Hiyo inatokana na kinachodaiwa kuwa ni ukosefu wa dawa ya usingizi, ambayo hutumika katika chumba cha upasuaji. Walidai kwamba hali sio nzuri kutokana na umuhimu wa tiba hiyo, ambayo imeshindwa kutolewa kwa wagonjwa kuanzia Desemba 28 mwaka huu.
Baadhi ya wagonjwa waliozungumza hospitalini hapo jana na mwandishi kwa sharti la kutotajwa majina yao, kwa kuhofia usalama wa afya zao, walidai kwamba mgonjwa wa mwisho kufanyiwa upasuaji, alifanyiwa juzi mchana. Kwamba wagonjwa wengine, wanalazimika kuendelea kusubiri wodini bila matumaini.“Mimi ni mmoja wa wagonjwa waliokuwa wameshaandaliwa kupata matibabu haya na hapa unaponiona sijaruhusiwa kula chakula tangu hiyo jana (juzi) alasiri na tayari nimeshawekewa mpira wa haja ndogo (lathers) wakati mwenzetu wa mwisho alipofanyiwa upasuaji na dawa kuisha, “ alisema mgonjwa huyo.
Mgonjwa mwingine anayesubiri tiba hiyo, alisema usiku wa kuamkia jana kulijitokeza watoto wawili waliokuwa wakihitaji kufanyiwa upasuaji kwa dharura kutokana na matatizo yaliyokuwa yakiwakabili, lakini pamoja na madaktari kufika hospitalini hapo, hawajaweza kupata matibabu mpaka asubuhi.
Hata hivyo, juhudi za kupata Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Asha Mahita ili kuzungumzia kadhia hiyo, hazikufanikiwa baada ya kudai kwamba muda huo alikuwa katika majukumu mengine na pia taarifa hiyo ndio anaisikia kwa mara ya kwanza kutoka kwa waandishi wa habari.
Dk Mahita aliwaambia waandishi wa habari kuwa atalifanyia kazi suala hilo ili kujua kulikoni. Wakati huo huo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu jana alikuwa mkoani Tanga kwa ziara ya kikazi wilayani Muheza.
Akiwa katika ofisi ndogo ya kituo cha Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) eneo la Ubwari wilayani humo, Ummy baada ya kupokea taarifa, aliombwa na waandishi kufanya mahojiano ili kuzungumzia tatizo hilo, alisema hana muda wa kutosha kufanya hivyo kwa kuwa anaelekea katika vikao vya chama.
No comments :
Post a Comment