Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kati kati akiangalia nyumba ya Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana iliyoporomoka ukuta wa mbele baada ya kufanya ziara fupi ya kuangalia mkasa huo uliosababisha kifo cha Mtu Mmoja.
Balozi Seif wa Pili kutoka Kushoto akimuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Uhifadhi na Utunzaji wa Mji Mkongwe wa Zanzibar Nd. Issa Sarboko Makarani wa kwanza kushoto kufanya ukaguzi wa Nyumba zilizomo ndani ya Mjui huo ili punguza maafa yanayoweza kuepukwa mapema.
Kushoto ya Balozi Seif ni Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Ayoub Mohamed Mahmoud na Mkuu wa Wilaya ya Mjini Nd. Marina Joel Thomas.
Nyumba ya Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana ikionekena kuharibika vibaya baada ya ukuta we mbele kunyofoka mapema asubuhi ya Jumatano wakati mafundi wakiwa kazini.
Eneo la juu la nyumba ya Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Zanzibar iliyopo Hurumzi ambalo lililonyofoka upande wa mbele na kusababisha kifo cha Mtu Mmoja aliyekuwa miongoni mwa Mafundi Wanne waliokuwa wakiendelea na matengenezo makubwa ya Nyumba hiyo.
Na Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameuagiza Uongozi wa Mamlaka ya Uhifadhi na Utunzaji wa Mji Mkongwe wa Zanzibar kuandaa mpango maalum utakaoshirikisha Taasisi nyengine husika kwa ajili ya kuzifanyia ukaguzi wa mara kwa mara nyumba zote zilizomo ndani ya Mji huo.
Alisema mpango huo wa Kitaalamu utaweza kutoa muelekeo wa kina kwa kuzitambua nyumba zote zilizochakaa na ambazo kwa mazingira ya Mji huo haziwezi tena kuhudumia makaazi ya Wananchi wake.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa agizo hilo mapema asubuhi alipofanya ziara fupi ya kulikagua Jengo la Ghorofa Tatu la Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana katika Mtaa wa Hurumzi ndani ya Mji Mkongwe wa Zanzibar baada ya kuporomoka wakati mafundi wakiwa katika harakati za kulifanyia matengenezo makubwa.
Maporomoko hayo yaliyomfunika Fundi Mmoja aliyetambuliwa kwa jina la Khamis Kombo yalisababisha kifo chake kilichothibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa Mjini Magharibi na Fundi mwengine kulazwa Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja baada ya kujeruhiwa vibaya.
Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kamwe haitovumilia kuona Wananchi wake wanaendelea kuishi katika mazingira hatarishi ndani ya nyumba ambazo itathibitishwa na Uongozi na Wataalamu hao wa Mamlaka ya Mji Mkongwe kwamba hazistahiki kuishi Wanaadamu.
Mapema Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Uhifadhi na Utunzaji wa Mji Mkongwe wa Zanzibar Nd. Issa Sarboko Makarani alisema Uongozi wa Mamlaka hiyo pamoja na ule wa Shirika la Nyumba Zanzibar uko katika hatua ya mwisho ya kufanya mazungumzo ili Wataalamu wake wafanye zoezi maalum la kuzikagua nyumba zote za Serikali zilizomo ndani ya Mji huo.
Nd. Sarboko alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba zoezi hilo litabainisha wazi Ngumba zilizoharibika kabisa na kuwa katika mazingira hatarishi jambo ambalo juhudi za makusudi zitachukuliwa katika kuona lile fungu dogo la fedha linalopatikana lielekezwe katika kuziokoa kwanza nyumba hizo.
“ Tunatarajia kuwa na zoezi la pamoja kati yetu sisi watu wa mamlaka ya Mji Mkongwe na wenzetu wa Shirika la Nyumba Zanzibar kuzikaguwa ili tuzitambue nyumba za Serikali zilizo katika hali mbaya na baadaye kuzifanyia matengenezo ya dharura ”. Alisema Nd. Issa Sarboko Makarani.
Naye kwa upande wake Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Ayoub Mohamed Mahmoud alisema Uongozi wa Serikali ya Mkoa wake hautokubali kuridhia malalamiko yanayotolewa na yatakayoendelea kutolewa na baadhi ya watu dhidi ya Serikali kwa uamuzi wake wa kuhami maisha ya wananchi wake.
Mheshimiwa Ayoub alisema jambo la msingi litakaloendelea kuchukuliwa na kutiliwa mkazo na Serikali ni dhima ya kuhami uhai wa maisha ya Raia wakati panapojitokeza dalili za maafa bila ya kujali kasumba za kisiasa zinazopigiwa debe na baadhi ya watu wakiwepo pia wanasiasa.
Ujenzi wa jengo hilo la Ghorofa Tatu Mali ya Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Zanzibar ulikuwa unafanyika kwa mujibu wa sheria na taratibu zote za mamlaka ya Uhifadhi na Utunzaji wa Mji ya mkongwe wa Zanzibar.
Kikosi cha zimamoto na Uokozi Zanzibar kilifika katika eneo la tukio mara baada ya kuanguka kwa ukuta wa mbele wa Nyumba hiyo na kujaribu kumuokoa fundi aliyefukiwa na kifusi ambae tayari alikuwa ameshafariki Dunia na maiti yake kupelekwa hospitali kuu ya Mnazimoja kwa uchunguzi kabla ya kukabidhiwa familia kwa ajili ya mazishi.
No comments :
Post a Comment