Sh 179 bilioni: Gawio lililotokana na kazi zinazofanywa na kampuni tanzu za ABG PLC
Dar es Salaam. Baraza la Rufaa za Kodi (TRAT), limeibana Kampuni ya Madini ya African Barrick Gold Plc (kwa sasa Acacia) baada ya kuridhika kuwa ilijenga mazingira ya kukwepa kodi ya Dola za Marekani 41,250,426 (Sh89 bilioni) kwa kipindi cha miaka minne mfululizo.
Fedha hizo zilizopaswa kulipwa na ABG kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kama kodi ya zuio katika kipindi hicho, lakini ikakata rufaa kupinga kodi hiyo na baraza hilo kuipa haki TRA.
Katika uamuzi huo uliotolewa Machi 31, mwaka huu na Mwenyekiti wa TRAT, Jaji Dk Fauz Twaib, baraza hilo limekubaliana na hukumu ya Baraza la Rufaa za Kodi nchini (TRAB) na hoja za TRA kuwa ABG imekuwa ikifanya mchezo wa kukwepa kodi.
Kwa mujibu wa hukumu hiyo, ABG ilikwepa kulipa kodi hiyo kuanzia 2010 hadi 2013 kwa namna mbili, kwanza ikiwa ni kudai kuwa kampuni tatu zilizo chini yake zinazojishughulisha na uchimbaji wa madini nchini zimekuwa zikipata hasara.
Kampuni hizo ni Bulyanhulu Gold Mining Ltd, inayomiliki mgodi wa Bulyanhulu, North Mara Mining Ltd na Pangea Minerals Ltd, inayomiliki migodi ya Buzwagi na Tulawaka.
Hata hivyo, wakati kampuni hizo zikidai kuwa zilikuwa zikipata hasara, baadaye ilibainika kuwa kampuni mama ya ABG PLC, yenye makao yake makuu jijini London, Uingereza katika vipindi hivyo, ilikuwa ikitangaza kutoa gawio kwa wanahisa wake.
Gawio hilo lilitokana na mapato yaliyopatikana kutoka na shughuli zake nchini za uchimbaji madini, ambayo katika kipindi hicho cha miaka minne yalifikia Dola 818,431,285 za Marekani (Sh179 bilioni). Wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo katika ngazi ya Bodi, TRA iliwasilisha taarifa ambazo zilitolewa na ABG za mapato za kila mwaka kama kielelezo ambazo ilidai kuzipata katika upelelezi wake.
Taarifa hizo ambazo ni moja ya vigezo vilivyojenga msingi wa uamuzi wa TRAB na TRAT, zinaonyesha kuwa 2010, ABG ilitoa gawio kwa wanahisa wake la Dola 259,542,367 za Marekani.
Katika kiwango hicho, TRA ilionyesha kuwa ilitakiwa kulipwa kodi ya zuio la asimilia 10 ambayo ni Dola 25,954,237 za Marekani, wakati kwa mwaka 2011 ABG ilitoa gawio la Dola 28,295,899 na kodi ya zuio kwa TRA Dola 2,829,5809.
Mwaka 2012, gawio lilikuwa ni Dola 70,124,620 wakati kodi ya zuio ni Dola 7,012,462 na mwaka 2013, gawio lilikuwa Dola 54,541,371, ambapo kodi ya zuio ilikuwa Dola 5,454,137 za Marekani.
Katika hukumu yake, TRAT imeelezea kushangazwa na mwenendo wa AGB na kampuni zake zinazoendesha biashara ya uchimbaji madini kutangaza kupata hasara katika kipindi hicho wakati kampuni mama ambayo pato lake linatokana na shughuli za kampuni hizo, ikitangaza na kutoa gawio kwa wanahisa wake.
Baraza hilo linaeleza katika hukumu hiyo kuwa TRAB katika kesi ya msingi, ilibaini katika ukurasa wa 123 wa taarifa yake (ya fedha), AGB inaeleza kwamba pato lake lote linatokana na shughuli za madini zinazoendeshwa na kampuni zake ndogo nchini.
Linaendelea kueleza baraza hilo kuwa taarifa hiyo ya AGB haionyeshi mbali na migodi ya Tanzania, hakuna shughuli nyingine yoyote duniani kote inayoendeshwa na ABG ambayo huchangia pato hilo.
Baraza hilo lilisema kitendo cha kampuni zake zote ambazo ndizo chanzo cha mapato yake zikitangaza kupata hasara, kinamaanisha kuwa hakuna gawio la kulipa kwa wanahisa wake na hazijalipa kodi ya kampuni zake kwa miaka yote hiyo. “Kwa kweli tunaungana na Bodi (TRAB) kushangaa, kwamba hili linawezekana vipi. Ni jambo lisiloshawishi kwamba mrufani (ABG) aliweza kulipa gawio hilo wakati raslimali zake pekee ni kampuni tatu zinazopata hasara zilizoko Tanzania, ambazo hazipati faida kabisa na hazitoi gawio,” ilisema TRAT.
“Katika mazingira hayo ni sawa kuhitimisha hoja ya mjibu rufaa (Kamishna Mkuu wa TRA kupitia kwa Wakili wake, Noah Tito) kuwa miamala hiyo ni namna iliyotengenezwa na mrufani (ABG) kwa lengo la kukwepa kodi ilithibitika,” iliongeza TRAT katika uamuzi huo.
TRA baada ya kupitia vifungu mbalimbali vya sheria na hoja za pande zote, pia ilikubaliana na hoja za mamlaka hiyo pamoja na msimamo wa TRAB kwamba mrufani huyo ni kampuni mkazi nchini, hivyo anastahili kulipa kodi zote.
No comments :
Post a Comment