Daraja la Kigamboni
Dar es Salaam. Mradi mkubwa wa ujenzi wa mji mpya wa Kigamboni jijini Dar es Salaam uitwao Dege Eco Village, ulioanzishwa na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) umesimama huku ikiripotiwa kuwapo kwa ufisadi wa zaidi ya Sh179 bilioni katika mradi huo.
Mchoro wa mradi huo ulioanzishwa mwaka 2014 kwa gharama ya Dola za Marekani 653 milioni (Sh1.3 trilioni) unaonyesha utakapokamilika utachangia kubadili sura ya jiji la Dar es Salaam kwani kutakuwa na nyumba za kifahari, majengo ya hoteli, maduka makubwa, eneo la wazi la mapumziko, baa, shule, hospitali, kumbi za mikutano, nyumba za ibada na migahawa.
Hata hivyo, mradi huo unaosimamiwa na kampuni ya Hifadhi Builders Limited iliyoanzishwa na Bodi ya NSSF kwa ushirikiano na kampuni ya Azimio Housing Estate Limited (Ahel), huku wajenzi wakiwa kampuni ya M/s Mutluhan Construction Industry Company Limited kutoka Uturuki, huenda usikamilike kwa muda uliopangwa kwani umesimama tangu Januari, ingawa unadaiwa utaanza tena mwezi huu.
Ofisa mmoja mwandamizi wa Serikali ameliambia gazeti la Mwananchi kwamba ujenzi wa nyumba za Dege Eco Village ni miongoni mwa miradi ya kisasa ambayo NSSF imekaguliwa na kubainika kufisadi fedha baada ya kuingia mikataba bila kufuata taratibu, kanuni wala sheria za nchi.
Kwa mujibu wa ofisa huyo, ripoti ya ukaguzi iliyoishia Juni 2015, uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) akishirikiana na taasisi ya kimataifa ya ukaguzi ya Ernst and Young imeanika ufisadi mkubwa unaotishia usalama wa fedha za wanachama wa shirika hilo.
Mtoa habari huyo amesema mradi wa nyumba za kisasa wa Kigamboni unaojengwa katika ekari 300, unakabiliwa na kashfa baada ya kubainika kuwa NSSF imenunua ekari hizo kutoka kwa mbia mwenzake Azimio Housing Estate Limited kwa zaidi ya Sh800 milioni kwa ekari, wakati shirika hilo linamiliki viwanja vingine maeneo hayo vyenye thamani ya Sh4.5 milioni kwa ekari.
“Ukipata ripoti hiyo ya ukaguzi utaweza kuona ilivyochambua miradi mbalimbali ya ujenzi jijini Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Pwani na Mtwara. Kwa mfano mradi wa Arumeru mkoani Arusha, NSSF imenunua viwanja kutoka Azimio kwa Sh1.8 bilioni kwa kila ekari,” alieleza ofisa huyo.
Uchunguzi unaonyesha kwamba Bodi ya NSSF na Azimio walitiliana saini Novemba 15, 2013, kuhusu uendeshaji wa miradi mbalimbali. Azimio walijieleza kuwa wanamiliki ardhi yenye ukubwa wa ekari 20,000 Kigamboni, ekari 655.3 Arumeru, ekari 7,832.7 Pwani, ekari 200 Mwanza, ekari 5,723.6 Mtwara, na kwamba maeneo hayo yanafaa kwa ujenzi wa miji ya kisasa.
Taratibu ziliitaka NSSF kujiridhisha kuhusu uwepo wa ardhi hiyo, uhalali wa kisheria wa Azimio kumiliki eneo hilo pamoja na thamani halisi ya ardhi hiyo kutoka mamlaka zinazohusika. NSSF hawakufanya hivyo na wala hawakumshirikisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
“Napenda kukuthibitishia kwamba NSSF waliridhia bila ya kujiridhisha kuhusu uwapo wa ardhi hiyo bali walitiliana saini miradi ya pamoja kujenga nyumba Kigamboni na Arumeru bila kujiridhisha,” alisema ofisa huyo.
