consulting ya Kenya kwa kushirikiana na Midas Touché East Africa ya hapa nchini kwa ufadhili wa Mwananchi Communications Ltd wachapishaji wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti, kupima utendaji wa Rais Magufuli kwa siku 100 za kwanza, wananchi wameonyeshwa kutoridhika na suala la Zanzibar.
Utafiti huo uliowashirikisha wananchi 1,200 kutoka Bara na Zanzibar, unaonyesha kuwa asilimia 48.8 ya waliohojiwa walisema Rais hajachukua hatua kushghulikia mgogoro huo, asilimia 34.4 walisema amefanya vyema wakati asilimia 16.8 hawajui kinachoendelea.
Katika utafiti huo uliofanyika kati ya Februari 1 na Februari 7, washiriki kutoka ngazi ya familia wenye zaidi ya miaka 18 waliulizwa: “Kwa maoni yako, unadhani Rais John Magufuli ameushughulikia ipasavyo mgogoro wa Zanzibar?”
Washiriki walipatikana kutoka Kanda ya Kati yenye mikoa ya Dodoma na Tabora (144), Kanda ya Mashariki (Dar, Morogoro na Mtwara, watu 303), Kanda ya Ziwa (Mwanza, Mara, Kagera na Kigoma, 335); Kanda ya Kaskazini (Arusha na Tanga, watu 188), Kanda ya Kusini (Mbeya na Ruvuma, watu 194) na Zanzibar (Kaskazini Unguja na Mjini Magharibi watu, 36).
Matokeo ya utafiti huo yanalingana na maoni ya wadau ambao wamekuwa wakimtaka Rais Magufuli aingilie kati mgogoro huo na kuumaliza badala ya kwenda kwenye marudio ya uchaguzi bila ya maridhiano.
Tayari CUF imetangaza kujitoa kwenye uchaguzi huo baada ya vikao tisa baina yake na Rais Ali Mohamed Shein kukosa ufumbuzi.
Huo ni utafiti wa kwanza kuchapishwa tangu Rais Magufuli aingie madarakani na kutoa maoni ya wananchi juu ya masuala mbalimbali hasa mzozo huu. Awali, umoja wa mabalozi wa nchi za Ulaya uliwahi kutoa msimamo wake juu ya kupinga marudio ya uchaguo huo.
No comments :
Post a Comment