Hili blog ni kuhusu Tanzania na dunia nzima kwa ujumla. Pita kila siku kwa habari moto moto. (This blog is about Tanzania and the world as a whole. Pass-by everyday for breaking news). ***********************KARIBUNI NYOTE / YOU ARE ALL WELCOME!***********************
Tuesday, March 7, 2017
Kwenye orodha ya Makonda vigogo watano wahojiwa!
MAMLAKA ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya inawashikilia, kuwahoji na kuwachunguza vigogo watano walio katika orodha ya watu 97 wanaodaiwa kuhusika na biashara hiyo, waliokabidhiwa na serikali ya mkoa wa Dar es Salaam.
Hatua hiyo ilibainishwa jana jijini humo na Kamishna wa Intelijensia wa mamlaka hiyo, Fredrick Kibuta, wakati wa uzinduzi wa ripoti ya mwaka 2016 ya Umoja wa Mataifa (UN) ya kuzuia na kupambana na dawa za kulevya.
Ufafanuzi huo ulikuja baada ya waandishi wa habari kutaka kujua hatua zilizochukuliwa baada ya mamlaka kukabidhiwa orodha hiyo mapema mwezi uliopita.
Majina ya wanaodaiwa kuwa ni vigogo, watoto wa viongozi na wafanyabiashara wakubwa wa mihadarati ilikabidhiwa kwa Kamishana Mkuu wa Mamlaka, Rogers Sianga na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, siku mbili baada ya kuteuliwa na Rais John Magufuli, Februari 10.
Majina hayo, alidai Makonda, ni ya watu wanaohusika na biashara ya mihadarati tangu utawala wa awamu ya pili hadi ya tano.
“Tumekamata watu watano ambao ni muhimu sana katika mapambano ya dawa za kulevya, na wengine wengi tunawahoji," alisema Kibuta. "Uchunguzi wetu unaendelea."
"Sisi hatutangazi, lakini kazi inaendelea.
“Kuna operesheni nyingi sana zinaendelea kwa sasa na zipo katika hatua tofauti tofauti za uchunguzi. Pia biashara hii ina uhusiano wa moja kwa moja na utakatishaji fedha.”
Awali, akizungumza mara baada ya kupokea ripoti hiyo, Kamishna Sianga alisema mapambano yanafanyika kwa njia kuu tatu ambazo ni kuzuia uingizwaji wake, kutoa elimu ili wananchi wakatae kutumia dawa hizo na kama imeshindikana, kuwasaidia waathirika wa dawa za kulevya kwa kuwapatia matibabu.
“Kuna wengine wametajwa kwenye orodha ni wagonjwa (watumiaji wa dawa), hatuwakamati ili tuwafunge maana tukifanya hivyo tutajaza magereza na haitasaidia," alisema Sianga.
"Tunawahoji watuonyeshe wanaowauzia ili kupata waingizaji na wao tunawapeleka kwenye tiba.”
Alisema jamii ya kimataifa ambayo nchi inajifunza huko, inaeleza kuwa watumiaji wa dawa za kulevya wanatazamwa kama wagonjwa wanaohitaji matibabu na msaada mkubwa, hivyo pamoja na kuwakamata wanapelekwa kwenye vituo vya kutibu watumiaji wa dawa vya Hospitali ya Rufani ya Temeke, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Hospitali ya Rufani ya Mwananyamala, zote za Dar es Salaam.
“Ripoti imesisitiza kuwa tuwatazame kama wenye kuhitaji msaada zaidi kuliko kuwatazama kama watu wa kukamata na kufunga," alisema.
"Wapo wengi mtaani na hata ukiwakamata na kuwajaza kwenye magereza haitasaidia bali tutawatibu.”
HATUA MADHUBUTI
Awali, Mwakilishi Mkazi wa UN, Alvaro Rodriguez, aliipongeza serikali kwa hatua madhubuti za kupambana na kuzuia dawa za kulevya nchini na kwamba jitihada hizo zimeleta mwamko kwenye jamii juu ya athari za dawa hizo.
“UN imejidhatiti katika mapambano haya. Ofisi yetu ya Makosa ya Jinai na Dawa za Kulevya (UNODC) na Mshirika ya Umoja huo wako mstari wa mbele kukabiliana na changamoto hii kwa kuwa na mfuko na programu ambao zimesaidia kupunguza umaskini na kusisitiza maendeleo endelevu,” alifafanua.
Rodriguez alisema mapambano ya dawa za kulevya yanazitaka nchi zote kuungana kutokana na ukweli kuwa upo uhusiano wa karibu wa makosa ya jinai, matokeo ya dawa ambayo yanahitaji huduma za afya na rushwa.
Alitaja changamoto zilizopo kuwa ni tamaduni na sheria tofauti za kupambana na dawa hizo huku akitolea mfano wa nchi jirani ya Kenya ambako matumizi ya mirungi yameruhusiwa wakati hapa yamekatazwa.
Mwakilishi huyo alisema Mkutano Mkuu wa 30 wa dunia katika kupambana na dawa za kulevya, ulitoa chapisho likionyesha maamuzi ya pamoja katika kupambana na dawa za kulevya, usafirishaji, matibabu na mambo yahusuyo matumizi mabaya ya kemikali za viwanda kuzalisha dawa za kulevya.
Alisema ripoti ya mwaka juzi ilieleza jinsi usafiri wa majini unatumika kufanikisha biashara hiyo, na kupongeza jitihada za nchi za ukanda wa Afrika Mashariki kwenye Pwani na mji wa Mombasa Kenya, kufanikiwa kupambana na uhalifu huo.
Mwezi uliopita, akiwaapisha Kamishna Sianga, Rais Magufuli alipigilia msumari wa mwisho katika mapambano hayo kwa kueleza kuwa vita hiyo itaendeshwa na serikali kwa mujibu wa sheria na kwamba Watanzania 1,007 wanaoshikiliwa kwenye magereza mbalimbali duniani, kwa mashtaka ya dawa za kulevya na wafungwa 68 waliohukumiwa kifo nchini China, serikali haitahusika kuwatetea.
Aidha, Rais Magufuli alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kutomuogopa mtu yeyote katika vita hiyo na hata ikiwa ni mkewe, Janet Magufuli, akamatwe bila ya kujali jina.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment