Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiiongoza Timu ya Mawaziri na Makatibu Wakuu kutembelea maeneo ya uchimbaji mchanga yaliyomo ndani ya Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Kulia ya Balozi Seif ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed, kushoto yake ni Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mh. Vuai Mwinyi, Nyuma ya Balozi Seif kushoto ni Waziri anayesimamia Tawala za Mikoa Mh. Haji Omar Kheir na Waziri wa Kilimo Mh. Hamad Rashid.
Balozi Seif akizungumza na baadhi ya wamiliki wa maeneo waliyoomba kibali kwa ajili ya kutaka kuchimba mchanga katika Kijiji cha Donge Kipange.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Maliasili, Mifugo na Uvuvi Nd. Juma Ali Juma akitoa ufafanuzi mbele ya Timu ya Mawaziri iliyoongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzbar Balozi Seif huko Donge Chechele.
Eneo la Hecta 14 liliopo katika Kijiji cha Donge Chechele ndio pekee lililobakia lenye mchanga mweupe katika Kisiwa cha Unguja.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Na Othman Khamis OMPR.
Harakati za ujenzi zilizopamba moto katika maeneo mbali mbali Mijini na Vijijini kutokana na ongezeko kubwa la Idadi ya Watu sambamba na ujenzi holela usiozingatia mipango Miji ni miongoni mwa masuala yanayotishia uchafuzi mkubwa wa mazingira hapa Nchini.
Kasi kubwa ya uchimbwaji wa mchanga katika vitalu tofauti vya rasilmali hiyo ili kukidhi mahitaji hayo ya ujenzi imepelekea Serikali Kuu kusitisha zoezi hilo kwa muda ili kukamilisha utaratibu sahihi kutokana na athari kubwa iliyokwisha jitokeza kwenye maeneo yaliyochimbwa mchanga.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiiongoza Timu ya Mawaziri, Manaibu Mawaziri, Makatibu Wakuu pamoja na Wataalamu wa Taasisi zinazosimamia mazingira, misitu na Ardhi walifanya ziara maalum ya kutembelea maeneo yaliyokwisha athirika na kadhia hiyo.
Ziara hiyo ilijumuisha pia maeneo ya ardhi ya Donge Kipange, Donge Mchangani, Donge chechele na Pangatupu ambayo wamiliki wake binafsi wameshapeleka maombi yao kwa ajili ya kuruhusiwa kuchimba mchanga ili kukidhi mahitaji yao ya kimaisha.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Maliasili, Mifugo na Uvuvi Nd. Juma Ali Juma aliieleza Timu hiyo ya Viongozi Wakuu kwamba kipande pekee cha ardhi chenye ukubwa wa Hekta 14 kiliopo katika kijiji cha Chechele ndicho kilichobakia cha mchanga bora wa kujengea ndani ya Kisiwa cha Unguja.
Ndugu Juma alisemaTimu ya Makatibu Wakuu iliyopewa jukumu la kufanya utafiti wa kuelewa maeneo yaliyoathirika na yaliyobaki kwa kushirikisha wataalamu wa Masuala ya Mazingira, Misitu na Ardhi imethibitisha kwamba hivi sasa zipo hekta 137 pekee zilizobakia kwa ajili ya kuchimbwa mchanga katika kisiwa cha Unguja zilizopo katika Kijiji cha Pangatupu.
Alisema timu hiyo hivi sasa inakamilisha ripoti ya utafiti huo na kutoa ushauri pamoja na mapendekezo na baadae kuyapeleka Serikalini kwa lengo la kuchukuliwa hatua zitakazofaa kufuatwa hapo baadae.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Ardhi na Usajili Zanzibar Nd. Said Salim Afuso alisema maeneo mengi yaliyochimbwa mchanga yangeweza kurejea katika uhalisia wake ndani ya miaka miwili iwapo uchimbaji uliofanywa kabla ungezingatia Kanuni za Mazingira.
Nd. Saidi alisema Kanuni hizo Nane zinaelekeza uchimbaji wa mchanga usiozidi Mita mbili kwenda chini, upandati miti baada ya kukamilika kwa zoezi la uchimbaji mchanga, eneo husika liwe na umbali na makaazi ya watu na usawa wa Bahari kwa urefu usiopungua Mita 500.
Mkurugenzi huyo wa Idara ya Ardhi na Usajili alifafanua kwamba maeneo yote ya Ardhi yaliyomo ndani ya Visiwa vya Zanzibar tayari yameshapimwa na kuwekewa utaratibu wa matumizi kulingana na hali halisi iliyopo ya mazingira.
Hata hivyo ameeleza kwamba baadhi ya maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za kuendeleza Kilimo yameshavamiwa kwa harakati za ujenzi wa makaazi ya kudumu na mengine kuchimbwa mchanga.
Kwa upande wao Wananchi wanaomiliki maeneo yanayotaka kuchimbwa mchanga wakisubiri kupata kibali kufuatia maombi waliyopeleka wameieleza Timu hiyo ya Viongozi Wakuu kwamba wamefikia hatua hiyo baada ya maeneo yao kukosa sifa za kuyaendeleza kwa shughuli za Kilimo.
Mzee Ali Songoro wa Donge Kipange, Mzee Aziz Khamis Aziz wa Kijiji cha Donge Mchangani na Bwana Makungu Khamis wa Kijiji cha Pangatupu kwa nyakati tofauti walisema ukosefu wa rutba, wizi uliokithiri sambamba na ufugaji Holela kwenye mashamba yao umechangia kukosa kuendelezwa kilimo kwenye maeneo hayo.
No comments :
Post a Comment