Mradi wa Kigamboni una thamani ya Dola za Marekani 653,436,675 (Sh1.3 trilioni), na mradi wa Arumeru thamani yake ni Dola 3,340,589,543 hadi utakapokamilika.
Tatizo jingine kubwa ni kuhusu umiliki wa mradi. Uchunguzi unaonyesha mkataba wa mradi huo uliitaka Azimio kuchangia asilimia 55 zikiwamo ekari 300 ambazo ni sawa na asilimia 20 ya mradi, huku NSSF ikichangia asilimia 45. Uchambuzi unaonyesha Azimio imetoa ekari 300 za Kigamboni kwa Dola 108,906,113, na ekari 655.3 za Arumeru kwa Dola 556,764,924.
Kwa hiyo kwa miradi miwili hiyo, NSSF ‘imenunua’ ardhi yenye thamani ya Dola 665,671,037 (Sh1.33 trilioni) kutoka Azimio.
Uchunguzi unaonyesha kuwa Serikali imekasirishwa na hatua ya taasisi hiyo ya umma ‘kununua’ ekari moja ya ardhi kwa zaidi ya Sh800 milioni huko Kigamboni, wakati bei halisi ya ardhi iliyotangazwa na Halmashauri ya Manispaa ya Temeke mwaka 2012 wakati ikiuza viwanja vyake ilikuwa Sh8, 000 kwa mita za mraba, kwa hiyo ekari moja ilikuwa Sh39 milioni.
Vilevile, NSSF yenyewe ilikuwa inamiliki ekari 267 Kigamboni ilizonunua kutoka kampuni ya Georgia Homes (T) Ltd kila moja kwa Sh4.5 milioni, hivyo hatua ya shirika hilo ‘kununua’ ekari moja kwa Sh800 milioni kutoka Azimio haikubaliki
Hata mradi wa Arumeru, NSSF pia imebainika kufuja fedha kutokana na kukubali kununua ekari moja kwa Sh1.8 bilioni, kinyume na thamani halisi ya viwanja kwenye eneo ambalo lipo kilometa 30 kutoka Jiji la Arusha. Uchunguzi umebaini wenyeji wa eneo hilo wanauza ekari moja kwa bei kati ya Sh500, 000 na Sh1 milioni.
Hatua ya NSSF ‘kununua’ ekari 300 Kigamboni kila moja kwa Sh800 milioni imesababisha hasara ya Sh179 bilioni na ekari 655.3 Arumeru kununuliwa kila moja kwa Sh1.8 bilioni imeingiza hasara ya Sh1.165 trilioni. Kwa hiyo, miradi miwili hiyo imeingiza hasara ya Sh1.3 trilioni.
“Tusubiri, lakini nina uhakika watu ambao kwa uzembe, walilishauri shirika kuingia kwenye matatizo haya na kuhatarisha fedha za wanachama lazima watawajibishwa ili kuepusha matatizo mengine yajayo kwa fedha za wanachama wa mfuko,” alisema ofisa huyo.
Ofisa huyo alisema kwamba hadi ukaguzi ulipofanyika shughuli zote hata manunuzi ya vitu muhimu kwa ajili ya mkandarasi zilikuwa zinafanywa na NSSF pamoja na mawasiliano na wasambazaji wa huduma. Hadi wakati wa ukaguzi, NSSF ilikuwa imeingiza kwenye mradi Sh205.141 bilioni na hazikuwapo nyaraka zilizoonyesha mchango wa Azimio mbali ya ardhi.
Kauli ya NSSF
Mwananchi lilifanya juhudi kupata ufafanuzi kutoka NSSF kwa zaidi ya mwezi moja lakini majibu hayakuridhisha. Kwanza liliambiwa shirika hilo halikuwa na Mkurugenzi Mkuu tangu Februari 15 baada ya Dk Dau kuteuliwa kuwa balozi.
