dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Saturday, December 17, 2016

WANA-DIASPORA WAKIZANZIBARI (ZAGLODINET) WAMUANDIKIA WAZIRI WA ARDHI ZANZIBAR!

Wazanzibari waishio Ughaibuni wameamua kumkabili Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira wa Serikali ya Zanzibar Mheshimiwa Salama Aboud Talib, wakitaka ufafanuzi juu ya Sera mpya ya Ardhi Visiwani Zanzibar.


Image result for zanzibar city

Katika barua yao kwa Mheshimiwa Salama ambayo Swahilivilla imeipata nakala yake, Wazanzibari hao chini ya mwemvuli wa Zanzibar Global Diaspora Network (ZAGLODINET), wamemtaka Waziri huyo kutoa ufafanuzi zaidi juu ya Sera mpya ya Ardhi Visiwani humo.

"Yahusu Ombi la Ufafanuzi Juu ya Kanuni Mpya za Kuendeleza Na Kumiliki Ardhi Zanzibar" kilisema kichwa cha maneno cha barua ya ZAGLODINET ambayo inajumuisha jumuiya mabalimbali za Wazanzibari Waishio katika nchi tofauti Ulimwenguni.

Barua hiyo imefafanua kuwa lengo kubwa la mawasiliano hayo ni kuendeleza mahusiano mema baina ya Wazanzibari waishio Ughaibuni na Serikali za Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
" Kwa heshima na taadhima kubwa, tunaomba kupatiwa maelezo na ufafanuzi bayana kutoka kwako ili uhusiano mwema uliopo na masikilizano baina yetu --wanachama wa jumuiya za Wanadiaspora wa Kizanzibari duniani; Serikali zote mbili za Tanzania, yaani Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Muungano; pamoja na washiriki na wadau wengine tunaoshirikana nao walioko nyumbani na katika nchi tunzoishi; uendelee kubaki na kuzidi kustawi". Ilifafanua barua hiyo.

Imeendelea kuelezea umuhimu wa Wanadiaspora na mchango wao mkubwa wanaoutoa katika kusaidia harakati za maendeleo katika nyanja tofauti Visiwani Zanzibar zikiwemo Elimu, Afya, Dini na nyenginezo.

"Tokea zamani hata kabla ya kuanzishwa kwa ZAGLODINET, vikundi mbali mbali vya Wazanzibari kutoka kila mahali, jumuiya nyengine zenye malengo maaalum ya kusaidia, pamoja na maelfu ya watu binafsi kutoka mataifa mbalimbali wenye kupenda kusaidia juhudi za Wanadiapora, wamekuwa wakijituma kwa namna mbali mbali bila kuchoka kutafuta kila njia za kusaidia". Ilisisitiza barua hiyo na kuongeza: "Maelefu ya Wazanzibari wanyonge wenye vipato vya chini na wale wasiojiweza wamefaidika na wanaendelea kufaidika kwa kiasi kikubwa kutokana na misaada ya aina hii kutoka kwa ndugu zao walioko nje".


Aidha, barua hiyo imekumbushia jinsi ambavyo Wanadiaspora wamekuwa wakishiriki katika mikutano na makongamano mbalimbali iliyoandaliwa na serikali za Tanzania na Zanzibar kwa ajili ya kudumisha mahusiano mema na kuweka misingi madhubuti na inayoeleweka ya kuwawezesha Wazanzibari wanaoishi Ng'ambo kushiriki kikamilifu katika kusaidia kuinua hali za kijamii na kiuchumi za nchi zao.

Kwa mujibu wa barua hiyo, katika mikutano hiyo, serikali zote mbili zimekuwa zikiwahimiza Wanadiaspora kuwekeza nyumbani katika sekta tofauti, ikiwemo ya ujenzi wa nyumba, huku zikiwahakikishia kuwawekea Wanadiaspora hao mazingira mazuri pamoja na sheria maridhawa ili kuhakikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo na uwekezaji.

" Mara kwa mara, viongozi wetu wamekuwa wakitushadidia na kutuhimiza juu ya kuendelea kukuza uzalendo wa Kizanzibari kwa njia mbalimbali zikiwemo ujenzi wa nyumba za kuishi, miradi ya kilimo, biashara pamoja na kuweka vitega uchumi vya aina tofauti. Serikali zetu zilituhakikishia kwamba zingefanya kila linalowezekana kutengeneza mazingira muafaka kwa kuweka sheria zinazohusika, miundombinu kabambe pamoja na sera maridhawa ili kurahisisha utekelezaji wa miradi ya kimaendeleo na uwekezaji", ulikumbushia waraka huo ambao nakala zake zimetumwa kwa Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais wa Zanzibar na Waziri wa Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Zanzibar.

Itafaa kukumbusha kuwa, Waziri wa Ardhi Zanzibar Mheshimiwa Salama Aboud Talib, hivi karibuni alitoa tangazo linaloelezea sera mpya ya umiliki wa ardhi visiwani humo.

Katika tangazo hilo ambalo Swahilivilla ilifanikiwa kunasa sauti yake, Waziri Salama alielezea kanuni za umilikaji wa ardhi zilizojumuisha kuchukuliwa kwa viwanja na serikali ya Zanizbar kote Unguja na Pemba ifikapo Februari 2017; iwapo wawekezaji wa viwanja hivyo watashindwa kuviendeleza, kwa madai ya kutunza mandhari na mipangilio ya miji.

Tangazo hilo lilipelekea hamkani kuwa si shwari tena na kuzusha mtafaruku miongoni mwa Wanadiaspora, na hivyo kupelekea vikundi na jumuiya mbalimbali za wahajiri hao kukutana ili kutafakari hatua za kuchukua kwa ajili ya kunusuru mali na vitegauchumi vyao.

"Jumuia mbali mbali zinazounda ZAGLODINET pamoja na wafuasi wao, kwa heshima na unyenyekevu, wanaomba kuleta mbele yako suala linalohusu tangazo kutoka ofisi yako juu ya sheria mpya za uendelezaji na umilikaji wa ardhi huko Zanzibar ambazo tumezipata kupitia mitandao ya kijamii. Mpaka sasa tangazo hilo linatupa wasiwasi na limekuwa ni kitadawili kwetu", ilisihi barua ya Wanadiaspora, na kuelezea majonzi yao kwa kusema: " Tuna wingi wa masikitiko kukufahamisha kuwa kutokana na tangazo lile, wengi wa Wazanzibari wanaoishi nje wamegubikwa na simanzi na kuchanganyikiwa kutokana na hali tete ya mustakbali wa mali na vitega uchumi vyao huko nyumbani".

Barua hiyo ambayo nakala zake zimetumwa pia kwa Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora Zanzibar na Mkurugenzi wa Idara ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), imemalizia kwa kuelezea matumaini ya Wanadiaspora kuwa swala hilo litapatiwa ufafanuzi kwa muda mwafaka ili kuwapa faraja, huku ikitiliwa maanani kuwa muda uliotolewa katika tangazo la Mheshimiwa Waziri wa Ardhi unazidi kuyoyoma.

"Tuna imani kubwa sana kwako ya kuwa utatumia busara zako kwa kadiri itakavyowezekana na kwa muda muwafaka kutoa ufafanuzi ulio bayana juu ya kauli iliyotolewa na Wizaya yako iliyogusa hisia za watu wengi ili kuwatoa wasiwasi Wazanzibari hao", ilikhitimisha.

Hadi tunaingia mitamboni, juhudi za Swahilivilla za kumpata Waziri wa Ardhi Zanzibar kutoa ufafanuzi kukhusu barua hiyo, hazikufua dafu.


No comments :

Post a Comment