RAIS Dk. John Magufuli leo anatimiza siku 100 tangu alipoapishwa kushika wadhifa huo Novemba 5, mwaka jana.
Tangu aingie madarakani, ametawala vichwa vya habari kwa hatua kadhaa alizochukua ikiwamo kupasua majipu na kubana matumizi, mambo ambayo ndiyo sifa yake kubwa.
Rais Magufuli aliingia madaraka baada ya kushinda Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, akitumia kaulimbiu ya ‘Hapa kazi tu’.
Akiwa katika kampeni za uchaguzi huo, Rais Magufuli alitoa ahadi nyingi, huku akisisitiza kuanza kuzifanyia kazi mara moja akiingia Ikulu.
Miongoni mwa ahadi zake ambazo tayari amezifanyia kazi ni kutoa elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne, ingawa kumekuwa na changamoto kubwa katika utekelezaji wake.
Katika utekelezaji wa ahadi hii, pamoja na mambo mengine, kumekuwa na malalamiko mengi kuhusu kupunjwa ruzuku kwa baadhi ya shule, hali inayoweza kusababisha kutofikiwa malengo yaliyokusudiwa.
SIKU ZA MWANZO
Mara tu baada ya kuapishwa, Rais Magufuli alianza kazi kwa kumteua mwanasheria mkuu wa Serikali, George Masaju.
Katika siku zake hizo za mwanzo, alitumia mtindo wa kufanya ziara za kushtukiza katika taasisi mbalimbali za Serikali pamoja na kukemea viongozi wazembe na wanaoendekeza ufisadi na rushwa serikalini.
Mtindo wake huo, ukatumiwa pia na watendaji wengine wa Serikali wakiwamo mawaziri na wakuu wa mikoa na wengine.
Katika siku zake hizo za mwanzo, Rais Magufuli pia alifanya mabadiliko makubwa Ikulu kwa kufuta baadhi ya vitengo, kikiwamo cha lishe na benchi la wageni na kuagiza wananchi wote wenye matatizo waanzie ngazi za chini.
AWEKA MSIMAMO
Novemba 7, mwaka jana akiwa Ikulu, Dar es Salaam, alikutana na watumishi wa Serikali ikiwa ni pamoja na manaibu katibu wakuu, manaibu wakuu na watendaji wakuu wa Serikali.
Katika kikao hicho, aliwataka kujiandaa kufanya kazi kwa ufanisi katika Serikali ya awamu ya tano chini yake. huku akiwasisitiza juu ya dhamira yake ya kuendeleza kaulimbiu yake ya “Hapa kazi tu”.
Kikao hicho pia kiliudhuriwa na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu na aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Rished Bade ambapo alitoa mwelekeo wa Serikali anayoitaka.
AFUTA SAFARI ZA NJE
Rais Magufuli alitumia kikao hicho kutangaza kufuta safari zote za nje ya nchi hadi hapo atakapolitolea suala hilo uamuzi mwingine, na kueleza shughuli zote zinazotakiwa kufanywa nje ya nchi zifanywe na kusimamiwa na mabalozi wa Tanzania wanaowakilisha nchi.
Alisema mtumishi atasafiri nje iwapo kutatokea jambo la dharura, na lazima kibali kitolewe na yeye, Katibu Mkuu Kiongozi au Makamu wa Rais.
Alisema mtumishi atasafiri nje iwapo kutatokea jambo la dharura, na lazima kibali kitolewe na yeye, Katibu Mkuu Kiongozi au Makamu wa Rais.
Badala yake aliwataka watendaji hao kufanya zaidi ziara za kwenda vijijini ili kuzijua na kutatua kero za wananchi.
Hadi sasa, Rais Magufuli bado hajakwenda safari yoyote ya nje ya nchi zaidi ya kuwatuma Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwenda kumwakilisha kwenye shughuli mbili tofauti.