Alipofuatwa Mkurugenzi wa Mipango na Uwekezaji wa Miradi wa NSSF, Yacoub Kidula alitaka apelekewe maswali ili ajibu kwa maandishi. Alipopelekewa maswali kwa maandishi alitaka yaandikwe kwenye karatasi yenye jina la kampuni na namba ya kumbukumbu. Baada ya kukamilisha takwa hilo, Kidula aliipeleka barua hiyo kwa Mhandisi Julius Nyamhokya ambaye ni Mkurugenzi wa Hifadhi Builders.
Baada ya wiki kadhaa za kufuatilia majibu, baadaye barua ilipelekwa kwa Mkurugenzi wa Mawasiliano, Eunice Chiume ambaye alisema hawezi kuijibu kwa kuwa bado ofisi hiyo haikuwa na mkurugenzi mkuu.
“Endeleeni kuwa wavumilivu kwa sababu sisi hatuwezi kuzungumza chochote bila kuwa na mkurugenzi mkuu. Tukimpata atajibu kwa sababu taratibu za ofisi zetu ni kuwa mkurugenzi mkuu ndiye mwenye majibu ya kila kitu,” alisema Chiume.
Rais John Magufuli alipomteua, Profesa Godius Kahyarara kuwa Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, bado majibu hayakutolewa. Chiume alisema Profesa Kahyarara bado anajifunza mazingira ya shirika.
Mkurugenzi wa Mradi wa Kampuni ya Azimio, Vital Dege alisema mradi unaendelea na mpaka sasa nyumba 300 tayari zimekamilika. “Mradi haujasimama, bado unaendelea na sasa tupo kwenye hatua za mwisho,” alisema Dege.
Lakini Mwananchi lilipotembelea eneo la mradi huo hivi karibuni, lilishuhudia shughuli zikiwa zimesimama; walikuwapo wafanyakazi wachache, wengi wao walinzi kutoka kampuni ya Usalama Corps na wajenzi kadhaa wa kampuni ya Uturuki ya M/s Mutluhan. Vibarua wote, mafundi na wataalamu mbalimbali hawakuwapo.
Walinzi wawili walionekana kwenye vibanda vya juu wakilinda majengo yaliyobaki kama magofu. Pia, walionekana walinzi wengine wanne ambapo wawili walikuwa kwenye lango kuu la kuingilia eneo lenye ofisi, mashine za kutengenezea nondo na kokoto huku wengine wawili wakiwa kwenye lango la kuingilia kwenye mradi.
“Ujenzi umesimama, kama ungekuwa unafanya kazi, nisingeweza hata kuzungumza na wewe, ningekuwa na kazi kubwa ya kupekua watu na kukagua magari yanayotoka nje na kuruhusu yanayoingia. Hapa pote pangekuwa vurugu tupu, hawa wanaingia hawa wanatoka. Kule (anaonyesha kwa kidole) kungekuwa na kelele za mashine za kokoto na nondo,” alisema mmoja wa walinzi wawili katika lango kuu la kuingia kwenye eneo la ofisi.
“Tumebaki walinzi tu na wasimamizi wachache. Wapo wajenzi wachache Waturuki, naona nao wanasubiri kuondoka.”
Ofisa masoko wa kampuni ya Hifadhi Builders, Alphonce Kayombo aliyekutwa eneo la mradi alisema mradi huo ulioko katika hatua ya pili ya ujenzi, umesimama kwa muda kutokana na alichodai wajenzi kwenda likizo.
“Mradi kwa sasa umesimama kwa sababu Waturuki waliopewa kazi ya ujenzi wamekwenda likizo. Watakaporudi wataendelea na ujenzi mwezi wa nne kumalizia hatua ya tatu na ya mwisho ili mradi uwe umekamilika ifikapo mwaka 2018,” alisema Kayombo.
No comments :
Post a Comment