Rais John Magufuli akiwa na Waziri Mkuu Mstaafu wa Kenya, Raila Odinga wakisali katika Kanisa la Bikira Maria, Parokia ya Chato mkoani Geita jana. Picha na Ukulu
Chato. Waziri mkuu mstaafu wa Kenya, Raila Odinga amesema Rais John Magufuli atakumbana na vikwazo na majaribu mengi katika mapambano dhidi ya ufisadi, rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma, hivyo anatakiwa kumtumainia Mungu.
Akizungumza na waumini wa Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria mjini Chato jana, Raila ambaye pia ni kiongozi wa muungano wa vyama vya upinzani wa Cord, alifananisha majaribu atakayokutana nayo Rais Magufuli kuwa ni sawa na yaliyompata Yesu Kristo, ambaye licha ya kupingwa na watu wake, pia alijaribiwa mlimani na shetani.
“Unatakiwa kusimama imara na kumtumaini Mungu kwa sababu utakumbana na majaribu mengi kama aliyoyapata Yesu Kristo akiwa mlimani alipojaribiwa na shetani,” alisema Raila.
Kiongozi huyo aliyeambatana na mkewe Ida na binti yao, Winnie Odinga wako Chato tangu juzi baada ya kuwasili kwa chopa wakiwa wageni wa familia ya Rais Magufuli aliyeko mapunzikoni.
Huku akimuangalia Rais Magufuli ambaye pia alihudhuria misa hiyo pamoja na mkewe Janeth, Raila alisema: “Jambo muhimu na la msingi nakusihi usimamie ukweli na haki katika utendaji wako.”
Ushirikiano EAC na utanzania wake
Akizungumzia ushirikiano katika ukanda wa Afrika Mashariki, Raila alisema umejengwa katika misingi ya utu, undugu na historia ya mataifa hayo kabla na baada ya ukombozi, akitolea mfano wake yeye alivyotumia hati ya kusafiria ya Tanzania kwa miaka mitatu baada ya Serikali ya kikoloni kumnyima hati ya Kenya.
“Mwalimu Julius Nyerere alijitoa mhanga kupigania uhuru wa mataifa mengine ya Afrika ikiwamo Kenya, natamani kuona umoja wa Afrika Mashariki ukiimarika kutimiza ndoto ya waasisi wa nchi hizi waliopigania uhuru na kuimarisha umoja wao,” alisema Raila.
Alisema bado anakumbuka urafiki wa kweli kati ya baba yake , marehemu Mzee Oginga Odinga na Mwalimu Nyerere aliosema unamfanya kujihisi Mtanzania, licha ya kuwa raia wa Kenya.
Urafiki wake na Magufuli
Kuhusu urafiki wake na Rais Magufuli, kiongozi huyo wa upinzani nchini Kenya alisema: “Urafiki wetu ulianza tangu Mheshimiwa Magufuli alipokuwa Waziri wa Ujenzi na mimi nikiwa na wadhifa huo nchini Kenya ambapo tulibadilishana uzoefu na kushirikiana katika mipango na miradi ya ujenzi wa barabara.”
Magufuli achanga Sh10 milioni, atishia kutumbua jipu
Rais Magufuli aliwataka Watanzania wote kufanya kazi kwa bidii ili kujenga Taifa lao huku wakiepuka ubaguzi wa aina yoyote miongoni mwao.
“Tuongozwe na mioyo ya mshikamano, upendo na ushirikiano huku tukimtanguliza Mungu kwenye kila jambo; tuepuke kubaguana kidini, kikabila wala kiitikadi huku tukiliombea Taifa letu liendelee kudumu kwenye amani, utulivu na mshikamano,” alisema Rais Magufuli
Rais alichangia Sh10 milioni kusaidia upanuzi wa kanisa hilo linalokaribia kusherehekea miaka 50 tangu lijengwe, huku akiutaka uongozi kutumia vema mchango huo akitishia kutumbua majipu iwapo atafuatilia na kubaini matumizi mabaya ya fedha hizo.
“Baba Paroko, nachangia Sh10 milioni kwenye ujenzi wa kanisa, lakini mzitumie vizuri nisije nikawatumbua nitakapofuatilia matumizi yake,” alisema Rais Magufuli huku akishangiliwa na waumini.
Kama alivyosema Raila, Rais Magufuli alisema urafiki wao umevuka viwango vya urafiki na kufikia undugu na kubainisha siyo mara ya kwanza wao kutembeleana kifamilia.
“Hata kwenye msiba wa marehemu baba yangu, Raila alikuja na kukaa Chato siku mbili, huyu ni rafiki wa kweli na tumesaidiana katika mambo mengi, naomba wana Chato mmtambue kama mtoto wa Chato,” alisema Rais Magufuli, ambaye mwishoni mwa wiki alitangaza mshahara wake kuwa ni Sh9.5 milioni.
No comments :
Post a Comment