SAFARI NDANI YA NCHI
Novemba 20, mwaka jana, Rais Magufuli alisafiri kwa mara ya kwanza nje ya Dar es Salaam alipokwenda mkoani Dodoma ambako alifungua Bunge la 11.
Katika mkutano wake, Rais Magufuli alijikuta akisusiwa hotuba yake na wabunge wa upinzani waliokuwa wakipinga uteuzi wake na kutomtambua Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein kama rais halali, baada ya kufutwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar.
Januari 12, mwaka huu, Rais Magufuli alisafiri kwa ndege ya kukodi kwenda Zanzibar ambako alihudhuria maadhimisho ya miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Januari 21, mwaka huu alifanya ziara ya kwanza mkoani Arusha, ambako alikwenda pia katika Chuo cha Maofisa wa Kijeshi (TMA) Monduli kutunuku vyeo askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) baada ya kuhitimu mafunzo, huku naye akiwa amevalia sare za jeshi hilo.
Februari 5, mwaka huu pia Rais Magufuli alisafiri kwa gari kutoka Dar es Salaam kwenda mkoani Singida kuhudhuria maadhimisho ya miaka 39 ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
WALIOKIUKA AMRI YA KUTOSAFIRI NJE WATIMULIWA
Katika kile kinachoonekana kuwa hatanii, Rais Magufuli aliagiza kusimamishwa kazi mara moja kwa watumishi waandamizi wanne wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ambao walikaidi agizo lake la kuwataka watumishi wa umma kutosafiri nje ya nchi.
Watumishi hao ni Mary Mosha, Ekwabi Mujungu, Doreen Kapwani na Rukia Nikitas ambao walisafiri kwenda nje ya nchi, licha ya kutokuwa na kibali cha safari kutoka kwa Rais ama Katibu Mkuu Kiongozi.
MAJIPU
Katika hotuba yake ya kuzindua Bunge la 11, Novemba mwaka jana, Rais Magufuli alisema atatumbua majipu, akimaanisha kupambana na ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma unaofanywa na watumishi wa umma.
Kauli hiyo ilionekana ‘kuianika’ Serikali iliyopita na kuibua mjadala mkubwa miongoni mwa wafuatiliaji wa masuala ya siasa nchini.
Rais Magufuli alitolea mfano wa namna safari za vigogo nje ya nchi zinavyoligharimu taifa ambapo alisema katika mwaka wa fedha wa 2013/14 na 2014/15 peke yake, zilitumika Sh bilioni 356.324 kugharimia safari hizo.
Kwa maelezo yake, kiasi hicho kingetosha kujenga barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 400 na kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwamo ya maji, elimu na afya.
Alisema mgawanyo wa matumizi ya fedha hizo ulikuwa ni tiketi za ndege (air ticket) Sh bilioni 183.160, mafunzo nje ya nchi Sh bilioni 68.612 na posho za kujikimu (perdiem foreign) Sh bilioni 104.552.
Alizitaja wizara na taasisi za umma zilizoongoza kwa kutumia fedha nyingi kwa ajili ya safari za nje ya nchi, kuwa ni Bunge, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikano wa Kimataifa, Wizara ya Fedha, Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali (NAOT) na Wizara ya Mambo ya Ndani.
Katika siku zake 100 za kwanza tangu alipoingia madarakani, tayari Serikali yake imewafukuza kazi vigogo zaidi ya 70 kwa tuhuma mbalimbali ikiwamo za ufisadi.
Rais Magufuli aliwang’oa vigogo wapatao 23 wa Mamkala ya Bandari (TPA) na kuvunja Bodi ya Wakurugenzi ya mamlaka hiyo kutokana na upotevu wa makontena.
Bodi hiyo ilikuwa na vigogo kadhaa akiwamo Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson na Mkurugenzi wa zamani wa Mamlaka ya Udhibiti ya Nishati na Maji (EWURA), Haruna Masebu.
Hatua ya kuvunjwa kwa bodi hiyo, ilitokana na kushindwa kuisimamia vyema Bandari ya Dar es Salaam, hali iliyosababisha makontena 2,716 kutolewa bandarani bila kulipia kodi na kuisababishia Serikali hasara ya mabilioni ya shilingi.
Uamuzi huo ulitangazwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa niaba yake, ambapo alisema pia Rais Magufuli ametengua uteuzi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk. Shaban Mwinjaka kutokana na ubadhirifu wa Sh bilioni 16 ndani ya Shirika la Reli Tanzania (TRL).
Sambamba na hilo, Waziri Mkuu Majaliwa alisema maofisa 12 wa TPA waliokuwa wakisimamia bandari kavu (ICD) pia walisimamishwa kazi na kuamuru wawekwe chini ya ulinzi ili wasaidie kujua wamiliki wa makontena hayo na gharama yake.
Alisema hatua hizo kwa upande wa TPA zimechukuliwa kutokana na madudu yaliyobainika, baada ya ziara alizofanya kwenye taasisi hiyo Novemba 27, mwaka jana ambapo alibaini upotevu wa kontena 329 na ile ya Desemba 4, mwaka huohuo iliyobaini upotevu wa kontena 2,387.
JIPU LA RAHCO
Rais Magufuli pia alimsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (RAHCO), Mhandisi Benhadard Tito.
Uamuzi huo ulilenga kupisha uchunguzi wa kina kutokana na ukiukwaji mkubwa wa taratibu za manunuzi uliobainika katika mchakato wa utoaji wa zabuni ya ujenzi wa reli ya kati.
Rais Magufuli alichukua uamuzi huo baada ya kuitisha kikao cha wataalamu kutoka wizara na taasisi mbalimbali za Serikali.
Taasisi hizo ni zile zinazohusika katika utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa yaani ‘Standard Gauge’.
Pamoja na kumsimamisha kazi mkurugenzi huyo, pia alivunja Bodi ya RAHCO baada ya kujiridhisha kuwa haikutekeleza ipasavyo wajibu wake wa kusimamia mchakato wa zabuni hiyo badala yake imeonekana kutetea kilichofanyika.
Alimtaka Mkurugenzi Mkuu wa RAHCO, Mhandisi Tito kutoa ushirikiano kwa vyombo vya Serikali ambavyo vitafanya uchunguzi zaidi kuhusu mchakato wa zabuni hiyo.
Aliiagiza Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) kuchunguza na kuchukua hatua dhidi ya kampuni za ukandarasi zilizopewa zabuni ya ujenzi huo kama itathibitika zimeshiriki katika ukiukwaji wa sheria.
Rais Magufuli alitangaza kuivunja Bodi ya Mamlaka ya Reli Tanzania (TRL) kutokana na kutoridhishwa na jinsi ilivyoshughulikia ripoti ya uchunguzi juu ya mchakato wa ununuzi wa mabehewa ya treni.
JIPU LA TAKUKURU
Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk. Edward Hosea, Desemba 16, mwaka jana.
Akizungumzia uamuzi huo, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alisema ulichukuliwa baada ya Rais Magufuli kutoridhishwa na namna taasisi hiyo ilivyokuwa ikitekeleza wajibu wake katika kukabiliana na rushwa, hususani kwenye upotevu wa mapato ya Serikali katika bandari ya Dar es Salaam.
Alisema Rais Magufuli alijiridhisha kwamba utendaji kazi wa Dk. Hosea usingeendana na kasi yake, hivyo alimteua aliyekuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Valentino Mlowola kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo.
JIPU LA NIDA
Januari 26, mwaka huu Rais Magufuli alitangaza kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dickson Maimu ili kupisha uchunguzi dhidi yake.
Maimu alisimamishwa pamoja na maofisa wengine wanne wa NIDA kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za Serikali.
Maofisa hao ni Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Joseph Makani, Ofisa Ugavi Mkuu, Rahel Mapande, Mkurugenzi wa Sheria, Sabrina Nyoni na Ofisa Usafirishaji, George Ntalima.
