Kigwangalla aiomba IAEA kuchangia ununuzi mashine ya saratani nchini
Ombi hilo lilitolewa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Dk Hamisi Kigwangalla, alipokutana na Ofisa Miradi wa IAEA Barani Afrika, Solomon Haile, jijini Dar es Salaam jana.
Katika makubaliano yaliyofikiwa miaka mitatu iliyopita, Mkurugenzi wa IAEA, Yukiko Amano, alimuahidi Waziri Mkuu wa wakati huo, Mizengo Pinda, kuwa wakala huo utachangia ununuzi wa Linac.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Tanzania ilipaswa kutoa nusu ya gharama ya Sh. bilioni nne na kiasi kingine kama hicho kingetolewa na IAEA.
Hata hivyo, Tanzania ilichelewa kukidhi mahitaji kadhaa yaliyoainishwa kwenye mradi huo, hivyo IAEA kufuta mchango wake.
Dk Kigwangalla alisema serikali imeshaikabidhi Taasisi ya Saratani ya Ocean Road Sh. bilioni nne, hivyo kuiomba IAEA kuchangia Sh. bilioni nne iliyoahidi.
Alisema ununuzi wa mashine hiyo utasaidia kuboresha huduma za tiba ya mionzi nchini.
Hata hivyo, akijibu rai ya Dk Kigwangalla, Haile alisema atawasilisha ombi hilo makao Makuu ya IAEA huko Vienna, Austria na uamuzi utapatikana baada ya wiki moja.
Wengine walikuhudhuria kikao hicho kutoka wizarani ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Tiba (magonjwa yasiyoambukiza), Profesa Ayoub Magimba, Mratibu wa Saratani na magonjwa yasiyoambukiza kwa watu wazima, Dk. Sara Maongezi na Kaimu Mkurugenzi taasisi ya saratani ya Ocean Road, Dk. Julius Mwaiselage.
No comments :
Post a Comment