Dar es Salaam. Siku moja baada ya Rais wa Awamu ya Pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi kuitaka Mahakama kutoa haki kwa wakati bila kuingiliwa, wanasheria na wanasiasa kutoka vyama mbalimbali wamepongeza kauli hiyo na kueleza kuwa amegusa hali halisi.
Akizindua maadhimisho ya Wiki ya Sheria na Utoaji Elimu ya Sheria Dar es Salaam juzi, Mzee Mwinyi alisema, “Ili Mahakama iheshimike, haina budi kutoa haki kwa wakati bila kuingiliwa na mtu au chombo chochote. Mahakama inatakiwa kudumisha nidhamu na kuzingatia maadili ya uhakimu na ujaji.”
Mzee Mwinyi alisema wakati akiwa Rais, alikuwa akipokea malalamiko ya watu wengi ambao walikuwa hawaridhiki na uamuzi wa Mahakama.Akizungumzia kauli hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Zanzibar), Vuai Ali Vuai alisema kauli ya Mzee Mwinyi ni kusisitiza haki katika chombo hicho cha sheria kwani huo ndiyo utaratibu, “Mahakama inatakiwa kuwa huru kwa mujibu wa sheria.”
Alisema uhuru wa Mahakama utaendelea kuheshimika endapo itaonekana inatenda haki kwa vitendo.
Mbunge wa Singida Mashariki na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alisema Mzee Mwinyi amezungumza jambo lenye uzito na maana kubwa. Alisema baadhi ya uamuzi unaotolewa na Mahakama hautendi haki kama inavyotakiwa kuwa.
Lissu alisema mhimili huo unashindwa kutekeleza jukumu lake la kuisimamia Serikali ipasavyo.
Alisema katika nchi nyingi zilizoingia kwenye machafuko chanzo kikubwa kilikuwa mahakama kushindwa kutenda haki. “Mahakama inatakiwa itetee haki za wanyonge siyo kuibeba serikali, tutafika mahali watu watapoteza imani na vyombo vya sheria na hapo ndipo watakapojitosa kuchukua sheria mkononi,” alisema Lissu.
Hata hivyo, Mhadhiri Mwandamizi wa Kitivo cha Sheria, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Onesmo Kyauke alitofautiana na Lissu akisema anaamini Mahakama za Tanzania ziko huru ikilinganishwa na nchi nyingine, licha ya kuwapo kwa changamoto kadhaa.
Pamoja na hayo, ili kuondoa mazingira kuwa Mahakama inaingiliwa, Dk Kyauke alishauri iwepo sheria itakayozuia watendaji wa ngazi za juu wa chombo hicho kupewa kazi serikalini.
“Si vizuri sana kwa majaji kuteuliwa kwenye nafasi serikalini mfano Msajili wa Vyama vya Siasa, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwani wakati mwingine inaweza kutengeneza mazingira kwa majaji wengine kufanya mambo ya kuifurahisha Serikali ili wapate nafasi hizo.
Suala la mishahara ya mahakimu nalo liangaliwe vizuri ili kusiwepo na mazingira ya rushwa na itengwe bajeti ya Mahakama sio kutegemea fedha kutoka serikalini. Ikiwezana hata asilimia tano ya bajeti kuu ielekezwe kwenye Mahakama.
Lakini Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha CUF na Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya alisema kuwa mfumo wa Mahakama Tanzania unapaswa kubadilika.
Alisema kwa nafasi aliyonayo Mzee Mwinyi, huenda ameona vitendo viovu vinavyofanywa na baadhi ya mahakama lakini viongozi wengine wanashindwa kuzungumzia.
“Mahakama inapaswa kuwa kimbilio la wananchi wanyonge ili waweze kupata haki, lakini mambo yamebadilika sasa rushwa inatumika kwa kiasi kikubwa kwenye utoaji wa maamuzi. Ukitaka kujua haya uwe unakutana na wananchi wa chini kabisa ndiyo utajua kuna kesi nyingi zinazoamuliwa kwa uonevu.”
Kauli ya kuonya Mahakama isiingiliwe pia ilitolewa na Wakili wa Crax Law Partners, Hamza Jabir, “Alichokisema Mzee Mwinyi ni kitu muhimu. Mahakama inatakiwa kuwa huru kama kuna mazingira ya kuingiliwa basi yaachwe mara moja maana itasababisha haki isitendeke.
Mahakama haitakiwi kuendeshwa kisiasa. Suala likishakuwa mahakamani halitakiwi kujadiliwa nje ya Mahakama na wasimamizi wa kesi wasiingiliwe.”
Katibu Mkuu wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Danda Juju alisema mhimili huo umeshindwa kufanya kazi yake inavyostahili kutokana na kuingiliwa na Serikali.
No comments :
Post a Comment