Balozi Sefue alisema taarifa zilizomfikia Rais Magufuli zinaonyesha kuwa NIDA hadi wakati huo ilikuwa imetumia Sh bilioni 179.6 kiasi ambacho ni kikubwa.
Alisema Rais Magufuli angependa ufanyike uchunguzi na ukaguzi jinsi fedha hizo zilivyotumika, maana amekuwa akipokea malalamiko ya wananchi kuhusu kasi ndogo ya utoaji wa vitambulisho hivyo.
Rais pia alielekeza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) afanye ukaguzi maalumu wa hesabu za NIDA, ikiwamo ukaguzi wa “value for money” baada ya kuthibitisha idadi halisi ya vitambulisho vilivyotolewa hadi sasa.
Pia aliitaka Takukuru ifanye uchunguzi kujiridhisha kama kulikuwa na vitendo vya rushwa au la.
MATUMIZI YA SERIKALI
Novemba 9, mwaka jana, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Sefue, alitangaza kuwa Rais Magufuli aliamua kufuta shamrashamra za Sikukuu ya Uhuru na kwamba fedha zitakazookolewa atazipeleka sehemu nyingine.
Hiyo ilitafsiriwa kuwa miongoni mwa hatua ambazo Rais Magufuli aliamua kuzichukua ili kubana matumizi ya Serikali kwa nia ya kupata fedha za kupeleka maendeleo kwa wananchi.
Fedha hizo kiasi cha Sh. bil. 4 zilielekezwa kwenye mradi wa upanuzi wa barabara ya Mwenge.
MAWAZIRI
Desemba 10, mwaka jana, Rais Magufuli alitangaza baraza lake la mawaziri ambalo alianza kwa kuteua mawaziri 19, ingawa wizara ni 18. Mawaziri sita kati ya hao ni wanawake.
Katika uteuzi wake, aliacha wazi nafasi nne za uwaziri kwa madai alikuwa akitafuta watu watakaofaa kuteuliwa kuongoza wizara husika.
Wizara ambazo hakuteua mawaziri katika baraza lake la awali alilolitangaza ni Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Wizara ya Maliasili na Utalii.
Desemba 23, mwaka jana ikiwa ni siku 13 tangu alipotangaza Baraza la Mawaziri, Rais Magufuli alikamilisha baraza lake kwa kuwataja mawaziri wanne waliokuwa wamebakia.
SERIKALI YA WASOMI
Uteuzi wa Rais Magufuli umekuwa wa tofauti ambapo viongozi wengi aliowateua kushika nafasi mbalimbali ni wasomi wa ngazi ya uprofesa na udaktari.
Kwa mfano, Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi inaongozwa na Profesa Joyce Ndalichako, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa na Wizara ya Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe.
Aidha Wizara ya Katiba na Sheria inaongozwa na Dk. Harrison Mwakyembe, Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk. Augustino Mahiga na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi.
MAKATIBU NA MANAIBU WAO
Katika mwendelezo wa kuhakikisha kuwa wale anaowateua wanakubaliana na kasi yake, Rais Magufuli aliwapa kiapo cha utii makatibu wakuu wa wizara na manaibu wao.
Akiwaapisha kiapo hicho aliwaeleza wazi kwamba yule atakayeshindwa kufanya kazi ni bora ajiondoe mwenyewe na kupisha wengine watumikie wananchi.
AWARUDISHA NYUMBANI MABALOZI ‘MIZIGO’
Katika utaratibu wake, Rais Magufuli aliiagiza Wizara ya Mambo ya Nje, Afrika Mashariki na Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa kuwarejesha nyumbani mara moja mabalozi wawili ambao mikataba yao ilikuwa imemalizika.
Mabalozi hao, Batilda Buriani aliyekuwa Japan na Dk. James Msekela aliyekuwa Italia walitakiwa kukabidhi kazi kwa ofisa mkuu au mwandamizi aliye chini yao.
Pia alimrejesha nyumbani Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Peter Kallaghe na kuagiza Wizara ya Mambo ya Nje, Afrika Mashariki na Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa kumpangia kazi nyingine.
MGOGORO WA ZANZIBAR
Pamoja na yote, suala la kufutwa kwa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar limekuwa likiitesa Serikali ya Rais Magufuli.
Wakati Chama Cha Mapinduzi kikitaka uchaguzi huo urudiwe, Chama cha Wananchi (CUF) kimeendelea kushikilia msimamo wake kuwa hakitakubali marudio ya uchaguzi huo na hakitashiriki.
CUF wanaamini Rais Magufuli pekee ndiye anayeweza kumaliza mzozo huo ulioibuka visiwani humo, lakini kiongozi huyo hajazungumza lolote hadi hivi sasa tangu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha alipotangaza kufutwa na kurudiwa kwa uchaguzi huo.
Kuendelea kuwako kwa mgogoro huo, ni wazi kwamba kunaitia doa Serikali ya Dk. Magufuli nje ya nchi.
GUMZO DUNIANI
Kutokana na kasi yake ya mabadiliko ya kweli ya uongozi wake, hasa kudhibiti matumizi na kuelekeza fedha katika huduma za kijamii, Rais Magufuli amekuwa gumzo kwenye anga za kimataifa.
Uongozi wake umeelezwa kuwa wa mfano, kwani miongoni mwa mambo anayoyafanya, yanagusa ulimwengu na anatekeleza yote bila kufanya safari yoyote ya nje ya nchi kama wanavyofanya viongozi wengine.
Tangu aingie madakarani, amedhibiti mabilioni ya fedha na kuzielekeza katika kuboresha huduma za afya, ikiwamo kuongeza upatikanaji wa dawa za kupunguza makali ya Ukimwi (ARV’s), ruzuku ya shule na miundombinu ya barabara.
Gazeti la The Sunday Independent, miongoni mwa vyombo vya habari vyenye nguvu nchini Afrika Kusini, liliandika katika moja ya tahariri zake kwamba “Afrika ifuate mfano wa Tanzania”.
Tangu aingie madakarani, amedhibiti mabilioni ya fedha na kuzielekeza katika kuboresha huduma za afya, ikiwamo kuongeza upatikanaji wa dawa za kupunguza makali ya Ukimwi (ARV’s), ruzuku ya shule na miundombinu ya barabara.
Gazeti la The Sunday Independent, miongoni mwa vyombo vya habari vyenye nguvu nchini Afrika Kusini, liliandika katika moja ya tahariri zake kwamba “Afrika ifuate mfano wa Tanzania”.
Tahariri hiyo ilisisitiza kuwa utekelezaji wa maazimio ya mkutano wa sita wa mawaziri wa Baraza la Ushirikiano kati ya Afrika na China (FOCAC), unahitaji rais kama Magufuli ambaye ameonyesha kwa dhati nidhamu katika matumizi ya Serikali.
Gazeti hilo limekuwa miongoni mwa vyombo vya habari vinavyosifu utendaji wa Rais Magufuli, ambaye alifanya kazi bila Baraza la Mawaziri kwa zaidi ya siku 30 tangu aapishwe.
Gazeti hilo limekuwa miongoni mwa vyombo vya habari vinavyosifu utendaji wa Rais Magufuli, ambaye alifanya kazi bila Baraza la Mawaziri kwa zaidi ya siku 30 tangu aapishwe.
Baadhi ya waandishi wa habari kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika, walilieleza gazeti dada la The Sunday Independent, Daily News katika siku ya mwisho ya mkutano wa FOCAC kwamba wameguswa kwa utendaji wa Dk. Magufuli na kuwataka viongozi wengine wa Afrika kuiga.
Mwandishi wa gazeti la Daily Graphic la Ghana, Emmanuel Adu- Gyamerah, alisema kazi anayofanya Dk. Magufuli, ikiwamo kubadili sherehe za Uhuru ambazo mataifa mengi huzifanya kwa gharama kubwa, ni jambo ambalo viongozi wengi wa Afrika wameshindwa, lakini yeye amefanya kwa muda mfupi tangu aingie madarakani.
Mwandishi wa gazeti la Daily Graphic la Ghana, Emmanuel Adu- Gyamerah, alisema kazi anayofanya Dk. Magufuli, ikiwamo kubadili sherehe za Uhuru ambazo mataifa mengi huzifanya kwa gharama kubwa, ni jambo ambalo viongozi wengi wa Afrika wameshindwa, lakini yeye amefanya kwa muda mfupi tangu aingie madarakani.
“Hii hatua ya kupunguza matumizi inapaswa kufanywa na Waghana pia,” alisema Adu-Gyamerah.
Rais Magufuli alibadili namna ya kusherehekea Sikukuu ya Uhuru kwa kuagiza Watanzania wote wafanye usafi katika maeneo yao ya kazi na makazi ili kupambana na magonjwa ya mlipuko, ikiwamo kipindupindu na kutunza mazingira.
Rais Magufuli alibadili namna ya kusherehekea Sikukuu ya Uhuru kwa kuagiza Watanzania wote wafanye usafi katika maeneo yao ya kazi na makazi ili kupambana na magonjwa ya mlipuko, ikiwamo kipindupindu na kutunza mazingira.
Baadhi ya wananchi wa Rwanda, walieleza kuwa hatua aliyochukua Rais Magufuli kuhusu sherehe za Uhuru ni “ya Kinyarwanda” kwa kuwa kwao Serikali ilifanya Jumamosi ya kwanza ya kila mwezi kuwa siku rasmi ya usafi nchi nzima.
Mtangazaji wa Televisheni ya China (CCTV) kutoka nchini Kenya, alisema kufuta safari za nje ni moja ya hatua muhimu.
Mtangazaji wa Televisheni ya China (CCTV) kutoka nchini Kenya, alisema kufuta safari za nje ni moja ya hatua muhimu.
Alisema Wakenya wamekuwa wakizungumzia safari za Rais wao, Uhuru Kenyatta anazofanya nje ya nchi.
Gazeti la mtandaoni la Nigeria, Naij.com, lilieleza hatua ya Dk. Magufuli ya kupunguza matumizi ni ya kuchukuliwa na Serikali ya Nigeria vilevile.
Gazeti la mtandaoni la Nigeria, Naij.com, lilieleza hatua ya Dk. Magufuli ya kupunguza matumizi ni ya kuchukuliwa na Serikali ya Nigeria vilevile.
Naij.com ilimnukuu mhariri wake, Abang Mercy akiandika katika ukurasa wa Twitter kwamba kinachofanywa na Dk. Magufuli anakitarajiwa kufanywa pia na rais wao.
“Tangu achaguliwe, Rais wa Tanzania, John Magufuli ametekeleza mabadiliko makubwa; na ndivyo ninavyotarajia kwa Rais Buhari (Rais wa Nigeria),” aliandika.
Naij.com ilimfananisha Rais Magufuli na Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, mwasisi na mtu asiyekwepeka katika historia ya Tanzania.
Naij.com ilimfananisha Rais Magufuli na Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, mwasisi na mtu asiyekwepeka katika historia ya Tanzania.
Nalo gazeti la Daily Nation la Kenya, liliripoti kuwa hatua ya Rais Magufuli kuzuia safari za nje, inapaswa kuchukuliwa pia nchini mwao, hasa kutokana na wananchi kuonyesha kutokupendezwa na safari za Rais Kenyatta nje ya nchi.
Aidha, suala la kupunguza matumizi kwa kuzuia kuchapisha kadi za sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya kwa taasisi na mashirika ya umma, limepongezwa pia na kumtaka Kenyatta kuiga mfano huo.
Aidha, suala la kupunguza matumizi kwa kuzuia kuchapisha kadi za sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya kwa taasisi na mashirika ya umma, limepongezwa pia na kumtaka Kenyatta kuiga mfano huo.
/Mtanzania.
No comments :
Post a Comment